NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 4, 2012

Wananchi wamshambulia mbunge, diwani

WANANCHI wa maeneo ya Ipagala na Ilazo katika kata ya Ipaga Manispaa ya Dodoma wamemshambulia mbunge wao wa jimbo la Dodoma Mjini, David Mallole(CCM), pamoja na diwani wa kata ya Ipaga, Charles Mamba, kwa kutokuwa karibu na wananchi katika shughuli za kimaendeleo.
Walisema kuwa wanajuta kuwachagua viongozi hao kwani wanatumia muda mwingi kufanya kazi zao badala ya kuwa karibu na wananchi.
Wananchi hao walidai kuwa licha ya hivi karibuni kupata adha ya mvua iliyoambatana na upepo mkali hivyo kusababisha nyumba zaidi ya 100 kuezuliwa na kuwafanya wakazi hao kukosa mahali pa kuishi hakukuwa na kiongozi yeyote aliyekwenda kuwasaidia.
Walieleza kwa nyakati tofauti kwamba kata yao inakabiliwa na matatizo mbalimbali ikiwemo ukosefu wa miundombinu jambo ambalo linawasababishia wakazi wa maeneo ya Swaswa kutembea umbali mrefu kufuata daladala.
Mmoja wa wananchi ambaye alijitambulisha kwa jina la Haule Khamisi, alisema kuwa mbunge huyo amekuwa akilalamikiwa na wananchi kutokana na kutowatembelea na kusikiliza kero zao ili aziwasilishe bungeni.
“Tunajuta kumchagua Malole, tangu aingie bungeni hajawahi kuwasilisha matatizo yetu yanayotukabili katika kata yetu; barabara ni mbovu lakini zaidi angalia hata maafa haya ambayo yametukuta mbunge wala hana habari na pamoja na diwani wetu wanakaa mjini badala ya kufiki katika maeneo yao ya kazi.
Mwandishi wetu alimtafuta mbunge huyo kuweza kujibu tuhuma hizo hakuweza kupatikana lakini siku moja baada ya wananchi kutoa tuhuma hizo mbunge huyo alikwenda kuwatembelea baadhi ya wahanga ambao nyumba zao ziliezuliwa kutokana na mvua iliyoambatana na upepo ambayo ilinyesha katika kata ya Kinyoya, manispaa ya Dodoma.

No comments:

Post a Comment