NJOMBE

NJOMBE

clock

Tuesday, February 21, 2012

Wasomewa mashitaka wakiwa wamejeruhiwa kwa risasi

WAKAZI watano wa jijini Dar es Salaam akiwamo mganga wa jadi wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu huku baadhi yao wakiwa wamejeruhiwa kwa kupigwa risasi, wakishitakiwa kwa kukutwa na bunduki na risasi bila kibali.

Kati ya watuhumiwa hao watano, wanne walikuwa wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili huku nguo zao zikiwa na damu.

Baadhi yao walionekana wamefungwa plasta za jasi na miguuni kuwekewa vyuma vya kurekebisha mifupa na kushindwa kutembea.

Watuhumiwa hao walisomewa mashitaka nje ya mahabusu ya Mahakama. Washitakiwa hao ni Yusuf Matimango (35), Athuman Kibambe (44), Ally Ngingame (42), Said Mangala (40) na mganga wa jadi Asha Ungando (45).

Wakili wa Serikali, Frida Mwela alimuomba Hakimu Bingi Mashabala kuwafuata washitakiwa mahabusu kuwasomea mashitaka kwa sababu hawezi kutembea kutokana na majeraha waliyonayo pamoja na maumivu makali.

Hakimu huyo alikubaliana na ombi hilo na kwenda mahabusu ambapo alisimama nje ya jengo la mahabusu na washitakiwa hao walitolewa nje na kuanza kusomewa mashitaka yao ambayo walikana yote.

Katika mashitaka yao walidaiwa Februari 10 mwaka huu katika mtaa wa Tandika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam walikutwa na Bunduki aina ya Shot Gun na kukutwa na risasi katika tarehe hiyo hiyo na eneo hilo hilo.

Baada ya kukana mashitaka, walidai kuwa walikamatwa na kupigwa na askari wa kituo cha Polisi Sitakishari na wengine kupigwa risasi miguuni bila kufahamu makosa yao.

“Mheshimiwa hakimu sisi tumekamatwa bila kidhibiti chochote na tulipofika Polisi tulipigwa sana tukalazimishwa kusaini maelezo ambayo hatuyajui na waliokaa wakapigwa risasi na mmoja wetu ameuawa,” alidai Matimango.
                                               Mganga Asha Ungado akiwa chini ya Ulinzi
 Mshitakiwa mwingine alidai kuwa waliwekwa kituoni wiki nzima ndipo walipelekwa Hospitali. Hata hivyo walifungwa majeraha tu bila kupewa dawa yoyote huku mwingine akilalamika kuwa alisikia polisi wakiwaeleza madaktari akatwe mguu tu.

Hakimu Mwashabala alitoa masharti ya dhamana yaliyowataka kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika pamoja na kusaini hati ya dhamana ya Sh milioni mmoja kila mmoja.
Imeandaliwa na Habari leo

No comments:

Post a Comment