NJOMBE

NJOMBE

Monday, February 6, 2012

Mhadhiri UDSM aumbuliwa na wasomi

MHADHIRI mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk. Benson Bana, ameshushuliwa na wasomi, wananchi na wadau wa demokrasia nchini, kufuatia kauli yake kuwa mpaka sasa hajaona chama mbadala cha kuongoza nchi zaidi ya CCM.
Akizungumza jana katika kipindi cha tuongee asubuhi kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Startv, Dk. Bana, ambaye ni mwenyekiti mwenza ya Taasisi ya Utafiti wa Elimu ya Demokrasia Tanzania (Redet), alisema kutokana na asilimia kubwa ya kura za udiwani, ubunge na urais ilizozipata CCM ni wazi kuwa bado wananchi wana imani nayo.
Alisema jambo la msingi kwa chama hicho sasa ni kujirekebisha na kujipanga upya kwa kushughulikia malalamiko yanayotolewa na wanachama, vinginevyo kitakuwa kimejiweka tayari kuchukua nafasi ya upinzani baada ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Hata hivyo, mtazamo na kauli za msomo huyo, ulipokelewa kwa hisia tofauti na wadau mbalimbali wakimtuhumu kuwa anafanya kazi ya kukisafisha chama hicho kwa muda mrefu licha ya kufahamu ukweli kuwa vyama vya upinzani vimeimarika na kuonekana vinaweza kuwa mbadala.
Wengi walionekana kukitaja moja kwa moja Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wakisema kwa namna kilivyojipambanua kabla na baada ya uchaguzi mkuu kwa kuweza kusimamia masuala ya msingi ya kitaifa ni wazi kinakidhi haja ya kuwa mbadala wa CCM.
Katika maoni mbalimbali yaliyoandikwa na wadau hao kwenye mitandao ya kijamii, walisema Redet haijawahi kufanya kazi kwa maslahi ya nchi isipokuwa mara zote imekuwa ikifanya kazi ya propaganda kwa niaba ya CCM.
Dk. Bana amewekwa pale na ndugu yake Mukandara, ambaye kwa kweli ameshindwa kuiongoza UDSM kama msomi. Mtakumbuka wakati ule wa uchaguzi wa 2005 na 2010 jinsi taasisi hiyo ilivyotumika.
Hata hivyo ilipata aibu mara zote kwani maeneo yote ya wasomi, CCM ilipata kura kidogo mno za wale walamba magamba.
“Huu ndiyo ubaya wa elimu ya kukariri inayokupa cheti na siyo uelewa, pamoja na elimu yake yote anashindwa kusoma hata alama za nyakati au anaongea kuwafurahisha watu fulani?” alihoji mchangiaji mmoja.
Mchangiaji mwingine, alisema ingawa Dk. Bana hakuzungumza kama mwakilishi wa Redet, ila wangemshauri kuwa kwa vile yeye ni mwenyekiti mwenza wa taasisi hiyo awe anajitahidi kutoa maoni yanayoakisi hadhi na heshima ya taasis hiyo maana kauli yake yoyote anayoitoa inatafsiriwa kuwa ni kauli ya Redet.
“Tufahamu kuwa Redet ya kweli ilikuwa ile ya kina Prof. Mwesiga Baregu, marehemu Prof. Samuel Mushi, na wengine. Dk. Bana hana jipya, ametumia takwimu za 2010 ambazo ni za muda mrefu, kwa nini asingetumia takwimu za Igunga?” Aliuliza mchangiaji mwingine.
Katika mjadala huo kwenye mtando, mchangiaji mwingine alihoji mhadhiri huyo ana maana gani hasa anaposema mbadala. Mbadala kwa vipi? kwa wizi? Kwa kutofanya maamuzi, kwa kuvuruga uchumi, au kwa kutotatua migogoro ya wafanyakazi?
“Nini hasa ulimaanisha Dk. Bana. Na kwa nini Redet haijafanya utafiti tangu uchaguzi mkuu 2010 uishe ili itueleze maoni ya wananchi yakoje?” alihoji mchangiaji huyo.
Mwingine alisema kuwa tatizo ni kuwa wasomi wetu wanazungumza huku wakiwa na maslahi fulani, hivyo anahisi hata Dk. Bana anaogopa kivuli chake mwenyewe na kuamini kama kweli kauli yake ina uhalisia. Tumsamehe!
Lakini wakati wengi wakimpinga Dk. Bana, mchangiaji mmoja alimtetea akiungana naye kuwa alichokisema ni kweli kabisa kwani mpaka sasa vyama vya upinzani bado havijaonyesha mfano wa kuongoza zaidi ya kupiga kelele.
“Wanachojivunia zaidi wapinzani ni mwamko wa wananchi kutaka wawapigie kura lakini wamejipanga vipi katika kuendeleza taifa hili au ni kuwatoa madarakani CCM tu?
“Mimi naungana naye kuwa bado hakuna mbadala ingawa chama kimeonyesha mapungufu katika baadhi ya maeneo lakini ni chama imara,” alisema.
Kwa mtazamo wa mchangiaji huyo, anamini kuwa CCM inaruhusu mawazo tofauti kutoka ndani na nje ya chama, jambo alilodai ni gumu kuthubutu kufanywa na vyama vingine.

No comments:

Post a Comment