NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 11, 2012

Mbowe awashawishi wabunge upinzani marekebisho muswada wa katiba

KIONGOZI wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amewashawishi wabunge wa upinzani kupitisha marekebisho ya mabadiliko ya Katiba, huku akionya kuwa utamaduni unaojengwa bungeni sasa unabeba sura ya ‘funika kombe mwanaharamu apite’.

Hatua hiyo, ilitokana na mvutano kati ya wabunge wa CCM na wale wa upinzani, kuhusu upitishaji kifungu cha 17 cha sheria hiyo baada ya kufanyiwa marekebisho na kuweka wakuu wa wilaya na wakurugenzi kwamba wanaweza kutumiwa na Tume ya Katiba kuitisha mikutano ya maoni.

Marekebisho ya kifungu hicho juzi yalilazimika kurejeshwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, baada ya kutokea mvutano mkali kati ya wabunge wa CCM ambao walikuwa wakitaka kuwekwa mkuu wa wilaya, huku upinzani ukitaka mkurugenzi wa halmashauri kama ilivyopendekezwa na Serikali.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema, alipendekeza ili kuondoa kila upande kuonekana mshindi kwa suala hilo, kifungu hicho kiruhusu mkuu wa wilaya na mkurugenzi wanaweza kutumiwa na Tume ya Katiba, kuitisha mkutano wa maoni ingawa yalipingwa na wabunge wa CCM.

Mvutano huo ulimlazimisha Spika Makinda kurudisha kifungu hicho kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala ili kijadiliwe na kuona kinavyoweza kutekelezwa kwa njia nzuri.

Akisoma maafikiano ya Kamati na pande husika jana, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Angela Kairuki (CCM), alisema wamekubaliana na marekebisho yaliyopendekezwa na AG, ya kuwekwa kwa mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri.
Hata hivyo, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alisema marekebisho hayo ni mkanganyiko mtupu na kwamba, wakurugenzi wa halmashauri wanatosha kutumiwa na Tume ya Katiba, lakini kuingiza wakuu wa wilaya kunalenga kulinda maslahi ya CCM.

Mbowe alilazimika kuingilia kati na kuomba wapinzani kupitisha marekebisho hayo kwa ajili ya mustakabali wa nchi.
“Wakurugenzi wa halmashauri ni watendaji wa Serikali ya CCM, wanaosimamia shughuli za maendeleo ya wananchi… inasikitisha kuona kwamba Serikali haiwaamini watumishi wake,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Wabunge wa upinzani tunalazimika kuweka record (kumbukumbu) kukubaliana na marekebisho ya Mwanasheria Mkuu yapite…, lakini utamaduni huu tunaojenga humu ndani wa ‘kufunika kombe mwanaharamu apite utatu-cost (gharimu) baadaye.

“Wabunge wenzangu wa upinzani tukubali jambo hili limalizike kwa sababu lazima tufike sehemu tu-compromise (turidhie) twende tukatunge Katiba ambayo itadumu zaidi ya miaka 100 bila kujali kuwapo kwa CCM au Chadema.”
Baada ya Mbowe kumaliza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Steven Wassira, alisimama na kumpongeza kwa kutumia hekima na busara kushawishi wenzake.

Maoni ya Dk Slaa
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amewaasa Watanzania kutokubali kuburuzwa na watu watakaotoa elimu ya upotoshwaji wakati wa mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania kwa kuzingatia maslahi yao binafsi.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam jana Dk Slaa, alisema ikiwa itikadi zitaachwa zitawale mchakato huo ni hatari kwa kuwa zinaweza kuliingia taifa kwenye migogoro huku ikiwezesha kupatikana kwa Katiba isiyo na manufaa kwa wananchi.

“Suala kuandika Katiba Mpya ni kubwa, linahitaji umakini na ushirikishwaji. Ombi langu ni kwa wananchi, nawasihi kutokubali kuburuzwa na watu wachache watakaotoa elimu kuhusu Katiba yenye mlengo wa itikadi za vyama vyao vya siasa,” alisema Dk Slaa na kuongeza:

“Mtu yeyote awe wa CCM, Chadema au chama chochote ikigundulika anafanya kazi hiyo kwa itikadi ya chama chake cha siasa, apuuzwe kwani Katiba ni chombo muhimu cha kitaifa kinachopaswa kubeba maslahi ya Taifa la Tanzania kwa kipindi kirefu kijacho.”

Alisema ikiwa wananchi wataruhusu hali hiyo iliyojitokeza, mchakato wa kupata Katiba yenye maslahi ya kitaifa hautafanikiwa, badala yake taifa linaweza kuingia katika kipindi cha miaka hamsini mingine likiwa na Katiba isiyokidhi mahitaji ya Watanzania.

“Nimelazimika kusema hayo kwa sababu ninazo nyaraka za CCM zinazowahimiza wanachama wao kutumia kila njia kuhakikisha wanaingiza mahitaji yao mengi katika katiba mpya.  Nawasihi wananchi wayakatae na wahakikishe kuwa kila kinachoingia kwenye Katiba Mpya kinahusu maslahi ya taifa na si ya chama fulani; mwisho wa siku tusije kuwa na Katiba yenye mlengo wa chama cha siasa,” alisema Dk Slaa.

Alielezea dhamira ya chama chake kuwa ni kutetea maslahi ya taifa na kwamba hiyo ndiyo sababu iliyowafanya waanzishe na kusimamia agenda ya kutaka kuandikwa kwa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi.

Akizungumzia mjadala bungeni kuhusu Katiba Mpya, Dk Slaa alielezea kusikitishwa  kwake na namna wabunge walivyokuwa wakitetea itikadi za vyama vyao vya siasa badala ya maslahi ya umma huku akiwapiga kijembe wabunge wa CCM kuwa waliacha hoja na kujadili Chadema kumtambua Rais.

“Binafsi nilihuzunishwa na namna  wabunge walivyojadili mchakato wa Katiba Mpya, wengi waliweka pembeni maslahi ya taifa na kujadili  kwa kuzingatia misingi ya itikadi za vyama vyao vya siasa , hata hivyo  ninashukuru busara za mwenyekiti wetu zilisaidia kufikia maridhiano,” alisema.

No comments:

Post a Comment