NJOMBE

NJOMBE

Thursday, February 2, 2012

Posho zaota mbawa zaleta mzozo

IMEFAHAMIKA kuwa tabia ya Rais Jakaya Kikwete kushindwa kufanya uamuzi kuhusu posho za wabunge ndiko kumesababisha mzozo uliopo kati ya Ikulu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda na uongozi wa Bunge.
Habari za kuaminika kutoka uongozi wa Bunge zinasema Spika Anne Makinda asingeweza kuruhusu posho mpya bila kukubaliwa na rais.
Kwa mujibu wa kiongozi mmoja mwandamizi wa Bunge aliyezungumza jana kwa sharti la kutotajwa jina, amesema Rais Kikwete alipopelekewa mapendekezo hayo, hakukataa bali alitoa maelekezo yaliyoashiria kukubali.
Hata hivyo, sasa imegundulika kwamba maelekezo ya rais yalikuwa tata, na yamegeuka mtego kwa uongozi wa Bunge.
“Kwa kawaida, rais anapoletewa jambo la kusaini, kwa mfano muswada wa sheria au hili la posho mpya za wabunge, anapaswa kusema ndiyo au hapana. Lakini katika hili, rais amefanya ujanja, kwani badala ya kukubali au kukataa, yeye ameandika sentensi moja kwamba tutumie busara kutafakari na kuamua jambo hili katika mazingira ya sasa. Busara yetu sisi ni kuongeza kulingana na mazingira ya sasa,” alisema kiongozi huyo.
Sasa siku moja baada ya Ikulu kukanusha kauli ya Spika wa Bunge kwamba rais ndiye alibariki posho mpya za kikao za wabunge, chama chake CCM, ambacho kimekuwa kinatetea posho hizo, sasa kimewataka wabunge wake kuachana nazo.
Kwa maana hiyo, posho mpya za vikao kwa wabunge, zilizotarajiwa kupanda kutoka sh 70,000 hadi sh 200,000, zimeota mbawa.
Na baadhi ya wabunge wamesema msimamo wa Ikulu unawagawa wabunge wa CCM, huku ukiwapa ushujaa wale waliokuwa wakizipinga tangu awali; lakini pia unaonyesha udhaifu wa uongozi kwa upande wa rais.
Kauli hiyo inakwenda sambamba na ya baadhi ya wasomi na wananchi wengine waliosema suala hili limethibitisha tena kwamba nchi inakabiliwa na ombwe la uongozi, ambalo sasa linatishia uhusiano kati ya mihimili miwili ya dola – Bunge na Serikali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Uongozi, Hebron Mwakagenda, alisema kiongozi imara ni yule anayekuwa na msimamo katika kauli na uamuzi.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema kauli zinazopingana za JK, Pinda na Makinda, zimemshangaza. Hakutaka kufafanua zaidi.
Katika kikao kilichofanyika mwanzoni mwa wiki mkoani Dodoma, baadhi ya wabunge wa CCM waliwasulubu wenzao kwa kupinga nyongeza ya posho hizo.
Miongoni mwa walionyooshewa kidole ni Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, ambaye aliambiwa anazikataa kwakuwa anatumia gari la CCM, ndiyo maana haoni ugumu wa maisha.
Mbunge mwingine wa CCM aliyewekwa kikaangoni ni Dk. Hamis Kigwangalah, ambaye ilidaiwa amekuwa akizipinga kwa lengo la kujitafutia umaarufu.
Katika kikao hicho, Makinda aliwaambia wabunge wanaopinga nyongeza hiyo wanajitafutia umaarufu kupitia posho hizo, badala ya kuutafuta katika kutatua kero za wananchi.
CCM yazipinga
Taarifa iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, iliwataka wabunge walitafakari suala hilo na ikiwezekana watumie busara kuachana nalo kwa sasa.
Nape aliwataka wabunge kufungua masikio na kusikiliza sauti za Watanzania ambao wamekuwa wakilalamikia nyongeza ya posho hizo ambazo katika siku za hivi karibuni zimezusha zogo kubwa.
“Wabunge wakiwa huko bungeni wana wawakilisha hawa Watanzania. Ni vizuri kusikiliza hiki kilio chao, si busara kupuuza kilio cha waliokupa dhamana ya kuwawakilisha. Tunawasihi waheshimiwa wabunge wetu nao walitafakari hili na kuona busara ya kuachana nalo kwa sasa,” alisema.
Mzozo wa posho mpya juzi uliingia katika hatua mpya baada ya Rais Kikwete kukana kubariki posho hizo, huku Spika akisisitiza kwamba Rais Kikwete ndiye alibariki posho hizo.
Kauli ya Makinda ilishabihiana na ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyewaeleza wahariri wiki iliyopita kwamba Rais Kikwete amelirejesha faili la suala hilo mezani kwake kwa ajili ya uamuzi; na baadaye alinukuliwa akisema lugha ile ile ya Makinda.

No comments:

Post a Comment