NJOMBE

NJOMBE

Friday, July 6, 2012

UN haitafadhili jeshi kukomboa Mali

Wapiganaji wa Kiisilamu wakiharibu makaburi ya kale
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linasema haliko tayari kuunga mkono harakati za jeshi la kanda ya Afrika Magharibi katika kukabiliana na wapiganaji wa Kiisilamu ambao wameteka kaskazini mwa Mali.
Baraza hilo limelaani uharibifu,wa makuburi na minara ya kale katika mji wa Timbuktu ambao umewekwa chini ya urithi wa dunia na kusema uharibifu huo ni sawa na uhalifu wa kivita. Muungano wa kanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS unanuia kutuma wanajeshi 3,00 nchini Mali.
Hata hivyo afisa wa kibalozi wa Umoja wa Mataifa ameambia BBC kwamba Baraza hilo limeomba kupata taarifa zaidi, ili kujua malengo ya harakati za jeshi la ECOWAS kabla ya kufadhili. Majirani wa Mali wametaka Umoja wa Mataifa kuunga mkono pendekezo lao kwa hofu ya maasi kusambaa katika maeneo mengine nje na Mali.
Kundi la Ansar Dine lenye uhusiano na mtandao wa Al Qaeda liliuteka mji wa Timbuktu mapema mwaka huu.Kundi hilo tayari limeharibu madhabahu ambayo linasema yamejengwa kinyume na imani ya Kiisilamu.
Msemaji wa Ansar Dine Sanda Ould Bamana aliambia BBC Sharia ya Kiisilamu hairuhusu makaburi yaliyojengwa kwa urefu wa zaidi ya inchi sita. Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi na Utamaduni{UNESCO} pamoja na serikali ya Mali zimeomba kundi la Ansar Dine kusitisha harakati za kuharibu turathi hizo.
UNESCO pia imeelezea wasi wasi kwamba nyaraka za kale na vifaa vingine muhimu huenda vikaporwa na kuvukishwa kimagendo na imeziomba nchi jirani kuzuia kosa hilo kufanyika.
Timbuktu imepata sifa za kimataifa kutokana na eneo hilo kua moja wapo ya kitovu cha mafunzo ya imani ya Kiisilamu hususan misikiti yake iliyojengwa karne za 15 na 16. Timbuktu pia wanatoka Mawalii 333 ambao wanaheshimiwa sana katika madhehebu ya Sufi.
Ansar Dine ambao wana msimamo mkali{Salafist} wanapinga heshima kwa Mawalii.Waliuteka mji wa Timbuktu baada ya mapinduzi ya kijeshi kutokea. Katika mwanzo wa harakati za kutwaa kaskazini mwa Mali Ansar Dine walishirikiana na wapiganaji wa Tuareg waliotaka kujitenga na Mali.
Hata hivyo makundi hayo yametofautiana katika siku za karibuni hali iliyosababisha makabiliano makali katika maeneo matatu muhimu ya Mali ikiwemo Timbuktu, Gao na Kidal.

No comments:

Post a Comment