NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, February 7, 2012

Ubinafsi wa wanasiasa unawaumiza Watanzania, taifa letu


TAIFA letu hili lina uwezo wa kuwa taifa kubwa katika Bara la Afrika, uwezo ambao unabakia kuwa ndoto kuufikia kutokana na matatizo ya ubinafsi.Tabia ya ubinafsi ambayo imo ndani ya mtu mmojammoja imekuwa ni tatizo kubwa linalokwamisha maendeleo katika ngazi zote kama familia, jamii na taifa.

Ubinafsi hapa nchini umekuwa ni ugonjwa mbaya ndani ya baadhi ya watu na una athari katika nyanja muhimu katika jamii, hivyo unahitaji kupigwa vita na kila mpenda maendeleo ya nchi yetu, kwani tusipoupiga vita basi tutaendelea kuwa maskini huku wachache wakineemeka.Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere hata kabla ya Uhuru alikuwa ameshajua kuwa Taifa lina maadui wabaya watatu, umaskini, ujinga na maradhi, lakini nadhani alisahau aduni mmoja ambaye ni ubinafsi.

Mwalimu Nyerere aliamini Taifa haliwezi kuendelea bila kuwapiga vita maadui hao hata kama nchi itapewa uhuru wake, hivyo baada ya uhuru  alitangaza vita ya mapambano kuwatokomeza maadui hawa.

Nasema kwa uhakika kabisa kwamba katika nchi zote zilizowahi kupitia katika machafuko kama vile Rwanda, Burundi na Somalia "Ubinafsi" wa watawala aidha waliotangulia ama waliokuwapo ulichangia sana kuziingiza nchi zao katika vita.
Ni ubinafsi ndio uliopelekea ukiukaji wa haki za msingi za binadamu na ndio siku zote umesababisha vita. Ndiyo maana nasema kwa uhakika kwamba, tukitaka amani ya kweli tuupige vita ubinafsi wa makundi.

Ni ubinafsi ndio unaowafanya watu wengine kukwepa kodi kwa njia ya kupewa misamaha na baadhi ya wafanyakazi wa TRA wasio na waadilifu katika nchi hii kisha watu hao baada ya kunufaika na hizo njia haramu ndipo hugeuka na kuwabeza masikini wakidai ni wavivu na hawajishughulishi wakati wao ndiyo waliowadhulumu haki zao.

Vyuo vikuu na Wizara zetu zimejaa tafiti zilizoandikwa kitaalamu na kibunifu mno, lakini bahati mbaya ubinafsi umefanya nyaraka hizo zisiweze kubadilishwa kuwa miradi inayoishi, pengine ingeondoa tatizo kubwa la ajira.
Tunahitaji kuondoa utamaduni kutunza nyaraka kwenye mashubaka au kuwaachia watu wengine watufanyie mambo yetu au ugonjwa unaofahamika maarufu kama ‘tunaiomba serikali’.

Nchi yetu hii hivi sasa imefika njia panda ambayo hatima yake kisiasa si kueleweka bali kutabirika. Chama CCM kinatawala, lakini Chama cha Chadema kinadai kina nguvu ya umma, CUF wao nao wanawaona CCM wanawacheleweshea utawala Zanzibar.
Si watawala wala wapinzani wote wanacheza muziki ule ule, wote wabinafsi kwani wakati watawala wanaposimama kwa hoja zao wakidai wanawatetea wananchi wenzao wa vyama vya upinzani wanafanya kila mbinu za kuwachonganisha na wananchi wao wanazungumza ya kwao wanajaribu kuchora picha nyingine ya kile kinachosemwa na Serikali.

Kiufupi taifa limekuwa taifa la maneno tupu, badala ya kupingana kwa hoja ili kuboresha zaidi inakuwa tofauti ni kubishana kwa kwenda mbele na kurudisha nyuma maendeleo.

Kila anayeweza kusema zaidi na kuunganisha hoja zake ndiye ambaye anayedhani amemudu kutawala hisia za Watanzania, anadhani kuwa Watanzania watakula maneno au kelele anazojitahidi kuzitoa.

Katika ngazi mbalimbali za jamii ubinafsi umechochea chuki na manung’uniko mathalani ubinfsi wa viongozi wa mkoa wa Mbeya umesababisha maafa makubwa kwa wananchi wa mkoa huo, kwa viongozi wa mkoa huo kutokuwa wakweli.

Kilichotokea waliwaahidi wafanyabishara ndogo ndogo wa mji huo wa eneo la Mwanjelwa kwamba wangewapatia sehemu nyingine kwa ajili ya kujipatia mkate wo lakini cha kushangaza wakawatimua wakiwataka wapotee katika maeneo ya mjini jambo ambalo lilizua balaa.

Ni ubinafsi huu huu ndiyo unaoifanya Serikali ikimbize muswada wa marekebisho ya kusomwa kwa mara ya pili na ya tatu kisha kuupitisha, huku ubinafsi huo huo ukiwatuma watu wa upinzani wa Chadema, wanaharakati kudai kuwa wataanzisha mchakato mpya kivyao.

Hali hii inaliweka taifa njia panda ni nani mkweli kati ya pande hizo mbili, ni nani anawatakia mema Watanzania. Nionavyo hakuna anayemtakia mema Mtanzania. Kilichotakiwa ni kuketi chini kukubaliana kupata mustakabali ili tusonge mbele.

Siamini kabisa kwamba eti pande hizo ndiyo Watanzania zaidi, Watanzania ni wengi na wanahitaji amani zaidi kuliko mkorogano, wanahitaji uhuru zaidi kuliko kulazimishana, kwa maana hiyo ubinafsi hauna budi kukoma ili kusaidia maisha ya Watanzania.

No comments:

Post a Comment