NJOMBE

NJOMBE

clock

Sunday, February 5, 2012

Zahanati yafungwa kwa kukosa muuguzi

ZAHANATI ya Kata ya Ngula, Wilaya ya Kwimba, Mwanza, imefungwa baada ya muuguzi kwenda likizo.
Mwandishi wetu alibaini kuwa zahanati hiyo ina muuguzi mmoja, aliyejulikana kwa jina moja la Magdalena, ambayo inahudumia vijiji vinne vya Nyamatale, Ngula, Ng'hulya pamoja na kijiji cha Ngogo.
Taarifa zaidi kutoka katika kata ya Ngula, zinaeleza kwamba, zahanati hiyo imefungwa tangu Januari 26 mwaka huu, na kwamba hadi sasa serikali kupitia Idara yake ya Afya wilayani humo, haijapeleka muuguzi mwingine.
Mkuu wa Wilaya ya Ngula, Christopher Kangoye, pamoja na diwani wa kata hiyo, Palu Mashagu (CUF), walisema kuwa hivi sasa wananchi wanaotegemea zahanati hiyo, wamelazimika kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta matibabu katika hospitali nyingine.
Diwani huyo aliishangaa serikali kwa kushindwa kutatua tatizo hilo, hali iliyosababisha kituo hicho kikafungwa.
 Kwa mujibu wa diwani huyo, hiyo si mara ya kwanza kwa zahanati hiyo kufungwa kwa kukosa muuguzi.
”Mwaka jana zahanati hii ilifungwa kwa tatizo hili hili la mtaalamu kwenda likizo, ilikuja kufunguliwa mwezi wa nne. Nasema kwa niaba ya wananchi wangu wa Kata ya Ngula hatutavumilia hali hii mbaya.
“Kwa nini serikali isilete wauguzi wengine wengi? Inakuwaje kituo kama hiki kinahudumia maelfu ya watu kiwe na mtaalamu mmoja tu? Tunataka serikali ilete haraka muuguzi ili watu wangu wapate huduma,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya hiyo, Kangoye alikiri kufungwa kwa zahanati hiyo kutokana na ukosefu wa wataalamu wa kutosha.
 

No comments:

Post a Comment