NJOMBE

NJOMBE

Thursday, February 2, 2012

NSSF yatamba kujiimarisha kiuchumi

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii Nchini (NSSF), umetamba kujiimarisha kiuchumi na kiuwekezaji kiasi cha kumudu kulipa mafao kwa wanachama wake wote kwa kipindi cha miaka sita ijayo bila kukusanya michango.
Mkurugenzi wa Uendeshaji wa NSSF, Crescentius Magori, alisema ndani ya kipindi hicho, mfuko huo utalipa mafao bila hata kukusanya mapato kutoka kwenye miradi, vitega uchumi na vyanzo vyake mbalimbali vya mapato.
Magori aliyekuwa akitoa taarifa kuhusu miradi na uwekezaji wa mfuko huo kwenye mkutano wa pili wa mwaka wa wadau wa mfuko huo, pia aliwataka waajiri nchini kuacha kuwabagua wanawake katika ajira kwa kuogopa likizo ya uzazi, kwani mfuko huo unatoa mafao ya uzazi ambayo ni mishahara ya miezi mitatu kwa mzazi baada ya kujifungua.
Alisema NSSF imeamua kutoa mafao ya uzazi ili kumpunguzia mwajiri gharama kwani sehemu ya fedha ambayo angelipwa mfanyakazi aliye katika likizo ya uzazi zitatumika kumlipa mfanyakazi wa muda anayeshikilia nafasi yake.
Kuhusu changamoto za ulipaji wa mafao kwa wanachama wanaotoka kwenye ajira kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kwa lazima wa miaka 60, Magori alisema tayari mfuko huo umewasilisha mapendekezo serikalini ili sheria hiyo ifanyiwe marekebisho kuruhusu mwanachama kulipwa kulingana na kipindi alichochangia badala ya kulazimika kusubiri hadi afikishe umri huo.
Naye Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Kangi Lugora (CCM), aliushauri mfuko huo kubadilisha mfumo wake wa uwekezaji katika ujenzi wa nyumba kwa kujenga na kuziuza kwa wananchi, badala yake watoe mafao au mikopo itakayowawezesha wanachama wao kujijengea nyumba zao wenyewe.

No comments:

Post a Comment