NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 18, 2012

Liyumba kusimama kizimbani tena Machi 15

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imeshindwa kumsomea maelezo ya awali aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, anayekabiliwa na kesi ya kukutwa na simu kwenye gereza la Ukonga, kutokana na wakili wake anayemtetea Majura Magafu kutokuwapo mahakamani.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Elizabeth Kaganda, jana alidai mbele ya Hakimu Mkazi Stuart Sanga, kuwa kesi imekuja kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali yanayohusiana na mashtaka yanayomkabili.

Baada ya kutoa maelezo hayo, Liyumba aliieleza mahakama kuwa wakili wake hayupo amekwenda mkoani Arusha kuhudhuria mkutano.Hivyo, Hakimu Sanga aliiahirisha kesi hiyo hadi Machi 15, mwaka huu itakapopelekwa tena kwa ajili ya Liyumba kusomewa maelezo ya awali.

Hatua hiyo ilikuja baada ya Mahakama ya Kisutu kulitupilia mbali ombi la Liyumba kutaka afutiwe kesi hiyo kwa sababu, haina mamlaka ya kuisikiliza.

Liyumba kupitia kwa Wakili Magufu aliwasilisha pingamizi hilo la awali akidai mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza, kwa sababu taratibu za awali za sheria ya Magereza ya mwaka 2002 hazikufuatwa.

Wakili Magafu alidai kwa mujibu wa Sheria ya Magereza ya mwaka 2002, inataka mshtakiwa anayeishi mahabusu kabla hajaletwa mahakamani asomewe mashtaka na ofisa wa magereza gerezani, iwapo atapatikana na hatia atapewa adhabu.
Alidai kuwa iwapo mshtakiwa huyo ataonekana amekuwa mtendaji sugu wa makosa akiwa gerezani,  italazimika afunguliwe mashtaka katika mahakama za uraiani.

Akipangua hoja za upande wa utetezi, Wakili wa Serikali Eliezabeth Kaganda, alidai kuwa kesi ya aina hiyo inayomkabili Liyumba siyo ya kwanza kufunguliwa mahakama nchini.

Kaganda alitaja kesi ya jinai Na. 472/2009 iliyokuwa ikimkabili Juma Matonya katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke na Hakimu Mzava alimhukumu kifungo cha miezi sita jela baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kukutwa na simu gerezani.Kesi nyingine mbili za aina hiyohiyo, ambazo washtakiwa walitiwa hatiani moja akitakiwa kulipa faini ya Sh20,000 na nyingine kwenda jela miezi sita.

 Wakili Kaganda alieleza kuwa kabla hawajamfikisha Liyumba mahakamani hapo Jeshi la Magereza lilikuwa na mamlaka ya kushughulikia tuhuma zilizokuwa zikimkabili mshtakiwa na kwamba, mkurugenzi wa mashtaka na maofisa wa magereza walikuwa wameishaamua kuifungua kesi hiyo mahakamani hapo.

Lakini kwa sababu hiyo haikuwa mara ya kwanza kukutwa na simu gerezani na alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la damu, hivyo haikuwa rahisi kumpa adhabu akiwa gerezani.

Awali, Septemba 8, mwaka jana Liyumba alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza akikabiliwa na shtaka la kukutwa na kitu kilichokatazwa gerezani chini ya kifungu cha 86 (1,2) cha sheria ya Magereza kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Liyumba ambaye wakati huo alikuwa mfungwa mwenye Na.303/2010, Julai  mwaka jana, aliyokuwa akitumia kufanyia mawasiliano binafsi wakati ni kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment