NJOMBE

NJOMBE

Thursday, February 2, 2012

Mbunge adai kuvuliwa nguo gerezani

MBUNGE wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF), amesema alipekuliwa sehemu zake za siri na kuachwa uchi wa mnyama wakati akiingizwa magereza kama wanavyo nyanyaswa wanawake wengi waofikishwa kwenye mikono ya dola.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana baada ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Khamis Kagasheki, kumtaka Mbunge wa Viti Maalumu, Mhonga Said (CHADEMA), aliyeuliza swali la msingi juu ya manyanyaso wanayopata wanawake wanapoingia katika Gereza la Bangwe, Kigoma, kuleta ushahidi wa madai kwamba wanavuliwa nguo na kuachwa uchi.
Akizungumza kwa uchungu na hisia kali, Sakaya alisema yeye ni shahidi wa madai hayo kwani aliwahi kutendewa hivyo wakati aliposwekwa mahabusu kwa tuhuma za kufanya mkutano bila kibali, akiwa na viongozi wenzake wa CUF mkoani Tanga.
“Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wanawake wananyanyaswa, wanavuliwa nguo zote na kubaki kama walivyozaliwa kwa kisingizio cha kupekuliwa kabla ya kuingia mahabusu, wanaofanya hivyo ni wanawake wenzao na mimi ni mmoja wa waathirika wa hali hiyo. Tunaiomba serikali itoe tamko kali na kuwachukulia hatua watakaobainika kuendeleza unyanyasaji huo,” alisema mbunge huyo.
Katika swali lake la msingi, Mhonga alisema kumekuwa na matendo ya kikatili na uvunjwaji mkubwa wa haki za binadamu katika magereza, likiwamo Gereza la Bangwe, Kigoma.
Alisema wanawake wanaoingia gerezani hapo, hupekuliwa kwa kuvuliwa nguo zote na kuamriwa kurukaruka kichura wakiwa uchi kama walivyozaliwa.
Kutokana na madai hayo, Mhonga alitaka kujua serikali itawachukulia adhabu gani askari hao wa magereza wanaowadhalilisha wafungwa wanawake.
Akijibu swali hilo la msingi, Waziri Kagasheki alisema kuwa serikali kwa mara ya kwanza ndiyo inasikia taarifa za kushtua kama hizi kuhusu Gereza la Bangwe.
“Tumefuatilia bila kupata ushahidi wa jambo hili. Namuomba mbunge kama anao ushahidi wa jambo hili anipatie mara moja kwani bila kuwabaini askari wanaofanya vitendo hivi ni vigumu kuwaadhibu,” alisema.
Alisema kuwa kimsingi wahalifu wanapoingia na wawapo magerezani zipo kanuni na taratibu zinazolinda na kuthamini haki na utu wao chini ya kanuni za kudumu za uendeshaji wa Jeshi la Magereza za mwaka 1968.
“Kanuni hizi hazimruhusu askari kutothamini au kumdhalilisha mfungwa na kumtesa mfungwa. Endapo askari yeyote anakiuka kanuni na sheria hizo, hatua kali za kinidhamu huchukuliwa mara moja dhidi ya askari mhusika,” alisema.

No comments:

Post a Comment