NJOMBE

NJOMBE

clock

Friday, February 3, 2012

Madaktari watikisa Bunge

MGOMO wa madaktari umelitikisa Bunge ambapo sasa limetishia kutoendelea na shughuli zake endapo serikali haitotoa hatima ya mgomo huo leo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge jana.
Ndugai alisema anashangazwa na ukimya wa serikali kwani iliahidi tangu juzi kutolea kauli, lakini hadi jana haijasema chochote huku mgomo huo ukiendelea kushika kasi na hali za wagonjwa zikizidi kuwa mbaya.
“Ninaiagiza serikali kesho iwe imeleta maelezo yake bungeni, vinginevyo shughuli za Bunge zitavurugika kwa wabunge kutaka kujadili hali hiyo,” alisema Naibu Spika huyo.
Huku akiungwa mkono na wabunge wengi kwa kupiga piga meza zao, Ndugai alisisitiza kuwa jambo hilo ni la dharura, hivyo linapaswa kuwa na ufumbuzi wa haraka badala ya kuendelea kuchelewa kulishughulikia.
Akitolea mfano alisema juzi nchini Misri, zaidi ya watu 78 walifariki katika uwanja wa mpira na Bunge la nchi hiyo ambalo lilikuwa likizo kwa wakati huo, liliitwa kwa dharura kujadili hali hiyo.
“Mgomo wa madaktari wetu una zaidi ya wiki mbili sasa na hatujui umesababisha vifo vya watu wangapi, lakini serikali iko kimya kabisa. Tunaitaka serikali leo ije na kauli yake juu ya hatma ya mgomo huo,” alisema Ndungai.
Awali kabla ya kutoa kauli hiyo, Ndugai alizima mwongozo wa Spika uliotolewa na Mbunge wa Kigamboni, Dk. Faustine Ndungulile (CCM), na John Mnyika (Ubungo), ambao kwa nyakati tofauti walisimama kutaka kujua kauli ya serikali na pia Bunge kuvunja shughuli zake za jana kwa ajili ya kujadili hoja ya mgomo wa madaktari.
Mnyika alisema kwa kuwa jambo hilo ni la dharura na tayari limeshaleta madhara makubwa, aliliomba Bunge kuvunja shughuli zake ili kujadili hatma ya mgomo huo wa madaktari.
Akitoa mwongozo wa hoja za wabunge hao, Ndugai alisema kuwa wabunge hao wako sahihi, lakini wakitoa hoja hiyo, wabunge wanaounga mkono walipaswa kusimama kwa mujibu wa kanuni ili kuiunga mkono.
“Wabunge hao wako sahihi, wametumia kanuni vizuri, tatizo ni moja tu wakati wanatoa hoja hiyo, wabunge wanaounga mkono kutaka shughuli za Bunge leo zivunjwe kutoa nafasi kujadili hoja hiyo, walipaswa wote wasimame, hivyo naitupa hoja hiyo kwa sasa,” alisema Ndugai.
Madaktari watoa tamko
KAMATI ya Jumuiya ya ya Madaktari imetoa tamko na kukataa mpango wa madaktari bingwa wa kuonana na Waziri Mkuu Mizngo Pinda, wakisema kuwa jumuiya hiyo imepewa mamlaka kuratibu madai ya madaktari.
Alisema jumuiya hiyo pia inaratibu madai ya madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Mhimbili ambao juzi waliunda kamati ya watu watano kwenda kumuona Pinda kwa ajili ya kutafuta suluhu ya mgomo uliodumu kwa takriban wiki mbili sasa.
Akizungumza na waandishi habari jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk.Stephen Ulimboka, alisema kuwa uamuzi huo umetokana na kikao kati ya madaktari bingwa na kamati ya jumuiya ya madaktari.
Alisema kuwa mpango mkakati wa madaktari bingwa hauna jukumu la upatanishi na hata siku moja madaktari hawakuwahi kukaa na kuteua kikodi kazi cha upatanishi.
Dk. Ulimboka alisema kuwa jukumu pekee la kikosi kazi kilichoundwa Muhimbili ni kuishinikiza serikali itoe majibu kwa tuhuma zilizo mbele yake na si kwa jumuiya ya madaktari.
Hali bado tete Muhimbili
HALI imeendelea kuwa tete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kutokana na mgomo wa madaktari unaoendelea hospitalini hapo.
Wagonjwa mbalimbali waliolazwa katika wodi ya Mwaisela, Kibasila na Sewa Haji wamewaambia waandishi wa habari waliotembelea wodi hizo jana kuwa wanaiomba serikali kukaa pamoja na madaktari ili kuweza kutatua mgogoro huo.
Hata hivyo, meneja wa kitengo cha magonjwa ya dharura, Silanda Optatus, aliwaambia waandishi wa habari kuwa huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida ingawa kuna tofauti kubwa ya wagonjwa wanaoingia katika kitengo hicho.
Alisema hapo awali kwa siku walikuwa wanapokea wagonjwa 80 hadi 100 lakini kwa sasa wanapokea wagonjwa 25 na wote wakipatiwa huduma.
Wakati huohuo,Mwenyekiti wa Chama cha NCCR Mageuzi, James Mbatia, aliyetembelea hospitalini hapo kwa ajili ya kuwapa pole wagonjwa, alisema hali ni mbaya na kwamba serikali isifanye mzaha na masiaha ya watu.
Alisema kuwa alitembelea hospitali ya Amana na kijionea hali mbaya pia kama ilivyo Muhimbili kutokana na hivyo kuitaka serikali kuchukua hatua za makusudi kunusuru hali hiyo.
Aidha alisema kuwa kama mgogoro huo hautasimamiwa na kupatiwa ufumbuzi ndio utakaoiondoa serikali madarakani.
Aliwaomba madaktari watumie hekima kupitia kwa Waziri Mkuu Pinda ambaye hapo awali serikali ilimtumia katika kutoa kauli ambayo haijazaa matunda.
Habari hii imeandaliwa na Martin Malera, Chalila Kibuda na Asha Bani

No comments:

Post a Comment