NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 4, 2012

Serikali yajipalia makaa,Madaktari wasema serikali haina nia ya kumaliza mgomo


MVUTANO baina ya serikali na madaktari umechukua sura mpya baada ya wataalamu hao kusema Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, amelidanganya Bunge.
Wakati madaktari wakitoa kauli hiyo, Dk. Mponda amesema madai mapya ya watalaamu hao hayalipi na amemtuhumu Mwenyekiti ya Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimbukoa Stephen, kuwa ndiye kinara wa mgomo huo.
Waziri Mponda jana aliwasilisha taarifa ya serikali kuhusu namna ilivyoshughulikia mgomo huo wa madaktari na kudai imechukua hatua nyingi kuutatua.
Dk. Mponda alitumia muda mwingi kueleza chanzo cha mgogoro huo na hatua zilizochukuliwa kuumaliza; alisema pamoja na madai mengine, madaktari hao walipendekeza kuwa daktari anayeanza kazi alipwe sh milioni 3.5 kwa mwezi pamoja na asilimia 120 kama malipo ya posho mbalimbali za mazoezi.
Akieleza athari za pendekezo hilo, Waziri Mponda alisema hali hiyo itailazimu serikali kurekebisha viwango vya mishahara kwa watumishi wote wa kada za afya pamoja na kada nyingine ili kuweka uwiano kufuatana na stahiki za miundo katika utumishi wa umma.
“Kwa mujibu wa mapendekezo yao, kiwango cha kuanzia mishahara kwa mhudumu wa afya, kitakuwa sh 670,316 na mshahara wa juu kwa kada hiyo, utakuwa sh 8,145,573. Utekelezaji wa pendekezo hilo utagharimu sh 83,508,834,430 kwa mwezi ambayo ni sawa sh 417,544,172,150 kwa kipindi kilichobaki cha miezi mitano ya mwaka huu wa fedha,” alisema.
Alisisitiza kuwa madai yao hayalipiki kwani mshahara wa daktari anayeanza kazi, atapata sh 7,700.000, ikijumuisha mishahara na posho wakati daktari mwandamizi mshauri, anapaswa kuweka kipindoni sh milioni 17,231,020 na kuongeza kuwa madaktari hao wanapendekeza kuwa watumishi wa kada zingine za afya, wapandishiwe mishahara na posho kama zao.
“Endapo nao watapewa pesa wanazodai, serikali itapaswa kulipa sh 202,413,397,568.00 katika makundi hayo mawili tu. Nyongeza yao ya mshahara ni sawa n ash 1,002,110,603,160.00 kwa mwaka.
“Ukijumlisha na nyongeza ya posho yao wanayodai ya sh 1,037,184,854,550, unapata sh trioni 2.03 ambayo ni karibu theluthi mbili ya mishahara ya wafanyakazi wote nchini ambayo kwa sasa ni sh trioni 3.45, hii haiwezekani,” alisema Mponda.
Alitetea kiwango cha sasa cha mshahara wa daktari anayeanza kazi kuwa ni sh 900,000 mbacho alisema ni kikubwa ukilinganisha na watumishi wa kada zingine nchini.
Akizungumzia ukaidi wa madaktari hao, Waziri Mponda alisema serikali imejitahidi mara nyingi kuwaita viongozi wa madaktari hao na kujadiliana nao, lakini mara zote walikataa na hakuna sababu ya msingi.
Waziri Mponda alisema serikali imeunda kamati kushughulikia maazimio yaliyowasilishwa kwa Waziri Mkuu Pinda ili kamati hiyo iyachambue na kutoa maoni yakayosaidia kumaliza mgogoro huo.
Pamoja na hatua hizo, waziri huyo aliwahakikishia wabunge na Watanzania kuwa serikali imedhamiria kwa dhati kulimaliza tatizo hili na kuwataka wadau mbalimbali wa afya kujitokeza na kutoa maoni mbele ya kamati hiyo.
Akizungumzia hali ya mgomo baada ya kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwataka madaktari hao warejee kazini vinginevyo watakuwa wamejifukuzisha kazi, alisema huduma katika hospitali ya Muhimbili na katika vitengo vyote, zimerejea katika hali ya kawaida huku kukiwa na madaktari 15 kutoka JWTZ.
Alisema hospitali za rufaa za kanda: Bugando, KCMC, Mbeya, Hospitali za Dar es Salaam, Dodoma, Iringa na Tanga, zimerejea katika hali ya kawaida wakati mikoa iliyobaki haikuwa na mgomo.
Waziri Mponda, aliwataka madakatari wanaoendelea na mgomo kusitisha mgomo kwa kuwa serikali imedhamiria kwa dhati kumaliza madai yao.
Hata hivyo mara baada ya kumaliza kutoa kauli hiyo ya serikali, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, Zitto Kabwe Kigoma Kaskazini, wote CHADEMA, waliomba mwongozo kutaka kauli hiyo ijadiliwe, lakini Naibu Spika Job Ndugai alisema kanuni haziruhusu.
Ndugai alisema Bunge litajadili kauli hiyo baada ya kupitia kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii na kuwataka wabunge wenye maoni kwenda kutoa maoni yao kabla ya hoja hiyo kuletwa bungeni.
Kamati ya madaktari yajibu
Kamati ya madaktari, imetoa tamko la kupinga taarifa ya serikali kuhusu mgomo wa wanataaluma hao iliyosomwa bungeni jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda.
Taarifa iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari hao, Dk. Stephen Ulimboka, ilisema kuwa wanalishukuru Bunge kupitia kwa Naibu Spika, Job Ndugai, kwa kuiagiza Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii kuanza kazi mara moja ya kukutana na madaktari.
Alisema waliazimia kuwa kamati pamoja na jumuiya ya madaktari wako tayari kukutana na kamati ya huduma za jamii na kutokana na umuhimu na dharura kubwa, mkutano wa jumuia ya madaktari unatarajiwa kufanyika leo kuanzia saa nne asubuhi.
Dk. Ulimboka alisema kuwa kamati imesikitishwa na kauli ya Waziri Mponda aliyoitoa bungeni ambayo imejaa upotoshaji mkubwa kwa jamii na wabunge.
Alisema wanamshukuru Naibu Spika Job Ndugai kwa kutumia busara na kutoa ufafanuzi kuwa kauli hiyo ni ya upande mmoja na wangependa kusikia kutoka kwa madaktari.
Alitaja baadhi ya maeneo aliyodai kuwa yalipotoshwa akisema kuwa si kweli kuwa huduma zinaendelea kama kawaida katika hospitali tajwa, na kutolea mfano KCMC ambapo taarifa za jana zilionyesha kuwa hali ilikuwa mbaya sana kiasi cha kusitisha huduma zote kasoro huduma ya magonjwa ya ngozi.
“Si kweli kuwa madaktari bingwa walikataa kwenda mikoani, taarifa ya kweli ni kuwa taratibu hazikufuatwa kabisa, badala yake kejeli na ubabe ulitumika huku madaktari bingwa wengi kati yao wakihamishwa kupitia magazetini,” alisema.
Aliongeza kuwa mfano upo wa madaktari ambao walienda kuripoti mikoani wakasumbuliwa na kuzungushwa kupewa masurufu ya safari, hospitali ya mkoa ikimuelekeza kuwa jukumu hilo ni la wizara na wakati huohuo wakienda wizarani wanaambiwa jukumu hilo ni la mikoa.
Dk. Ulimboka alifafanua kuwa mojawapo ya madai ya madaktari ni suala la uboreshaji wa huduma kwa wagonjwa na mazingira ya kazi, akidai kuwa waziri alikwepa na kupoteza muda wa wananchi kuzungumzia propaganda zisizo na tija.
Kuhusu bima ya afya kwa watumishi wa afya, alisema hajatolea tamko lolote na kwamba suala la uwajibishwaji wa watendaji wa wizara akiwemo yeye, alilikwepa kabisa.
“Waziri ametumia muda mrefu kupiga propaganda za mshahara badala ya kusema wao wanatoa ofa gani ili tuelekee kwenye meza ya mazungumzo. Jumuiya ya madaktari inaona kuwa serikali haina nia ya dhati kupata ufumbuzi wa mgogoro huu,” alisisitiza.

No comments:

Post a Comment