NJOMBE

NJOMBE

Thursday, February 2, 2012

Muhimbili kumwangukia Pinda

MADAKTARI bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wameingilia kati suala la mgomo wa madaktari walioko kwenye mazoezi na kuunda timu ya watu watano kwa ajili ya kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ili kumaliza tatizo hilo.
Ofisa Habari Mwandamizi wa MNH, Aminieli Aligaesha, alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa madaktari bingwa na Mkurugenzi Mtendaji wao, Dk. Marina Njelekela.
Alisema katika mkutano huo, madaktari waliielezea hali ya hospitalini hapo kuwa si nzuri, hivyo ni vema wakakutana na Pinda kwa ajili ya kupata suluhu ya mgogoro huo.
Aligaesha alisema madaktari hao walisema kuna haja ya kwenda kumuona Pinda ili kurahisisha mazungumzo baina ya serikali, madaktari na wauguzi waliogoma.
Alikiri kuzorota kwa huduma mbalimbali hospitalini hapo, zikiwamo za upasuaji na wagonjwa wanaohudhuria kliniki mbalimbali.
Wakati huo huo, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya Tanzania (TUGHE), kimetoa tamko la kuitaka serikali kufanya mazungumzo na kamati teule ya madaktari na wauguzi haraka iwezekanavyo ili kuwanusuru wagonjwa katika hospitali mbalimbali nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa TUGHE, John Sanjo, alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mgogoro wa masilahi ya madaktari, wauguzi na wafanyakazi wote wa afya.
Alisema serikali ndiyo imesababisha mgogoro huo kuwapo kwa kutofuata mkataba waliojiwekea na wafanyakazi hao wa Idara ya Afya.
“Serikali imezembea kwa kutoheshimu mikataba hiyo. Huu ni mgogoro wa masilahi wa madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa kada ya afya,” alisema.
Sanjo aliwataka wafanyakazi hao waliogoma kurudi kazini pale mazungumzo yatakapokuwa yanaendelea, kwa kuwa kinaamini kuwa mazungumzo ya pamoja na ya haraka ndiyo suluhisho la Watanzania kuendelea kupata huduma.
Awali katibu huyo wa TUGHE alisema kuwa chama kinaunga mkono madai yote yaliyotolewa na madaktari kwa kuwa ni haki yao ya msingi, pia madai ya wauguzi ambayo wanaidai serikali ikiwamo kupewa kurugenzi yao.
Kauli ya CCM kuhusu madaktari
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (CCM) wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ilisema kuwa mgomo huo umekuwa na athari kubwa kwa Watanzania maskini ambao ni wengi, kiasi cha kugharimu hata maisha yao .
“Chama Cha Mapinduzi kinachukua nafasi hii kuwapa pole sana wale wote walioathiriwa kwa namna moja ama nyingine na mgomo huu. Na kwakweli tunasikitishwa sana na hali inayoendelea,” alisema Nape.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, CCM inawapongeza na kuwashukuru madaktari walioonyesha ubinadamu na uzalendo kwa kuamua kurudi kazini na ambao hawakugoma kabisa kwani wametambua kuwa hakuna masilahi yanayovuka thamani ya uhai wa binadamu wenzao.
‘Tunachukua fursa hii pia kuwashukuru sana na kuwapongeza askari wetu wa Jeshi la Wanachi wa Tanzania kwa uamuzi wao wa kizalendo wa kuamua kuitikia wito wa serikali kwenda kwenye baadhi ya hospitali kusaidia kuwatibu Watanzania wenzao. Moyo huu ni wa kizalendo na wa mfano. Tunajivunia uzalendo wa jeshi letu.
“Tunachukua nafasi hii kuwaomba madaktari wanaoendelea na mgomo kurudi kazini huku wakiendelea na mazungumzo na serikali. Tunaamini madai yao yanawezekana kushughulikiwa ikiwa pande zote mbili zitaamua kukaa chini kwa dhati na kuzungumza,” alisema Nape
Kwa upande wa serikali, Nape aliwataka watafute kwa makini chanzo cha mgogoro huu na kutafuta majibu, na madaktari nao kwa upande wa pili, wawe tayari kukaa mezani na kuzungumza.
Aliitaka serikali kujenga utamaduni wa kushughulikia matatizo haya ambayo yanaathiri wananchi wengi kwa uharaka na udharura unaostahili badala ya kusubiri hali inapokuwa mbaya zaidi.

No comments:

Post a Comment