NJOMBE

NJOMBE

Monday, February 13, 2012

Hekima za Mbowe zaleta amani bungeni

KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe,Mbowe alitumia hekima kumaliza mvutano mkali wa hoja kati ya wabunge wa upinzani na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyowezesha kupitishwa kwa marekebisho ya mabadiliko ya katiba.
Mvutano huo wa hoja ulisababishwa na hatua ya wabunge wa CCM kupinga pendekezo la kuwataka wakurugenzi wa halmashauri ndiyo wawe wasimamizi wa mikutano ya Tume ya Katiba itakayokuwa ikiratibu maoni ya mabadiliko ya katiba.
Wabunge wa CCM ambao walionyesha wazi mwelekeo wa kuwa na ajenda moja walikuwa wakitaka wakuu wa wilaya ndiyo wawe na wajibu huo badala ya wakurugenzi wa halmashauri.
Msimamo huo wa wabunge wa CCM ulikuwa ikipingwa vikali na wabunge wa CHADEMA ambao kwa maoni yao waliiona hoja hiyo ya kuwataka wakuu wa wilaya kuwa iliyokuwa ikilenga kukinufaisha chama hicho tawala.
Akizungumza kabla ya Mbowe kusimama na kutuliza mambo, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), aliita hatua hiyo ya wabunge wa CCM kuwa inayoibua mkanganyiko.
Lissu katika hoja yake alisema wakurugenzi wa halmashauri walikuwa ni watu wenye uwezo na waliokuwa wanafaa kutumiwa na Tume ya Katiba badala ya wakuu wakuu wa wilaya ambao kupiganiwa kwao kunalenga kulinda maslahi ya CCM.
Mvutano kuhusu hoja hiyo iliyokuwa ikigusa kifungu cha 17 cha marekebisho hayo ya sheria, ulianza juzi hatua ambayo ilisababisha Spika wa Bunge, Anne Makinda, kulipeleka suala hilo kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria na Katiba kabla ya kurejea na mapendekezo mapya jana.
Hoja hiyo iliporudishwa tena bungeni jana ilikuja na mapendekezo ya kuwajumuisha wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kwa pamoja katika kazi ya kuratibu kazi za tume ya katiba.
Kabla ya suala hilo kupelekwa katika Kamati ya Katiba, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Fredrick Werema, alisema ili kila upande uonekane mshindi katika suala hilo, kifungu hicho kinapaswa kuwaruhusu wakuu wa wilaya na wakurugenzi kutumiwa na Tume ya Katiba, kuitisha mikutano ya maoni.
Akisoma maafikiano ya kamati na pande husika jana, makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Angela Kairuki (CCM), alisema wamekubaliana na marekebisho yaliyopendekezwa na AG, ya kuwekwa kwa mkuu wa wilaya na mkurugenzi wa halmashauri.
Hata baada ya maoni hayo ya kamati, mvutano kati ya wabunge wa CCM na wale wa upinzani uliendelea kuwa mkali hadi pale, Mbowe aliposimama na kutoa kauli ambayo iliwatuliza wabunge anaowaongoza.
“Wakurugenzi wa halmashauri ni watendaji wa serikali ya CCM, wanaosimamia shughuli za maendeleo ya wananchi…inasikitisha kuona kwamba wabunge wa CCM hawawaamini watumishi hawa wa serikali,” alisema Mbowe na kuongeza: “Wabunge wa upinzani tunalazimika kuweka rekodi kukubali marekebisho ya Mwanasheria Mkuu yapite…lakini utamaduni huu tunaojenga humu ndani, wa kufunika kombe mwanaharamu apite utatugharimu baadaye.
“Wabunge wenzangu wa upinzani tukubali jambo hili limalizike kwa sababu lazima tufike sehemu tu-compromise (turidhie), twende tukatunge katiba ambayo itadumu zaidi ya miaka 100 bila kujali kuwapo kwa CCM au CHADEMA,” alisema Mbowe.
Baada ya Mbowe kumaliza, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uratibu na Uhusiano), Steven Wassira, alisimama na kumpongeza kwa kutumia hekima na busara kuwashawishi wenzake.

No comments:

Post a Comment