NJOMBE

NJOMBE

Monday, February 6, 2012

Wasomi wapata changamoto juu ya katiba

WASOMI nchini, hususan vijana, wametakiwa kuwa wazalendo kwa nchi yao na kujitokeza kwa wingi kutoa maoni juu ya Katiba mpya badala ya kuwachia wanasiasa ambao watafanya hivyo kwa maslahi yao binafsi hivyo kulipeleka taifa pabaya.
Mkurugenzi wa elimu jimbo Katoliki la Moshi, Padri Wiliam Ruahichi, alisema hayo kwenye mahafali ya 21 ya kidato cha sita katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Kilimanjaro iliyoko wilayani Rombo.
Alisema vijana ndiyo nguzo kuu ya taifa hivyo wanatakiwa kujitokeza kwa wingi na kutoa maoni yao katika mchakato huo wa kupata Katiba mpya.
Pamoja na mambo mengine amewataka vijana hao kuepuka vitendo viovu ikiwemo kujiingiza katika uuzaji wa dawa za kulevya kwa lengo la kujipatia utajiri wa haraka.
“Ninyi ni wasomi wa taifa hili, nawasihi kuwa wazalendo na nchi yenu katika masuala mtambuka hususan suala la utoaji wa maoni juu ya Katiba mpya; hii ni Katiba yenu na siyo ya wanasiasa hivyo ni vyema kila kijana na msomi akajitokeza katika kutoa maoni yake, nawaombeni muepuke utumiaji na uuzaji wa dawa za kulevya kwa lengo la kupata utajiri wa haraka,” alisema mkurugenzi huyo.
Naye mkuu wa shule hiyo, Bradha Robert Mwigirah, aliwataka wahitimu hao kuishi kulingana na hali ya maisha ilivyo na kuwa wavumilivu katika maisha kwa kuzingatia nidhamu waliyofundishwa.

No comments:

Post a Comment