NJOMBE

NJOMBE

clock

Sunday, February 5, 2012

CHADEMA kuwasha moto,mgomo wa madaktari

WAKATI serikali ikiwa bado inajikanganya na kushindwa kuwaambia ukweli wananchi juu ya sakata la nyongeza ya posho za wabunge, zinazopingwa vikali, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeamua kuwasha moto kwa kueleza umma mfumo mbovu uliopo serikalini.
CHADEMA kimesema kitatumia kampeni za uwakilishi Jimbo la Uzini kukoleza moto wa kupinga ongezeko la posho za wabunge na mfumo mzima wa kulipana posho za vikao serikalini.
Chama hicho kimesema kuwa suala la nyongeza ya posho ya vikao kwa wabunge na mfumo mzima wa kulipana posho ya vikao serikalini ni kitu ambacho hakitakubalika kwa mwananchi yeyote mwenye uchungu na nchi yake.
Wakizungumza katika mikutano ya kampeni zinazoendelea kumnadi mgombea uwakilishi, Maalim Ali Mbarouk Mshimba, katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Uzini, viongozi waandamizi wa chama hicho wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Mussa Yusuf, walisema kuwa chama hicho kitaendelea kupinga hatua zozote za kikundi kidogo cha watu kujineemesha kupitia migongo ya wananchi, inayozidi kupinda kwa umaskini.
Walisema makundi mengine katika kada mbalimbali za utumishi kwa umma kwa muda mrefu yamekuwa yakilalamika juu ya ufinyu wa mishahara isiyokidhi hata mahitaji ya mwezi mmoja lakini serikali imeamua kuwaongeza fedha wabunge.
Akimnadi mgombea mbele ya wananchi katika mikutano ya jana, Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Benson Kigaila, aliwaambia wananchi wa maeneo mbalimbali ya Uzini kuwa kitendo cha kuwaongezea wabunge posho ya kikao kufikia sh 330,000 kwa siku hakikubaliki.
Alisema makundi mengine ya watumishi katika jamii yanakabiliwa na hali ngumu ya mishahara yao na hayana posho kama wanavyolipana wabunge, ambao sasa wanaonekana kutumia rasilimali za taifa kwa masilahi ya wachache.
“Ndugu zangu wa Uzini, tunaposema Serikali ya CCM imewasaliti wananchi wake, tunaposema kuwa imesaliti hata malengo na shabaha za mapinduzi ya mwaka 1964, tunakuwa tunamaanisha mambo kama haya.
“Walimu wanafanya kazi katika mazingira magumu sana, mishahara yao kwa mwezi ni kidogo mno, wengine hawafikii hata hiyo posho ya zamani ya mbunge ya siku moja, achilia mbali hii iliyoongezwa.
“Madaktari na wauguzi, wanadai walau shilingi elfu kumi ya posho wanapoitwa kazini, wanaitaka serikali iboreshe sekta ya afya ili wananchi mkienda hospitali tupate huduma zinazostahili katika nchi hii tajiri,” alisema.
“Viongozi hao wa CHADEMA walisema kuwa madaktari wanaitaka serikali isiendelee kuingia gharama za kuwapeleka wakubwa kutibiwa nje ya nchi, wanaitaka iboreshe mazingira ya utendaji kazi wao, lakini serikali inasema haina hela, lakini inazo za kuwaongeza wabunge.
“Wananchi angalieni, angalieni kwa makini, mwaka juzi wafanyakazi nchini waliitisha mgomo mkubwa sana, mojawapo ya madai yao ilikuwa ni kuongezwa kima cha chini kiwe shilingi 315,000, lakini Rais Kikwete akawaambia serikali yake haina hela.
“Rais akaleta mahesabu ya uongo na kweli, kama alivyofanya juzi Waziri Mkuu wake, Pinda, lakini sasa wanadiriki kufanya kufuru ya kujiongezea posho wanasiasa kwa kukaa bungeni, wazungumze, wasizungumze, wanapata posho laki tatu na ushei,” alisema Kigaila.
Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Mussa Yusuf, alisisitiza kuwa kamwe CHADEMA hakitarudi nyuma katika mjadala huo wa kupinga posho za vikao, kiliouanzisha kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, wakati akiwa mbunge, katika vita dhidi ya ufisadi.
Aliongeza kuwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 kwenye ilani yake, kisha kikauingiza bungeni katika Bunge la bajeti mwaka jana, kupitia hotuba ya Kambi ya Upinzani iliyosomwa na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Kabwe Zitto kilipinga matumizi yasiyofaa.
Alisema baada ya Zitto kusoma hotuba hiyo iliyopinga posho, huku mawaziri wengine vivuli wakiendelea kulisisitiza katika hotuba zao, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, aliweka msimamo akiitaka serikali ifanye mabadiliko ya sera na sheria ili kuondoa posho kwa wabunge na watumishi wa umma na ununuzi wa magari ya kifahari.
Aliongeza kuwa chama hicho kilitaka fedha hizo zitumike kuwanufaisha Watanzania kupitia miradi ya maendeleo, itakayoinua uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja.
Mussa alisisitiza kuwa CHADEMA hakipingi nyongeza ya posho za wabunge pekee, bali mfumo mzima wa kulipana posho za vikao, ambao umesababisha kuzorota kwa utendaji kazi na kuongeza matumizi makubwa ya serikali, ambapo takriban sh bilioni moja zinatumika kulipana posho ya vikao kwa watumishi waandamizi wa serikali, mashirika ya umma na wanasiasa.
Alisema kuwa serikali inapoteza uhalali wa kuyazuia makundi mengine ya jamii, kudai nyongeza ya posho na mishahara.
Aliongeza kuwa utendaji mbovu wa serikali umekuwa ukichochea migogoro, migomo na maandamano, lakini serikali imekuwa ikiishia kushughulikia matokeo badala ya kutatua vyanzo vya migogoro hiyo.

No comments:

Post a Comment