NJOMBE

NJOMBE

Friday, February 17, 2012

Kamati kujadili fedha zilizoibiwa UVCCM

KAMATI ya Siasa ya Wilaya ya Simanjiro kesho inatarajia kukutana na kumjadili aliyekuwa Katibu wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Alhaj Omar Kariaki anayedaiwa kutokomea na fedha zilizochangwa kwenye harambee maalumu ya kutunisha mfuko wa maendeleo ya vijana wilayani humo.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Kiria Laizer ikiwa ni siku moja baada ya Kariaki kuibuka na kukiri kutokabidhi fedha hizo.

Laizer alithibitisha jana kufanyika kwa kikao hicho alichosema pia kitahudhuriwa na mkuu wa wilaya hiyo, Khalid Mandya ambaye amevalia njuga upatikanaji wa fedha hizo zilizopatikana kwenye harambee iliyoongozwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Shamsi Vuai Nahodha.

Nahodha ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani katika Serikali ya Muungano, binafsi alichangia Sh2 milioni katika harambee hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa hoteli ya kitalii ya Manyara Inn ulioko mji mdogo wa Mererani wilayani Simanjiro.

“Kwanza nachukua fursa hii kukupongeza wewe binafsi na gazeti lako la Mwananchi kwa jinsi mlivyofuatilia kwa karibu suala hili hadi mtuhumiwa ambaye tumemtafuta kwa kipindi kirefu kujitokeza hadharani na kukiri kuondoka na fedha zetu. Jumamosi tunakutana kwenye kamati ya siasa wilaya kujadili hili,” alisema Laizer.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Simanjiro jana asubuhi, Mwenyekiti huyo wa vijana alisema kila siku anamwomba Mungu suala hilo lipate ufumbuzi kwani licha ya kuwapa picha mbaya mbele ya waliojitolea kuchanga fedha zao kuinua hali ya maisha ya vijana kwa kuanzisha mradi wa mahari ya kusafirisha abiria, yeye binafsi amekuwa akihusishwa na upotevu wa fedha hizo.
Habari zaidi katika Mwananchi.

No comments:

Post a Comment