NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 4, 2012

Dk. Magufuli vitani na makandarasi feki

WAZIRI wa Ujenzi Dk. John Magufuli jana alitangaza kiama kwa makandarasi wote nchini ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa uzembe na chini ya kiwango kuwa hatakuwa na msalia mtume nao.
Dk. Magufuli aliyasema hayo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Tabora Mjini Ismail Rage (CCM) na kusema hana kigugumizi wala huruma kwa watu wa aina hiyo.
“Mpaka sasa nimeshafukuza makandarasi 2059 hivyo nasema na wengine wazembe na wanaofikiria kucheza na kazi basi wakae mkao wa kula lazima nitawatimua,’’ alisema Dk. Magufuli.
Katika swali lake Rage alitaka kujua ni kwa nini ujenzi wa barabara za Tabora na Nzega-Tabora,Tabora-Manyoni na Tabora-Urambo unakwenda kwa kusuasua zaidi.
Rage pia aliitaka serikali kutoa tamko la lini barabara za lami zitakamilika katika mkoa wa Tabora ambao kwa muda mrefu umekosa barabara nzuri.
Waziri huyo alisema kusuasua kwa ujenzi a barabara za Tabora kulichangiwa na mambo mengi yakiwemo kuchelewa kwa makandarasi kufanya upembuzi na kuchelewa kupatikana kwa fedha kwa wakati.
Alisema tatizo hilo hivi sasa limepungua kwani serikali imepata fedha za kuanzia malipo ya makandarasi hao ambapo sh bilioni 45 zimelipwa.
Kutokana na hilo hivi sasa makandarasi hawana kisingizio cha kuanza kwa kasi ujenzi wa barabara hizo ambazo hadi ujenzi wake utakapokamilika zitagharimu jumla ya sh bilioni 453.

No comments:

Post a Comment