NJOMBE

NJOMBE

Friday, February 3, 2012

Mkulo, Werema wapata pigo

SERIKALI jana imepata pigo bungeni baada ya miswaada yake miwili ya mabadiliko ya shria kukatiliwa.
Mswaada wa kwanza kupigwa chini ulihusu marekebisho ya marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa unaotozwa kwenye maji yanayohifadhiwa kwenye chupa kwa madai kuwa marekebisho hayo yatawanufaisha wenye viwanda badala ya watumiaji wa kawaida.
Mswaada wa pili ambao uliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema ilihusu mrekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo sheria ya Bodi ya mikopo iliyozua kasheshe Bungeni na kusababisha ukataliwe.
Mbunge aliyesababisha mswaada wa madailiko ya sheria kukataliwa ni Mbunge wa Kigamboni Faustine Ndungulile (CCM) aliomba mwongozo wa Spika kutaka muswaada huo wote ukataliwe na kurejeshwa serikalini kwa madai kuwa ulikuwa na ubaguzi.
Hoja hiyo iliungwa na wabunge wengi na kutokana na hali hiyo, Naibu Spika Job Ndugai alilazimika kuwaambia wabunge wapige kura mara tatu ili kupata uamuzi wa mwisho.
Kabla ya hatua hiyo baadhi ya wabunge akiwemo Warema walitaka mswaada kuhusu bodi ya mikopo uondolewe na mingine 16 iendelee kujadiliwa.
Hoja ya Waziri Mkulo ilipendekeza kufanyia marekebisho sheria hiyo iliyoko kwenye jedwali la nne la sheria ya ushuru wa bidhaa sura 147 kwa kupunguza ushuru kutoka sh 69 kwa lita moja ya maji yanayohifadhiwa kwenye chupa hadi kufikia sh 12.
Bunge kwa sauti moja, lilifikia azimio hilo baada ya wabunge wengi waliochangia hoja hiyo kueleza kwamba marekebisho hayo kamwe hayalengi kumnufaisha Mtanzania wa chini na badala yake itawanufaisha wenye viwanda vya maji.
Hoja ya kukataa iliyoungwa mkono na wabunge wengi, iliibuliwa na Mbunge wa Buchosa, Charles Chizeba (CCM), ambaye alisema Waziri Mkulo katika kuleta marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa ya maji zinazohifadhiwa kwenye chupa, amelenga kuwanufaisha wenye viwanda.
Mbunge huyo aliomba mwongozo wa Spika na kutumia kanuni 58 kutaka hoja hiyo iahirishwe hadi wakati wa bajeti ijayo ambapo serikali itakuwa imejipanga kwani kwa sasa haoni sababu ya Bunge kuridhia hoja hiyo.
Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika Job Ndugai, alisema mbunge huyo alipaswa kutumia kanuni ya 60, badala ya kanuni 58.
Hata hivyo kwa mamlaka yake, aliendelea kuwahoji wabunge wanaoafiki hoja hiyo iondolewe waunge mkono kwa kusema ‘ndiyo’ ambapo kundi kubwa la wabunge bila kujali itikadi zao, walisimama kuunga mkono na wabunge wachache hasa mawaziri ndiyo walioketi kwenye viti vyao na kusema hapana kupinga hoja hiyo kuondolewa bungeni.
“Kwa hali hiyo waliosema ndiyo hoja hiyo iondolewe wameshinda, hivyo naamuru waziri mwenye dhamana aondoe hoja yake na kwenda kujipanga upya,” alisema Ndugai huku wabunge walioshinda wakipiga makofi kushangilia ushindi wao.
Baada ya hoja yake kutupwa, Waziri Mkulo akiwa nje ya ukumbi wa Bunge, alikuwa mbogo kuzungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua maoni yake hasa baada ya hoja yake kutupwa.
“Sitaki kuzungumza na waandishi, nina kikao muhimu natakiwa kuhudhuria, kila kitu kimeelezwa ndani ya Bunge,” alisema Mkulo.
Awali akiwasilisha hoja hiyo, Waziri Mkulo alisema Bunge lilipitisha marekebisho ya sheria ya ushuru wa bidhaa sura 147 ambapo pamoja na mambo mengine marekebisho hayo yaliweka ushuru wa bidhaa sh 69 kwa lita ya maji yanayohifadhiwa katika chupa. Kabla ya hapo bidhaa hiyo ilikuwa haitolewi ushuru.
Alisema tathmini iliyofanyika baada ya ongezeko hili la ushuru wa bidhaa, serikali imebaini kwamba bei ya maji yanayohifadhiwa kwenye chupa imepanda kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwafanya watumiaji wengi ambao ni wananchi wa kawaida, kushindwa kumudu bei husika.
“Ongezeko hili la ushuru wa bidhaa limesababisha bei za maji yanayozalishwa na viwanda vya hapa nchini kuwiana na bei za maji yanayoingizwa kutoka nje ya nchi na hivyo kuondoa ushindani uliokuwepo hapo awali. Hali hii itapunguza uzalishaji wa viwanda vya hapa nchini na hivyo kupunguza mapato ya ndani na ajira kwa wananchi,” alisema Mkulo.
Mkulo aliitaja sababu nyingine ya kuomba hoja yake iungwe mkono kuwa tathmini iliyofanywa, imebaini kuwa nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki za Kenya, Rwanda na Uganda zinatoza ushuru wa asilimia 10.
Mkulo aliendelea kutetea hoja yake kwamba tathmini iliyofanywa imebaini kuwa baada ya kurekebisha ushuru wa maji ya chupa kutoka sh 69 hadi sh 12, ushuru wa bidhaa uliotegemewa kukusanywa kwa kipindi cha Julai hadi Juni 2012, ungeingiza sh milioni 2.7 badala ya sh milioni 15.5, hivyo kusababisha  upungufu wa sh milioni 12,845.
Alisema punguzo hilo la mapato, linatarajiwa kuzibwa kwa kupunguza posho mbalimbali, kupunguza fedha za kongamano, ununuzi wa magari, ununuzi wa samani, gharama za uendeshaji wa ofisi, mafunzo ya ndani na nje, safari za ndani na nje na ukarabati za majengo.
Akisoma maoni ya kambi ya upinzani kuhusu hoja hiyo, Kaimu Msemaji Kivuli wa kambi ya upinzani, Christina Mughwai, alisema kambi hiyo katika maoni yake ilipendekeza kuwa ushuru huo wa maji ya kunywa ya chupa, uachwe kama ulivyo, lakini serikali iliamua kuongeza kutoka sh 12 hadi 69 kwa lita moja.

No comments:

Post a Comment