NJOMBE

NJOMBE

clock

Saturday, February 4, 2012

Kikwete ataka kutoa adhabu badala ya kifungo

Rais Kikwete Ikulu katika mkutano wa Sheria
RAIS Jakaya Kikwete, ameuagiza mhimili wa mahakama nchini kuhakikisha unatoa elimu kuhusu adhabu mbadala ya kifungo katika kesi za jinai, kwa kuwa hatua hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani.
Rais Kikwete, alitoa wito huo jana katika sherehe za Siku ya Sheria Nchini, iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ikiwa ni ishara ya ufunguzi rasmi wa shughuli za mhimili huo kwa mwaka huu, chini ya kauli mbiu ya ‘Adhabu mbadala ya kifungo katika kesi za jinai: faida kwa jamii’.
Alisema adhabu hiyo hutolewa chini ya Sheria ya Huduma ya Jamii ya mwaka 2002, na kwamba endapo mhimili huo utatoa elimu kwa umma kuhusu faida ya mahakimu na majaji kuamua kutumia adhabu mbadala katika kesi za jinai kwa watuhumiwa ambao adhabu zao ni ndogo, utapunguza msongamano magerezani.
Rais Kikwete alisema mbali na kupunguza msongamano, pia kutawafanya wale wahalifu waliofungwa vifungo vya nje kuwa karibu na jamii na kufanya shughuli nyingine za jamii, hivyo kujirudi kitabia.
Aliahidi kupigania mfuko wa mahakama ili uongezewa fedha na stahili nyingine za majaji zinaboreshwa ili mhimili wa mahakama uweze kufanya kazi zake kikamilifu.
Kwa upande wake Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman, alisema kwa watu wengi Sheria ya Huduma ya Jamii ni kitu kipya kwani kuna baadhi ya mahakimu bado wanasisitiza kutoa adhabu mbadala, ila wanahofia kuonekana wadhaifu wa uhalifu na kwamba mahakama za Mwanzo zina muamko zaidi kuliko mahakama za wilaya au zile za Hakimu Mkazi.
“Safari huanza kwa hatua...sheria hii ina upeo lakini haijatumiwa kikamilifu. Kwanza, sheria hiyo inatumika kwenye mikoa 12 tu. Pia tangu ianze kufanya kazi mwaka 2005 hadi kufikia Oktoba mwaka jana ni wafungwa 3,144 tu walioadhibiwa kwa amri za hudumia ya jamii na waliotoroka ni 23, mafanikio ya kishindo yatapatikana ikiwa wote watashirikiana na kushikamana,” alisema Jaji Othman.
Jaji Othman alisema ni vigumu kwa mahakama kwa hali iliyonayo kupata mafanikio yanayoonekana wazi ikiwa fedha za matumizi ya kawaida zitaendelea kuwa pungufu mno na kupatikana bila uhakika.
Fedha za matumuzi ya kawaida ambazo ziliainishwa kwenye bajeti ya 2011/2012 kwa ajili ya mahakama kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2011 zilikua sh bilioni 13.8 katika kipindi hicho mahakama imepokea sh bilioni 8.7 pungufu kwa sh bilioni 5.1.
“Hali hiyo imekuwa inachangia kukwamisha uendeshaji wa mahakama, tunashindwa kuwalipa wafanyakazi haki zao wanazostahili. Tunakuomba Rais Kikwete utupatie hiyo pungufu ya fedha iliyosalia ili tuweze kufanya kazi za mahakama vizuri,” alisema Jaji Othman.
Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisema ofisi yake inatoa wito kwa wadau wa sheria pamoja na jamii kwa jumla kuachana na fikra zinazotukuza adhabu ya kifungo pale ambapo adhabu mbadala inaleta matunda mazuri zaidi kwa mhalifu na kwa jamii husika.
Aidha Rais wa Chama cha Wanasheria Nchini (TLC), Francis Stola, alisema jamii haina budi kubadilika na kuanza kuikubali adhabu mbadala katika kesi za jinai kwa kuwa msongamano ulioko magerezani unavunja haki za msingi za binadamu.

No comments:

Post a Comment