NJOMBE

NJOMBE

Wednesday, February 8, 2012

NEC yatoa tamko uchaguzi Arumeru Mashariki

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kwamba Uchaguzi mdogo wa jimbo loa Arumeru Mashariki utafanyika Aprili Mosi mwaka huu na kuonya kuwa hakutakuwepo na uandikishaji wa wapigakura wapya bali watatumika wale ambao walijiorodhesha kwenye daftari kwenye uchaguzi mkuu 2010.
Uchaguzi huo unafuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Jeremia Sumari kilichotokea Januari 19, mwaka huu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu.
“Baada ya Tume kupokea taarifa hiyo ya kuwepo nafasi wazi kwa Jimbo la Arumeru Mashariki, Tume  imepanga kufanya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo hilo kwa mujibu wa sheria,” alisema Mwenyekiti wa NEC, Damian Lubuva kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Alisema kwamba tayari wametoa ratiba ya uchaguzi huo pamoja na wa kata nane ili kujaza nafasi za madiwani zilizowazi na kuonya: “Ifahamike kwamba, hakutakuwa na kuandikisha Wapiga Kura kwa ajili ya Chaguzi hizo. Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, ndilo litakalotumika.”

Vile vile alisema vituo vya kupigia kura kwenye uchaguzi  huo ni vile vilivyotumika kwenye chaguzi mkuu uliopita na kwamba watabandika orodha ya wapiga kura kwa siku saba kabla ya uchaguzi.
“Wananchi wote wa Jimbo la Arumeru Mashariki na Kata zote ambazo Chaguzi Ndogo zitafanyika mnaombwa kwenda katika vituo vyenu vya Kupiga Kura na kukagua majina yenu ili kujua Vituo mtakavyo pigia Kura,” alisema Lubuva.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo alisema uteuzi wa wagombea utafanyika Machi 8 na kampeni zitaanza siku inayofuata na kumalizika mwishoni mwa mwezi huo.

Katika hatua nyingine, Lubuva alisema wamepanga kufanya chaguzi za kujaza nafasi zilizo wazi katika kata nane, Vijibweni Halmashauri ya Temeke, Kiwangwa halmashauri ya Bagamoyo, Kirumba (Mwanza), Lugangabilili (Bariadi), Chang’ombe (Dodoma), Kiwira (Rungwe), Lizaboni (Songea) na Msambweni (Tanga).

No comments:

Post a Comment