NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 11, 2012

Madactari warudi vitengoni mwao


Daktari Bingwa katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili, Prof.William Matuja akitoa maelekezo kwa madaktari wa vitendo jinsi ya kuudumia mgonjwa, George Masubu, anayesumbuliwa na tumbo aliyelazwa katika wodi namba 6-Mwaisela baada ya madaktari hao kuanza kazi rasmi jana kufuatia kumalizika kwa mgomo jijini Dar es Salaam. Picha na Venance Nestory
HUDUMA za matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (MOI) jana zilirejea katika hali yake ya kawaida baada ya madaktari waliokuwa kwenye mgomo, kurudi kazini huku makundi ya wanaharakati yakiongeza shinikizo la kung’olewa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya.Madaktari hao wamerejea kazini baada ya mgomo huo  uliochukua siku 17 kushinikiza Serikali itekeleze madai yao kadhaa, likiwamo suala la nyongeza ya posho na kuwajibishwa watendaji wakuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kutekelezwa.
Mgomo huo ulimalizika juzi baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kukutana na madaktari hao jijini Dar es Salaam na kuahidi kutekeleza baadhi ya madai yao, huku akiwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Deo Mtasiwa.
Hatua hiyo ya Serikali ilitokana na tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwa watendaji hao, ikiwamo kashfa ya kudaiwa kuingiza nchini robo tatu ya vifaa bandia vya vipimo vya Ukimwi kutoka Korea Kusini, kuanzisha kampuni ya kusambaza nguo kwa madaktari na wauguzi na kuiingiza kinyemela kampuni inayofanya usafi ndani ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.


Jana Ofisa Habari Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aliegaesha alilithibitishia gazeti hili kuwa huduma katika hospitali hiyo, zimerejea katika hali ya kawaida ingawa idadi ya wagonjwa waliojitokeza, bado ni ndogo ikilinganishwa na siku za nyuma.
“Madaktari wa JWTZ wameondoka leo (jana), hii ni kutokana na kurejea kwa madaktari wote waliokuwa kwenye mgomo kutokana na mkutano wa maridhiano uliofanyika jana (juzi) baina yao na Waziri Mkuu,” alisema Aliegaesha.
Msemaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Frank Matua, naye alisema huduma katika taasisi hiyo zimerejea katika hali ya kawaida kwa vitengo vyote, zikiwamo za  kliniki.
“Huduma zinapatikana sasa. Kliniki zote zilizofungwa wakati wa mgomo sasa zimefunguliwa. Changamoto ni kwamba idadi ya wagonjwa waliofika leo (jana) kupata huduma ni bado ndogo,” alisema Matua na kuongeza;
“Hili linaweza kuwa limesababishwa na wao kutokuwa na taarifa za uhakika kuhusu kumalizika kwa mgomo huo.”
Awali madaktari hao waligoma wakidai kupatiwa nyumba za kuishi, kukopeshwa magari, kupatiwa bima ya matibabu, kulipwa fedha kwa ajili ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi na magumu na kuboreshewa mazingira ya kazi hospitalini, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa dawa na vifaa vingine muhimu.

Huduma mikoani
Mbali ya Muhimbili na MOI , huduma hizo pia  zimeanza kurejea katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Mbeya na Hospitali ya Bugando mkoani Mwanza.
Madaktari katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma walitangaza juzi jioni kuwa wamesitisha mgomo na sasa wanarejea kazini kama kawaida.
Katibu wa Afya wa Hospitali hiyo, Isack Kaneno alithibitisha kupewa taarifa ya madaktari kusitisha mgomo na kueleza kuwa huduma sasa zitaendelea kama kawaida.
Katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, hali imetengemaa baada ya madaktari waliokuwa wamegoma kurudi kazini jana.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Bugando, Dk Charles Majinge, alisema mwitikio wa madaktari kurudi kazini ni mzuri ingawa bado utawala wa hospitali hiyo hadi jana mchana ulikuwa unafanya tathmini ya idadi ya waliorejea.


Ombi kwa Rais Kikwete
Katika hatua nyingine, baadhi ya madaktari waliorejea kazini, wamemtaka Rais Kikwete awafukuze Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda na Naibu wake, Dk Lucy Nkya.

Dk Godfrey Kimaria, alisema kutokana na maelezo ya Waziri Mkuu, mawaziri hao hawana budi kufukuzwa kwa kuwa wamesababisha maafa.Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Edwin Chitage, alisema  kilichofanywa na madaktari ni mapinduzi makubwa kutokana na umoja waliouonyesha na Serikali inatakiwa kuisafisha wizara hiyo ili kuleta mwonekano sahihi wa kiutendaji.

Shinikizo zaidi kwa Mponda, Nkya
Siku moja baada ya Serikali kuwasimamisha kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali Dk Mtasiwa, wanaharakati nchini, wamemtaka Rais Jakaya Kikwete, kumng'oa  Waziri wa Afya na Naibu wake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wanaharakati wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Jukwaa la Katiba na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta), walisema, Dk Mponda na Dk Nkya wanapaswa kuwajibika kwa madhara yaliyotokana na mgomo huo.

Mkurugenzi wa LHRC, Helen Kijo Bisimba alisisitiza kuwa ni lazima Rais Kikwete awawajibishe mawaziri hao kama watashindwa kujiuzulu kwenye nafasi zao.

 “Nawaomba viongozi hawa wajiuzulu haraka ili uchunguzi uweze kufanyika. Wasimsubiri Rais awawajibishe, waonyeshe uzalendo wao kwa Watanzania wa kufanya uamuzi bila kushurutishwa,” alisema.

Bisimba aliupongeza uamuzi wa madaktari kurejea kazini akisema ni uamuzi wa kiungwana uliolenga kuokoa maisha ya Watanzania lakini Serikali nayo itimize ahadi zake kwao, alisema

Rais wa CWT, Gratian Mukoba naye alisema chama hicho kingependa kuona Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii na Naibu wake,wanajiuzulu kwa kuwa wamesababisha maafa makubwa Muhimbili.

Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Rodrick Kabangira alisema wameamua kurudi kazini kuitikia wito wa makundi mbalimbali ya kijamii. Aliongeza kuwa itakapofika Machi 3, mwaka huu, watakaa na kamati yao kutathmini matokeo ya mazungumzo yao na Serikali.


Viongozi wa  Dini
Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhaji Musa Salum amesema Serikali inapaswa kupongezwa kwa hatua iliyofikia ya kuwarudisha madaktari kazini.

Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Kagera, Dk Methodius Kilaini, amelaani kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata wanaharakati wa haki za binadamu huku akiitaka Serikali kuwasikiliza kwani wanatetea haki za Watanzania.


Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi jana Askofu Kilaini alisema polisi haikupaswa kuwakamata wanaharakati hao kwani wapo kwa lengo la kutetea haki za Watanzania.

Mbunge wa Jimbo Ubungo John Mnyika amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaondoa Waziri Mponda na Naibu wake Dk Lucy Nkya haraka ili kupisha uchunguzi baada ya kuonyesha udhaifu wa kutatua mgogoro wa madaktari na Serikali.
Imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Hamisi Mwesi, Dodoma,  Keneth Goliama, Ray Naluyaga, Godfrey Kahango, Mbeya, Raymond Kaminyoge

No comments:

Post a Comment