NJOMBE

NJOMBE

Thursday, February 9, 2012

Mawaziri wapendekeza waziri wa Afya atolewe

KUFUATIA mgomo wa madaktari unaoendelea nchini, Baraza la Mawaziri limependekeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Katibu mkuu wake, Blandina Nyoni, kuwajibishwa ili kurejesha imani ya madaktari kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

Katika kikao cha kazi kilichofanyika juzi chini ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, inadaiwa mawaziri hao walimweleza kuwa kutokana na hali ya mgomo wa madaktari kuchafuka kupindukia, hakuna budi Waziri, naibu wake na katibu mkuu wakawajibishwa.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho, zilidai kuwa suala la mgomo lilipofikia haliwezi likashughulikiwa kimyakimya, lazima Serikali ikakubali kukaa na madaktari hao na kusikiliza malalamiko yao.

“Tumemweleza Waziri Mkuu (Pinda) kwamba madaktari wanasema hawana imani na watu hawa (waziri na katibu mkuu), hivyo hakuna njia ya kuwarejesha meza ya mazungumzo hadi viongozi hawa wawe wameondolewa,” kilieleza chanzo chetu cha uhakika.

Tayari, pendekezo hilo lilishatolewa na Kamati ya Wabunge wa CCM, ambao walitaka Dk Mponda, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya na Nyoni wajiuzulu au wakikataa wawajibishwe.

Pia, mawaziri hao walikubaliana kusaidia kushawishi wabunge kupitisha muswada wa mabadiliko ya katiba, ambao unapingwa na wabunge wa CCM, huku wengine wakitaka wabunge wasidhibitiwe kutoa dukuduku lao.

Suala la mgomo wa madaktari ambalo hivi sasa linashughulikiwa na Kamati ya Bunge ya Huduma ya Jamii, halijapata ufumbuzi zaidi ya kuzidi kupanuka kila siku na kuathiri huduma za afya.

Hata hivyo, wakati akikabidhi suala la mgomo huo wiki iliyopita kwa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, Naibu Spika, Job Ndugai, alionyesha wasiwasi na kauli ya Serikali iliyotolewa na Dk Mponda bungeni, ambayo haikujumuisha baadhi ya malalamiko ya madaktari.

“Lakini pia, katika submission ya Mheshimiwa Waziri ya Kauli, ya madai yale yaliyodaiwa na Madaktari, hata Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye tunamshukuru sana alipolishughulikia suala hili alipoenda kule kukutana nao na wao hawakujitokeza, lilikuwepo dai moja ambalo sijalisikia likizungumzwa hapa na ni vigumu kuzungumziwa!” alisema Ndugai na kuongeza:

“Nalo ni kwamba, hawa mabwana wanadai kwamba katika Wizara ya Afya kuna baadhi ya watendaji wakuu wenye uwezo mdogo wa utendaji na wa kiuongozi, wasiowajibika ipasavyo."

Na hawa watendaji wana kauli za kashfa na dharau kwa Madaktari. Kwa kutegemea timu ile iliyoundwa na Serikali itakayoripoti kulekule, itakuwa ni vigumu vilevile kupata ukweli wa upande huu wa pili.”

No comments:

Post a Comment