NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, February 21, 2012

Jaji Mkuu awataka majaji kutathimini utendaji haki

JAJI Mkuu, Othman Chande amewataka Majaji Wafawidhi kupanga mikakati mbalimbali ya kuboresha tija, kutathimini majukumu yao pamoja na utendaji haki ulivyo sasa na wanakoelekea.

Alisema hayo juzi Bagamoyo mkoani Pwani wakati akifungua warsha ya siku mbili kwa majaji wafawidhi ya kujadili mambo mbalimbali wanayokabiliana nayo katika utendaji kazi wao wa kila siku ikiwamo utendaji haki na uendeshaji mashauri.

Alisema katika ofisi nyingi tija imepungua na kuwataka nafasi hiyo waliyopata waitumie kupanga mikakati ya kuongeza nguvu kuboresha tija, kuweka malengo nani ana jukumu gani na nani atatoa taarifa za utekelezaji wa majukumu.

“Lengo ni kuboresha utoaji wa haki … ni mara yetu ya kwanza kukutana tangu uteuzi wangu na madhumuni ya kukutana ni kujua tunakokwenda na mchango wa kila mmoja,” alisema Jaji Mkuu.

Alisema katika warsha hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani wataweka vipaumbele vya Mahakama kwa sababu fedha inayopatikana katika bajeti ya muhimili huo wa Dola haitoshelezi.

Jaji Othmani alisema fungu pia lililopatikana kwa kesi za uchaguzi, limechelewa kuwafikia hivyo wataangalia namna ya kuziendesha ziishe kabla ya Mei mwaka huu muda ambao ndio wa kikomo wa kesi za uchaguzi kisheria.
Imeandikwa na Regina Kumba habari leo

No comments:

Post a Comment