NJOMBE

NJOMBE

Friday, February 3, 2012

Dk. Bilal kuzindua kambi ya vijana

MAKAMU wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal, leo anatarajia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kambi ya maarifa ya vijana, itakayofanyika katika kijiji cha Msoga, wilayani Bagamoyo, Pwani.
Akizungumza kuhusiana na maandalizi ya kambi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, alisema kuwa itajumuisha jumla ya vijana 400 kutoka wilaya za Mkuranga, Rufiji, Kibaha, Bagamoyo, Mkuranga na Kisarawe.
Mwantumu alifafanua kuwa vijana hao 400 pindi watakapokuwa katika kambi hiyo, watajifunza mambo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa nyumba bora kwa gharama nafuu.
“Kwa kweli kwa upande wangu ninashukuru kuwa maandalizi yote kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa kambi ya maarifa ya vijana wa mkoa wa Pwani yanakwenda vizuri,” alisema Mwantumu.
Alisema kuwa kambi hiyo itafanyika katika shule ya msingi ya zamani ya Msoga na kwamba vijana watakaoshiriki ni wenye umri wa kuanzia mika 18 hadi 25.
Pia alisema kwamba vijana hao pindi watakapokuwa kambini watajenga nyumba tano za mfano pamoja na mashine ambazo alibainisha kuwa zitaweza kuwa mkombozi kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa mkoa wa Pwani.
Mwantumu alifafanua kuwa vijana watakuwa kambini hapo kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi Februari 29 ambapo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, atafunga mafunzo hayo.

No comments:

Post a Comment