NJOMBE

NJOMBE

Monday, February 13, 2012

Waziri wa Afya kitanzini, Pinda apewa siku saba kueleza madhara ya mgomo wa madaktari

JINAMIZI la mgomo wa madaktari bado linaendelea kuitafuna serikali baada ya jana, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na wanaharakati kutoa matamko mawili tofauti wakitaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Haji Mponda na naibu wake Dk. Lucy Nkya kujiuzulu nyadhifa zao au kuwajibishwa.
Mgomo huo uliokoma kuanzia jana baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kukutana na madaktari na kutangaza uamuzi wa serikali wa kusikiliza madai yao ya posho, umemalizika kwa kusimamishwa kazi kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Blandina Nyoni, na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa.
Wanaharakati pia wamempa wiki moja Waziri Mkuu Mizengo Pinda, awe ametangaza hasara na madhara ambayo wananchi na taifa wamepata kutokana na mgomo wa madaktari uliosababisha vifo kadhaa.
Aidha wamemtaka Spika wa Bunge Anne Makinda kuuomba radhi umma wa Watanzania kutokana na hatua na kauli zake walizodai ni za kibabe ndani ya Bunge za kuzima hoja za wabunge katika kutafakari mgogoro huo.
Akizungumza na madaktari hao juzi, Waziri Mkuu, alitangaza kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk. Deo Mtasiwa, ili kupisha uchunguzi wa vyombo vya dola, dhidi ya tuhuma mbalimbali zinazohusishwa na utendaji wao.
CHADEMA katika tamko lao mbali ya kuwataka viongozi hao wawili wa kisiasa kuwajibika, walieleza kushangazwa na ukimya ulioonyeshwa na Rais Jakaya Kikwete katika kipindi chote cha wiki tatu cha mgomo huo wa madaktari uliosababisha kuzorota kwa huduma katika hospitali zote kuu za serikali.
Mbali ya hilo, chama hicho pia kilielekeza lawama zake kwa Pinda kwa kuchelewa kuchukua hatua za haraka za kuzima mgomo huo hata kusababisha madhara makubwa ya kibinadamu.
Taarifa ya CHADEMA kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, iliuelezea ukimya huo wa Kikwete kuwa kielelezo cha kushindwa kwake kutumia vema madaraka aliyonayo kikatiba.
“Rais Kikwete aliahidi kuzungumzia suala la mgomo wa madaktari lakini mpaka sasa hajatoa kauli, hali inayoashiria ombwe la uongozi,” alieleza Mnyika katika taarifa hiyo.
Hata hivyo, Mnyika alisema kuwa, baada ya Pinda kufikia suluhu na kuahidi kushughulikia matatizo ya madaktari hao na kuwasimamisha kazi Nyoni na Dk. Mtasiwa, wanapaswa kupanua wigo wa uchunguzi.
Chama hicho pia kimetaka tathmini huru kufanyika ili kubaini athari zilizotokana na mgomo wa madaktari ikiwemo kueleza wazi idadi ya vifo vilivyotokea na madhara yake kwenye hospitali mbalimbali za umma.
Wakizungumzia suala hilo, wanaharakati walieleza kushangazwa na hatua ya waziri wa afya na naibu wake kuendelea na kazi hadi hivi sasa, hata baada ya Pinda kusema alikuwa akiiacha hatima yao mikononi mwa Rais Kikwete.
Akisoma tamko la wanaharakati wenzake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Kijo Bisimba, alisema kuwa, wakati Waziri Mkuu akitangaza kung’olewa kwa Katibu Mkuu na Mganga wa Mkuu wa Serikali, wangetarajia kuona Waziri na Naibu wake wakifanya mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kujiuzulu.
Katika tamko lao, walishauri kuwa ni vyema viongozi hao wakafanya uamuzi mgumu sasa wa kujiuzulu badala ya kumsubiri Rais Kikwete kuwaachisha kazi, kwani ukimya wao unamtia majaribuni.
Waliitaka tume iliyoundwa kushughulikia mgogoro huo, itoe taarifa zake kwa umma kila mwezi ili wananchi waweze kufuatilia utekelezaji wa makubaliano.
Walisema serikali imeonyesha udhaifu mkubwa katika kutumia mamlaka iliyopewa na wananchi, hususan wajibu wake wa kusimamia haki za binadamu, hivyo kusababisha madhara makubwa kwa jamii, na kushindwa kutumia raslimali kutatua tatizo hilo.
Kuhusu kukamatwa kwao juzi, Bisimba aliyekuwa ameandamana na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya, waliyekamatwa wote juzi alisema wataendelea kutetea haki za Watanzania pasipo kukoma.
Walisema kukamatwa kwao si mwisho wa kufanya harakati, na kwamba wanachukulia tukio hilo kama motisha katika kuendelea na harakati nyingine.
Madaktari warejea, wagonjwa wasuasua
Wakati madaktari wakirejea kazini jana baada ya kusitisha mgomo wao, huduma katika hospitali imerejea kama kawaida ingawa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), idadi ya wagonjwa ilikuwa ndogo jana.
Ofisa Habari Mwandamizi wa MNH, Aminiel Aligaesha, alisema kuwa mara baada ya kikao cha Waziri Mkuu na madaktari hao, walianza kufanya kazi katika zamu za mchana na usiku.
“Leo tena madaktari wote walikuwa katika maeneo yao ya kazi. Wameanza kurejea katika utaratibu wao, japo changamoto iliyopo hivi sasa ni wagonjwa wachache,” alisema.
Alibainisha kuwa madaktari 15 wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), waliopelekwa kwa dharura hospitalini hapo, hivi sasa wanafanya taratibu za mwisho ili waweze kuondoka.
Habari hii imeandaliwa na Datus Boniface, Lucy Ngowi na Irene Mark

No comments:

Post a Comment