NJOMBE

NJOMBE

Thursday, February 16, 2012

Polisi: Hatutambui maridhiano ya kuwanusuru wanaharakati

                                               Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni
JESHI la Polisi Wilaya ya Kinondoni  limesema halitambui maridhiano ya  madaktari na Serikali ya kuwaachia  huru wanaharakati  walioandamana kushinikiza Serikali kutatua madai ya madaktari.

 Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Kinondoni, Charles Kenyera alisema wanaharakati hao watafikishwa mahakamani kama watuhumiwa wengine.

 Alisema Jeshi la Polisi ni Taasisi inayojitegemea na haiwezi kufanya kazi kwa shinikizo la madaktari.
Kenyera alisema  wanaharakati  16    waliokamatwa na  Jeshi   hilo watafikishwa  mahakamani muda wowote kuanzia sasa iwapo mwanasheria wa Serikali ataona kuna umuhimu wa kupelekwa mahakamani.

 “Ninachoweza kusema hapa, upelelezi umekamilika na tumeshapeleka kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP) ndiye mwenye uamuzi wa kuwafikisha mahakamani,” alisema.  Jana jeshi hilo lilishindwa ama kuwaachia au kuwafikisha mahakamani wanaharakati 16 waolitiwa mbaroni Alhamisi iliyopita katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wakidaiwa kutaka kuandamana kuishinikiza Serikali kumaliza haraka mgogoro wake na madaktari.

Pia wanaharakati hao wanadaiwa kukutwa na mabango 30 yenye ujumbe tofauti wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda akizungumza na madaktari ambao walikuwa katika mgomo na kudaiwa kufunga baadhi ya barabara za jjiji la Dar es Salaam siku moja kabla ya kukamatwa kwao.

 Wanaharakati hao waliachiwa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam jana (Jumanne) lakini walipofika kituoni hapo walielekezwa kuonana na Ofisa Upelelezi Makosa ya Jinai Wilaya ya Ilala (RCO), Kituo Kikuu cha Polisi Kati kwa ajili ya maelekezo zaidi.

"Wametutaka turipoti kwa RCO Ilala, wanasema kwa kuwa tulikamatwa Muhimbili suala letu linatakiwa kwenda Ilala na hapa Oysterbay limeletwa kimakosa," alisema Mkurugenzi Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo-Bisimba.

Akizungumza na wanaharakati hao ofisini kwake, Ofisa Upelelezi Ilala, Duwali Dila aliwaambia kuwa suala lao lipo katika ngazi nyingine linashughulikiwa na warudi tena kituoni hapo Jumatatu wiki ijayo ambapo atakuwa katika nafasi nzuri ya kuweza kujua kinachoendelea.

 "Nafikiri tuonane Jumatatu, labda tukubaliane muda kwani suala hili kulingana na taratibu zetu siku hizi za jeshi la polisi lazima lipitie ofisi ya DPP kabla ya kufika kwetu," alisema na kuongeza kuwa sio wao polisi ambao wanatakiwa kuandaa mashtaka.

 Alisema ofisi hiyo ndio ambayo inapaswa kuandaa shtaka kama lipo baada ya kupitia vielelezo vyote na kujiridhisha kuwa kuna tuhuma ambazo zinapaswa kupelekwa mahakamani au vingine kisha kuwasilisha polisi.

Dila aliwahakikishia kuwa Jumatatu ndio itakuwa siku ya mwisho kwani mchakato utakuwa umekamilika, hoja ambayo ilikubaliwa na wanaharakati hao ambao waliondoka ofisini hapo na kuendelea na shughuli zao zingine.

Wanaharakati hao walikamatwa wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokuwa na mkutano na madaktari waliokuwa katika mgomo na walipopekuliwa katika magari yao, ambapo walikutwa na mabango 30 yenye jumbe mbalimbali ambayo yalikuwa yanaishinikiza serikali kumaliza mgogoro wake na madaktari.

Pia siku moja kabla wanaharakati hao walifanya maandamano ya kutaka kwenda Ikulu ambayo yalisababisha kufungwa kwa barabara ya Ocean na Ali Hassan Mwinyi eneo la Palm Beach, jijini Dar es Salaam kabla hawajaamriwa kutawanyika na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasi (FFU).

No comments:

Post a Comment