NJOMBE

NJOMBE

Saturday, February 4, 2012

CHADEMA yapewa barua ya karipio

TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kupitia kwa kwa ofisi ya uchaguzi wilaya ya Kati, imekiaandikia barua ya karipio Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kitendo chake cha kufanya mkutano wa hadhara katika maeneo ya Shehia ya Tunduni, ikidai ni kinyume na kifungu cha 34 cha kanuni za uchaguzi za mwaka 2010.
Katika barua hiyo ZEC ilisema kuwa CHADEMA ilifanya mkutano huo uliohudhuriwa na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, Januari 27 mwaka huu saa 10 jioni katika eneo ambalo si ofisi ya chama hicho ambapo kwa mujibu wa mwenendo mzima wa uchaguzi, mkutano huo umetambulika kama ni kampeni.
“Kumbuka kwamba kwa mujibu wa ratiba ya tume ambayo umepatiwa kipindi cha kampeni ni Januari 28 hadi Februari 11 mwaka huu, hivyo basi mkutano huo ni haramu na ni kinyume na maadili ya uchaguzi tuliyokubaliana,” ilisema sehemu barua hiyo.
Hata hivyo, CHADEMA kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Hamad Musa Yussuf, ilijibu karipio hilo ikisema kuwa inasikitishwa na barua hiyo kwani kwa mujibu wa maadili ya uchaguzi, chama na mgombea, wakifanya kitu ambacho ni kinyume na maadili, watatakiwa kufunguliwa malalamiko kwa msimamizi wa uchaguzi.
Alisema baada ya msimamizi wa uchaguzi kupata malalamiko hayo, atamwandikia mlalamikiwa, akimfahamisha juu ya tuhuma zinazomkabili na kuambatanisha na tuhuma husika na kisha mtuhumiwa atatakiwa kujibu tuhuma hizo na kuwasilisha kwa msimamizi.
“Huu ndio mchakato wa kushughulikia malalamiko uliowekwa na maadili ya Tume ya Uchaguzi ambayo unatakiwa kuyasimamia, kinachotushangaza na kufanya tuhoji ni uelewa wa ofisi yako.
“Barua yako haina ambatanisho la malalamiko uliyopokea na kukusukuma wewe kutoa karipio na wala hukuelekeza kama mlalamikaji ni wewe au ni nani, vitendo vya ofisi yako kujigeuza kuwa mlalamikaji, msikiliza malalamiko na hakimu bila kuhusisha vikao ni kinyume na tarartibu,” alisema Yussuf.
Katika hatua nyingine CHADEMA imetetea maamuzi yake ya kuamua kukodi nyumba nane katika jimbo la Uzini baada ya Chama cha Mapinduzi kuirushia vijembe kuhusu kitendo chake hicho.
Akizungumza katika mikutano miwili ya hadhara katika shehia ya Kiboje Mwembeshauri na Kiboje Mkwajuni, ofisa msaidizi wa kampeni, Benson Kigaila, alisema kukodi nyumba hizo huko ni kwamba fedha zote watakazotumia kila siku zitaenda kwa wananchi wa Uzini.
Naye mgombea wa chama hicho katika jimbo hilo, Ally Mbarouk Mshimba, alisema katika uzinduzi wa kampeni za CCM, Rais mstaafu, Aman Abeid Karume, aliwaambia wakazi wa Uzini wasimchague mtu mgeni jambo ambalo limewafagilia njia CHADEMA kwa kuwa Mohamed Raza, ndiye mgeni.

No comments:

Post a Comment