NJOMBE

NJOMBE

Monday, February 6, 2012

JK ahofia 2015 CCM kupigwa chini


RAIS Jakaya Kikwete amekiri kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kina hatari ya kuanguka vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ikiwa hali mbaya inayoendelea katika nchi haitarekebishwa.
Kauli hiyo ya kwanza ya aina yake, aliitoa saa chache tu baada ya kutamba kwamba CCM ina uhakika wa kurudisha nafasi zote za uongozi tangu za vitongoji hadi ubunge zilizonyakuliwa na upinzani katika uchaguzi mkuu uliyopita.
Akipokea maandamano ya matembezi ya wana CCM katika viwanja vya Furahisha majira ya saa 5 asubuhi, Kikwete aliwahakikishia waandamanaji hao kuwa chama hicho kimejizatiti kikamilifu na kina uhakika wa kushinda kwa kishindo katika uchaguzi ujao.
Hata hivyo, katika hotuba yake ndefu katika Uwanja wa CCM Kirumba majira ya mchana, Kikwete aligeuka na kukiri kuwa vyama vya upinzani sasa vina nguvu kubwa nchini inayotishia kukishinda chama hicho tawala katika uchaguzi mkuu ujao.
Kikwete alisema hali ya sasa ndani ya chama hicho haiwezi kuleta na kutetea ushindi wake katika chaguzi zijazo ikiwa viongozi wa juu wa CCM hawatachukua hatua za haraka za kuondoa misuguano mikubwa iliyopo.
Kuhusu kujivua gamba

Rais Kikwete katika hilo alisema, “Hivi karibuni nikiwa na NEC hapo Dodoma, nilitumia kauli ‘Nyoka Kujivua Gamba’. Usemi huo ulienezwa tofauti kabisa. Kimsingi tulipitisha maazimio mengi, lakini wenzetu wameona azimio moja tu la kujivua gamba.
Alisema hoja ya kujivua gamba iliyopitishwa na NEC mwaka jana si ya hovyo, hivyo kiongozi na mwanachama yeyote ndani ya CCM anayeuona uamuzi huo ni wa hovyo, basi yeye ndiye wa hovyo mbele ya jamii.
“Haiwezekani tukaendelea kuwa na watu wa hovyo, lazima chama kijipange na kujiweka sawa ili kisipoteze sifa kwa jamii,” alisema Mwenyekiti huyo wa CCM, ambaye alipokea wanachama wapya wapatao 1,847.
Alikiri kuwa ajenda ya watu kujivua gamba imegonga mwamba na kuwatupia mzigo wanachama wake kuwawajibisha viongozi hao na wale wanaowaona hawaendani na maadili wala sera za chama hicho tawala.
Alisema maamuzi ya kujivua gamba hayakulilenga kundi ama watu fulani ndani ya CCM, bali linawahusu wanachama wote wanaojitambua kwamba si waaminifu kujiondoa wenyewe ndani ya chama kwa kuachia nyadhifa za kiuongozi.
“Wito wa kujivua gamba haujapewa mwitikio mzuri. Tumetupa mpira huo kwa wanachama kuwawajibisha viongozi hao, maana tunawafahamu. Sasa kazi kwetu sote,” alisema Rais Kikwete.
Akwepa kuzungumzia mgogoro wa madaktari

Katika hali ya kushangaza, Rais Kikwete alishindwa kabisa kugusia suala zima la mgogoro wa madaktari ambao umelitikisa taifa kwa wiki mbili sasa, akisema atatafuta muda wa kulizungumzia sakata hilo.
Maelfu ya wananchi waliokuwa wamefurika uwanjani hapo walishikwa na butwaa baada ya Kikwete kumaliza hotuba yake bila kugusia jambo hilo.
Watu wengi walisikika wakilalamika na kushutumju vikali hali hiyo, huku mmoja wa watu waliokuwa uwanjani hapo alisikika akidai kuwa serikali ya CCM imejimaliza yenyewe.
Katiba mpya

Rais Kikwete aliwapongeza wabunge wa CCM kwa uamuzi wao wa kuitetea Sheria ya Mabadiliko ya Katiba mpya 2011, na kwamba muswaada huo umeshawasilishwa tena bungeni, hivyo ataunda tume ya kukusanya maoni kwa Watanzania ambapo aliwaomba wana CCM kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao, maana muwamba ngoma huvutia kwake.
“Hili la Katiba mpya tumechukua mapendekezo ya vyama vya upinzani, kikiwemo CCM ambacho nacho kimetoa mapendekezo manane. Nawashukuru sana wabunge wa CCM katika hili, lakini wana CCM jitokezeni kwa wingi kutoa maoni yenu maana muwamba ngoma huvutia kwake.”
Waandamanaji wasombwa kwa malori
Katika kile kilichoonekana kuwa nguvu ya CCM imepotea mjini Mwanza, chama hicho kililazimika kukodisha mabasi na malori maalumu tangu juzi kwa ajili ya kuwasomba watu wa kuhudhuria sherehe hiyo kutoka maeneo kadhaa ya ndani na nje ya Mwanza.
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya watu waliohudhuria walikiri kuletwa kwa magari kutoka katika wilaya kadhaa za mkoa huo na wengine wakitoka mikoa jirani na Mwanza.
Pia katika juhudi za kupata watu wengi uwanjani hapo CCM inadaiwa kuwakodi vijana wengi wasio na kazi maalumu jijini hapa kwa kuwalipa ujira kidogo na kuwapatia fulana, kapelo za chama na chakula.
Imani za ushirikina zajitokeza

Wakati Rais Kikwete akiingia uwanjani hapo, kulijitokeza dalili za uwepo wa vitu vilivyoashiria nguvu za ushirikina, jambo lililoonekana kuwashtua wasaidizi wake wa Usalama wa Taifa.
Wasaidizi wake waliona chupa mbili zilizokuwa zimejazwa vitu vilivyodaiwa kuwa ni dawa za kishirikina, kisha mmoja wao akaipiga teke chupa moja.
Chupa hizo mbili za maji zenye ujazo wa lita moja na nusu, ziliwekwa upande wa kulia na kushoto wa zulia alilotandikiwa Rais kupita kwenda kwenda meza kuu.
Kinana ajuta
MJUMBE wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amesema kitendo cha kuwa Meneja wa Kampeni wa Rais Jakaya Kikwete katika kipindi cha uchaguzi mwaka 2010, kimekuwa kitanzi kwake.
Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akifunga maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa chama hicho, yaliyofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Buguruni.
Kwa mujibu wa Kinana, wananchi na wana-CCM wamekuwa wakitumia umeneja wake kumpatia kero nyingi ili azitolee majibu au kumpelekea Rais Kikwete.
Alisema katika ziara yake ya siku 10 mkoa wa Dar es Salaam, amekuwa akipokea kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.
Hata hivyo, alisema anatarajia kuziwasilisha kero zao kwenye Kamati Maalumu ili zijadiliwe.
Hali hiyo ilitokana na wakazi wengi wa mjini kuonekana kukisusia chama hicho na hivyo viongozi wake wakajawa na hofu ya kupata idadi ndogo ya mashiriki.
Majimbo ya Mwanza ambayo chama hicho kiliyapoteza kwa CHADEMA katika uchaguzi mkuu uliopita ni Nyamagana linaloongozwa na Ezekiel Wenje, Ilemela lililo chini ya Highness Kiwia na Ukerewe, linaloongozwa na Salvatory Machemli

No comments:

Post a Comment