NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 4, 2012

Wabunge CCM wamuwashia moto Kikwete

MOTO umewaka ndani ya kikao cha wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo wawakilishi hao walifikia hatua ya kutoa maneno makali dhidi ya Mwenyekiti wa chama hicho Rais Jakaya Kikwete.
Wabunge hao wamesema hawaridhishwi na mwenendo wa serikali ya Rais Kikwete kiasi cha kufikia hatua ya kutishia kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Wabunge hao pia walipendekeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Haji Mponda, Naibu Waziri Dk. Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Blandina Nyoni watimuliwe kwa kusababisha mgomo wa madaktari uliochangia kuongezeka kwa vifo vya wagonjwa waliokosa huduma za kitabibu katika hospitali mbalimbali nchini.
Wabunge hao waliichachamalia serikali katika kikao cha ndani cha wabunge wa CCM, kilichofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa mjini hapa, chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo.
Vyanzo vyetu vya habari kutoka ndani ya kikao hicho vilisema kuwa pamoja na mambo mengine, wabunge hao walionyeshwa kukerwa na mambo mawili makubwa yaliyofanywa na Rais Kikwete na kusababisha wabunge wake wa CCM waonekane wajinga mbele ya wenzao wa upinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Kwa mujibu wa habari hizo, mambo hayo ni pamoja na suala la posho mpya za wabunge na jinsi Rais Kikwete alivyoamua kumgeuka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Spika wa Bunge, Anna Makinda, juu ya suala la posho za wabunge.
Jambo jingine lililosababisha wabunge hao kumchambua Rais Kikwete ni suala la mabadiliko ya sheria ya Katiba ambapo mapendekezo mengi yaliyopitishwa na wabunge wa CCM bungeni yameondolewa baada ya Rais Kikwete kukubali mapendekezo ya CHADEMA.
Miongoni mwa wabunge waomlipua Rais Kikwete katika kikao hicho, Beatrice Shelukindo (Kilindi), alieleza kutofurahishwa kwake na majibu ya Rais Kikwete kuhusu posho mpya za wabunge.
Mbunge huyo machachari alisema kuwa anashangazwa na serikali ya Kikwete kutokuwa na mawasiliano na viongozi wenzake kiasi cha kutoa majibu yanayotofautiana katika jambo moja, hali ambayo imewashangaza wananchi wengi.
Shelukindo alisema kauli ya Rais Kikwete kusema kwamba hajabariki posho mpya na kwamba hakuna mahali alipotia saini, imewaumbua Spika Anne Makinda na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ambao walitamka hadharani kwamba Rais tayari ameshabariki posho hizo.
Shelukindo alisema pia kwamba Rais amewaudhi katika kushughulia sheria ya mabadiliko ya Katiba, kwani muswada ulioleta sheria hiyo ulipitishwa na wabunge wa CCM baada ya wabunge wa CHADEMA kuususia na kutoka bungeni, lakini baada ya Rais kukutana nao Ikulu, sasa Bunge zima linalazimika kuipitia sheria hiyo kuhalalisha mapendekezo yaleyale yaliyoletwa na CHADEMA.
Shelukindo alisema binafsi anakerwa na tabia ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda kuamua kutenda mambo kana kwamba hawawasiliani.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, Shelukindo alifikia mahali akatishia kuwa kama Rais ndiye tatizo, wabunge wana uwezo wa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye.
Hata hivyo, kauli hiyo nzito ilipingwa vikali na Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka ambaye alimtaka Shelukindo afute kauli yake na kuomba radhi kwani lengo la kumchambua Rais Kikwete na serikali yake, halina nia ya kumuangusha, bali kuisaidia serikali yake.
Kutokana na kauli hiyo, Shelukindo aliomba radhi na kufuta kauli yake, lakini alisisitiza kuwa hakuwa na lengo baya.
Sendeka alijikita kwenye suala la posho na kuwataka wabunge wenzake wa CCM kuachana nayo kwani inawajengea taswira mbaya mbele ya jamii.
Alipendekeza kuundwa tume kuchunguza tuhuma za ufisadi katika Wizara ya Ujenzi inayoongozwa na John Magufuli ambapo inadaiwa kuwa zaidi ya sh bilioni 10 zimechotwa kulipia kampuni hewa ya ujenzi.
Sendeka alisema kuwa katika tuhuma hiyo inayohusisha vigogo wanaotaka kuwania urais, kati ya malipo ya mkandarasi kampuni ya CHICO-CRSG JV, sh bilioni 10 zimeongezwa kwa lengo la kuwanufaisha vigogo hao.
Kuhusu sakata la mgomo wa madaktari, Sendeka alieleza kutoridhika kwake na jinsi serikali ilivyokuwa ikilishughulikia tatizo hilo.
Hata hivyo Sendeka na baadhi ya wabunge walipendekeza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Naibu wake na Katibu Mkuu, wajiuzuru kwa kusababisha kutokea kwa mgomo huo.

No comments:

Post a Comment