NJOMBE

NJOMBE

clock

Thursday, February 2, 2012

UGONJWA WA MWAKYEMBE: Sitta amtwisha zigo Pinda

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amemtwisha mzigo wa lawama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwa kushindwa kuueleza umma ugonjwa unaomsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe.
Sitta alisema kuwa anashangazwa na ukimya huo wa Pinda kwakuwa Dk. Mwakyembe alishatoa idhini kwa serikali kuuzungumzia ugonjwa wake, hasa baada ya madaktari waliokuwa wakimtibu katika Hospitali ya Apollo iliyopo nchini India kuwasilisha ripoti serikalini.
Waziri Sitta, alitoa kauli hiyo jana mjini hapa, alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu  kuhusu ukimya wa serikali juu ya afya ya Dk. Mwakyembe ambaye alidai amelishwa sumu na watu aliowaita ni mahasimu wake kisiasa.
Alisema kuwa ripoti ya ugonjwa wa Dk. Mwakyembe ipo Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, hivyo hakuna sababu yoyote kwa serikali kuificha.
Akizungumza kwa kujiamini, Sitta alisema hata kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwamba mwenye haki ya kueleza siri ya ugonjwa wake ni Dk. Mwakyembe si sahihi, kwani suala hilo linahusu jinai, hivyo serikali inawajibu wa kulizungumzia.
Kauli ya Sitta inakinzana na ile aliyoitoa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hivi karibuni kuwa serikali haiwezi kuzungumzia ugonjwa unaomkabili mtu, bali mhusika ndiye mwenye wajibu wa kueleza umma nini kinamsumbua.
Sitta, pia amesisitiza kuwa Dk. Mwakyembe amelishwa sumu na anazo sababu nne za kuamini jambo hilo.
Sitta alisema anashangazwa na kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, kumtaka apeleke ushahidi wakati suala la kuchunguza madai hayo liko chini ya polisi wake.
Waziri huyo alizitaja hoja nne kuthibitisha kwamba naibu waziri huyo amelishwa sumu kuwa ni pamoja na aina ya ugonjwa na mwonekano wa mgonjwa mwenyewe kwamba si wa kawaida.
“Mimi nina bahati ya kumtembelea nyumbani kwake mara kwa mara. Dk. Mwakyembe anapokaa, mfanyakazi wake kila baada ya muda anakuja kufagia unga unaoanguka kutoka miguuni mwake. Miguu yake imevimba na kuchanika mithili ya tembo. Je, huo ni ugonjwa gani?” alihoji Waziri Sitta.
Kwa mujibu wa Sitta, sababu ya pili kuthibitisha Mwakyembe kalishwa sumu ni pale madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili waliposhindwa kubaini aina ya ugonjwa na kushauri aende India kwa uchunguzi zaidi.
Aliitaja sababu ya tatu kuwa ni vitisho alivyokuwa akipata Dk. Mwakyembe kutoka kwa mahasimu wake wa kisiasa kwamba angeuawa kwa ajali ya gari ya kupangwa au sumu na mara zote alitoa taarifa polisi, lakini hazijafanyiwa kazi.
“Kwanini tusiamini kama kalishwa sumu?” alihoji.
Waziri Sitta alisema sababu ya nne ni ukimya wa serikali katika kuzungumzia suala hilo.
Alisema taarifa ya ugonjwa wa Dk. Mwakyembe kutoka kwa madaktari wa Hospitali ya Apollo nchini India iko Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, na akashangaa kwa nini inaona ugumu wa kuitangaza wakati mwenyewe ameridhia.
Sitta alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa uchunguzi aliofanyiwa Dk. Mwakyembe nchini India kwa kuchukua kucha, ngozi na uboho, umeonyesha kwamba Dk. Mwakyembe alilishwa sumu.
Waziri huyo alisema Dk. Mwakyembe anatarajiwa kwenda tena India Februari 19 mwaka huu na atakaporejea nchini ameahidi kupasua jipu juu ya ugonjwa wake.
Sitta alililaumu Jeshi la Polisi kupuuza madai ya vitisho vya kuuawa kwa baadhi ya viongozi, akiwamo yeye pamoja na watu binafsi.
Akitolea mfano, alisema aliwahi kupeleka taarifa za kutishiwa kuuawa mjini Dodoma wakati huo akiwa Spika wa Bunge, lakini Jeshi la Polisi mkoani humo hadi leo halijazifanyia kazi taarifa hizo wala kumpa majibu ya kuridhisha.
Alisema kuwa mbunge mmoja aliwahi kunasa mazungumzo ya watu fulani hapa Dodoma wakipanga kuligonga gari lake (Sitta), na kwamba alipeleka taarifa hizo polisi lakini hawakuzifanyia kazi.
Kwa muda mrefu Dk. Mwakyembe amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa ambao hadi sasa haujaelezewa hadharani huku taarifa zisizo rasmi zikidai amelishwa sumu.
Ugonjwa huo umemfanya anyonyoke nyusi, ndevu na vinyweleo, huku ngozi yake ikielezwa kutoa unga na miguu yake kupasuka mithili ya mtu mwenye magaga. Hali hiyo inadaiwa kumbadilisha kabisa muonekano wake wa asili.

No comments:

Post a Comment