NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, February 14, 2012

Muhimbili katika kashfa tena

Imrani Iddy akiwa amelazwa katika wodi ya wagonjwa wanahitaji uangalizi maalum (ICU) kwenye hosipitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam baada ya kudungwa sindano na mmoja wa madaktari wake iliyomsababishia kupooza mwili mzima.
HOSPITALI ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam, imekumbwa na kashfa nyingine inayotokana na mmoja wa madaktari wake, kumdunga sindano mtoto Imrani Iddy na kusababisha apooze mwili mzima.

Habari zilitolewa na wazazi wa Imrani, zilisema mtoto huyo amelazwa  katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu, katika hospitali hiyo.

Wazazi hao walisema mtoto wao amekuwa katika chumba hicho muda wa miezi sita sasa huku akiwa anapoteza fahamu. Kwa mujibu wa habari hizo, mtoto huyo alichomwa sindano hiyo na mmoja wa madaktari katika Kitengo cha Upasuaji.

Hii ni mara ya pili kwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kukumbwa na kashfa ya aina hiyo ndani ya kipindi cha takriban miaka mitano iliyopita. Novemba mosi mwaka 2007, wagonjwa wawili waliokuwa wamelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), iliyoko katika hospitali hiyo, walifanyiwa upasuaji kinyume cha matatizo yaliyokuwa yakiwakabili.

Katika upasuaji huo tata, Immanuel Didas aliyekuwa anasumbuliwa na goti baada ya kupata ajali ya pikipiki, alifanyiwa upasuaji wa kichwa na Immanuel Mgaya aliyepaswa kufanyiwa upasuaji wa kichwa , alifanyiwa upasuaji wa mguu. Katika tukio la mwaka huu lililothibitishwa na wazazi mtoto huyo wa umri wa miaka mitatu, Iramni alichomwa sindano hiyo Julai 28 mwaka jana.

Mama wa mtoto huyo Amina Mwerangi ambaye aliwahi kuwa mshindi wa mashindano ya ulimbwende  katika Mkoa wa Ruvuma mwaka 2003/04, alisema alimpeleka mtoto huyo Muhimbili ili akafanyiwe upasuaji mdogo wa nyama zilizoota puani.
"Baada ya kuchomwa sindano hiyo, mtoto alipatwa na mshtuko uliosababisha mapigo ya moyo wake kusimama. Tatizo hilo sasa limemletea mtindio wa ubongo na kupooza mwili wote," alisema Mwerangi.
Mwerangi alisema jitihada zake za kumpata daktari aliyemchoma sindano hiyo Imrani, hazikuzaa matunda na kwamba Dk Edwin aliyekuwa amfanyie upasuaji huo, hataki kujihusisha na tatizo hilo.
“Mtoto amelazwa ICU kwa miezi sita sasa huku kukiwa hakuna matumaini ya kupata nafuu, jambo la kushangaza ni kuona madaktari wakiwa hawataki kumpa rufaa ili apelekwe nje kwa matibabu zaidi,” alisema mama wa mtoto huyo.

  Alisema  katika upasuaji aliopaswa kufanyiwa, Imrani alifunguliwa jalada lenye namba IP.No.A586301 lililoeleza kuwa alikuwa na tatizo la kuota nyama kwenye njia ya hewa puani na kwamba nyama hizo zilikuwa zinamfanya apate shida katika kupumua.

Alisema mtoto huyo ambaye kabla ya kusababishiwa tatizo hilo jipya alikuwa anasomo katika Shule ya Awali ya Mtakatifu ya mjini Dodoma, alibainika kuwa na ugonjwa huo wakati alipoanza kutambaa.
“Baada ya kumpeleka Hospitali ya Muhimbili katika kliniki ya kawaida, waliniambia kuwa mtoto anapaswa kufanyiwa upasuaji mdogo ili kuondoa nyama hizo na Julai 28 mwaka jana, nilikwenda hospitalini hapo kupata huduma hiyo,” alisema Mwerangi.


 “Nilipokewa na mtoto na siku iliyofuata kwa maana ya  Julai 29 alipelekwa katika chumba cha upasuaji kufanyiwa huduma hiyo, lakini kabla ya hapo alipigwa sindano ya usingizi iliyomsababisha apate mshituko,” alidai mama huyo.

Alisema kutokana hali hiyo, mapigo ya moyo ya mtoto yalionyesha dalili za kusimama na hivyo  akahamishiwa  katika chumba cha wagonjwa wa moyo wanaohitaji uangalizi maalumu.

 “Mtoto  alilazwa katika chumba hicho  hadi Januari 24 mwaka huu, alipohamishiwa katika ICU ya kawaida ambako ndiko aliko hadi sasa,” alisema.
  Mwerangi alisema taarifa ya kitabibu  iliyotolewa baada ya kufanyiwa vipimo vya CT Scan, ilionyesha kuwa  mtoto huyo amesababishiwa mtindio wa ubongo na kwamba mwili wote umepooza.

 “Kila nikiuliza ni daktari gani aliyempiga sindano mtoto, sipewi jibu, kila mmoja anasema hajui na kwamba walimkuta tu ndani ya chumba cha upasuaji akiwa hivyo. Badala yake wananiuliza kuwa kwani  dereva akisababisha ajali na watu wakafa yeye akapona atasimama,” alisema mama wa Imrani.

Mwerangi alisema mbali na kumficha daktari aliyemchoma sindano mtoto, pia amekuwa akinyimwa ruhusa ya kumpeleka nje ya nchi kwa matatibu zaidi.
“Nilikwenda kwa Mkurugenzi wa huduma za tiba ya ugonjwa nyama, akasema  hakuwa na taarifa na akashangaa sana kusikia eti  mtoto amekuwa ICU kwa muda wote huo,”alisema.

  “Aliniambia angezungumza na madaktari waliotaka kumfanyia upasuaji mtoto. Lakini hadi sasa hakuna taarifa wala hatua zozote zilizochukuliwa,” alisisitiza mama Imrani.
 Hata hivyo alimshukuru  Dk Ulisubisya kwa kumpa ushirikiano wa karibu  licha ya ukweli kwamba si daktari aliyemhudumia mtoto.

Alisema pamoja na mambo mengine, daktari huyo ndiye aliyewezesha kupatikana kwa taarifa ya kitabibu za mtoto huyo.
Uongozi wa hospitali

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Muhimbili, Dk Merina Njelekela, na Ofisa Uhusiano wake, Aminiel Aligaeshi, hawakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, licha ya juhudi za kuwatafuta.

Juzi mwandishi wa habari hii alikwenda kwa ofisa uhusiano ili kupata ufafanuzi wa madai hayo, lakini jitihada hizo zililigonga mwamba baada ya kukataliwa kumuona.
 Juhudi  kama hizo ziligonga mwamba pia katika kumpta Dk Njelekele ofisini kwake, kufuatia kitendo cha wasaidizi wake kumzuia mwandishi kuonana naye kwa maelezo kuwa ana kazi nyingi.

 Hata hivyo, Ofisa Uhusiano Msaidizi wa hospitalini hiyo, Jeza Waziri, ambaye awali alisema hawezi kuzungumza lolote, alisema hakuwa na  taarifa kuhusu tukio hilo.

No comments:

Post a Comment