NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 4, 2012

Hatujawahi kuiona Katiba Kilosa

KUTOFAHAMIKA kwa Katiba ya nchi kwa viongozi na wananchi vijijini kumetajwa kuwa chanzo cha migogoro mingi isiyoisha kadhalika ikichangia ongezeko la umaskini nchini.
Madai hayo yako kwenye majumuisho na maazimio ya mafunzo ya utawala bora yaliyoandaliwa na shirika la Mapinduzi Forum for Development (MFD) kwa ufadhili wa The Foundation for Civil Society kwa viongozi wa serikali ngazi ya vitongoji hadi kata wilayani Kilosa.
Wakitoa uzoefu wa utendaji wa wenyeviti, maafisa watendaji vijiji na kata kwenye mafunzo ya utawala bora kijijini Rudewa wilayani humo baadhi ya washiriki walibainisha kuwa migogoro mingi ikiwemo ya ardhi inachangiwa na kutoifahamu Katiba.
Oriva Robert na William Mell walibainisha kuwa baadhi ya migogoro, ikiwemo ya ardhi, inatokana na wananchi na viongozi katika ngazi zote ikianzia katika vitongoji hadi wilaya kutoifahamu Katiba yenyewe, kazi yake na faida yake.
“Kwa mfano binafsi sisi hapa tulipo hatuifahamu hata hiyo Katiba ina rangi gani na imezungumzia vitu gani kwa faida ya nani...lakini hata hivyo inatumika vipi kwa jamii,” alisema Oriva.
“Ombi letu serikali ilete na kuzisambaza bure kwa wananchi hizo Katiba lakini pia suala la elimu ya umuhimu wa Katiba katika maisha ya kila siku ya mwananchi itolewe ili wananchi wazisome kama magazeti,” alifafanua.
Walibainisha kuwa migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji itapungua, mipaka ya vijiji na mwingiliano wa maeneo ya makazi na shughuli za kijamii itatoweka kutokana na wananchi kuifahamu vema Katiba.
Aidha wameiomba serikali kuzitawanya sera mbalimbali zinazotumika sasa nchini kwenye ofisi za serikali za vijiji au kata ili wananchi weweze kuzipitia na kuhoji pale ambapo hazitakuwa zimetekelezwa.
Katika mada hiyo ya utawala bora, kaimu ofisa maendeleo ya jamii wilayani humo Aloyce Buhori alifafanua kuwa kwa mujibu wa uchunguzi halmashauri ya wilaya Kilosa zaidi ya vijiji 12 viongozi wake wanaendesha tawala kinyume na sheria.
“Niseme kuwa dunia ya leo tuepuke sana utawala wa kizamani wa kiongozi kasema, washirikisheni wananchi...migogoro mingi inayoibuka katika wilaya zetu ni ya wananchi kutoshirikishwa,” alitahadharisha Buhori.
Mafunzo hayo ya siku tano yamewalenga zaidi ya washiriki 30 kutoka kwenye vijiji mbalimbali vilivyo kata ya Rudewa, Ulaya, Zombo na Dinima wilayani humo.

No comments:

Post a Comment