NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 4, 2012

NSSF yawataka wafanyakazi kudai mishahara mizuri

MFUKO wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii Nchini (NSSF) umewahamasisha wafanyakazi kupitia vyama vyao kudai mishahara mizuri itakayowahakikishia mafao bora ya uzeeni.
Kauli hiyo ya NSSF inatokana na kiwango cha shilingi 80,000 kinacholipwa kwa mwezi kama kima cha chini kwa wastaafu na mfuko huo ambacho kimekuwa kikipigiwa kelele na wastaafu kuwa kidogo.
Akizunguza kwenye mkutano wa pili wa wadau unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC) mjini Arusha, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko huo, Crescentius Magori, alisema pamoja na ukweli kwamba kiwango hicho ni kidogo kulinganisha na gharama halisi ya maisha, ndicho kikubwa kulinganisha na mafao yanayotolewa na mifuko mingine nchini.
“Changamoto kubwa inayotukabili kama mfuko ni mishahara midogo wanayolipwa baadhi ya wanachama wetu ambayo ikikokotolewa wastaafu hujikuta wakiangukia kwenye kiwango cha kima cha sh 80,000 kwa mwezi,” alisema Magori.
Mkurugenzi huyo aliwashauri wafanyakazi kupitia vyama vyao kudai nyongeza ya mishahara na kuchanganya posho na marupurupu mengine katika mishahara ili kuongeza viwango vya mafao.
Maelezo ya mkurugenzi huyo yalitokana na hoja iliyotolewa na Mzee Calsin Lyaro (70) ambaye ni mkurugenzi mstaafu wa Radio Sauti ya Injili Moshi aliyeomba NSSF kuongeza kiwango cha kima cha chini cha mafao kutoka 80,000 ya sasa ili kuwawezesha wastaafu kumudu gharama za maisha zinazobadilika kila kukicha.
Mbali na hilo NSSF pia imepanga kupanua wigo wa uwekezaji kwenye miradi inayolenga kukuza na kuinua pato la mwananchi mmojammoja na taifa.
Miradi itakayohusika katika mpango huo ni ile ya sekta ya kilimo, ujenzi wa miundombinu pamoja na nyumba bora za bei nafuu kwa ajili ya makazi, ofisi na mahoteli.
Hayo yalibainishwa juzi na Mkurugenzi wa Mipango, Miradi na Uwekezaji wa mfuko huo, Yacoub Kidula, wakati akiwasilisha taarifa ya uwekezaji wa mfuko NSSF kwa wajumbe na wadau wanaohudhuria mkutano huo.
Alisema NSSF pia itaongeza uwekezaji katika uboreshaji wa miundombinu ya elimu kama ambavyo tayari imefanya kwa kushiriki ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
“Katika mkakati huo tayari ujenzi wa nyumba za kuishi eneo la Bugarika mkoani Mwanza na Mtoni Kijichi jijini Dar er Salaam umeanza na unatarajiwa kuendelea katika awamu zinazofuata,” alisema Kidula.

No comments:

Post a Comment