NJOMBE

NJOMBE

Friday, February 3, 2012

Pinda: Tumeshindwa,Serikali yakiri maisha bora yameota mbawa

NDOTO na ahadi za maisha bora kwa kila Mtanzania za serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) zimeyeyuka. Sasa serikali imekiri kushindwa kudhibiti mfumko wa bei unaopandisha gharama za maisha na kuongeza ukali wa maisha ya Watanzania.
Na badala ya serikali kutoa majibu au kuonyesha mikakati ya kuwakwamua Watanzania, Waziri Mkuu Mizengo Pinda jana aliliambia Bunge kwamba taifa linakabiriwa na mtikisiko wa kiuchumi na kwamba mkakati wa kwanza wa kujinasua ni wananchi kutambua mtikisiko huo na kujikwamua.
Aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii ili kuzalisha bidhaa za kutosha, kujitosheleza kwa chakula na mikakati mingine mingi.
Pinda alitoa kauli hiyo wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo (CCM), aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kuwasaidia wananchi kuondokana na hali ngumu ya maisha iliyosababishwa na uchumi kuharibika.
Kwa mujibu wa maelezo ya Pinda, hali hiyo imetokana na kupanda kwa gharama za mafuta katika soko la dunia pamoja na mtikisiko wa uchumi wa mataifa makubwa duniani.
Ingawa alisema serikali imeweka mkakati wa kuwakwamua wananchi kutokana na hali hiyo ngumu ya maisha, Pinda hakusema serikali inafanya nini, bali aliishia kuwataka wananchi wenyewe kuitambua hali ngumu ya uchumi iliyopo sasa.
Kauli ya Pinda inakwenda kinyume cha tambo na ahadi za serikali ambayo imekuwa ikijinadi kwa wananchi kuwa itawaletea maisha bora, kama ambavyo Chama cha Mapinduzi (CCM) kiliahidi wakati wa kampeni mwaka 2005 na 2010.
Wakati Pinda akikiri kushindwa kwa serikali na kuwatwisha wananchi mzigo wa kujitambua na kujikomboa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (Tamisemi), George Mkuchika, naye alikiri kuwa serikali ina upungufu mkubwa wa fedha za ruzuku kwa halmashauri.
Kutokana na upungufu huo, alisema, serikali imeshindwa kupeleka fedha za ruzuku ya miradi ya maendeleo kwa kila halmashauri nchini kwa miaka miwili sasa.
Mkuchika alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Singida Magharibi, Mohamed Misanga, aliyeeleza kutoridhishwa na swali lake la msingi la miradi ya maji aliyoahidiwa tangu wakati wa Waziri wa Maji na baadaye Waziri Mkuu, Edward Lowassa, kwamba serikali itapeleka fedha kukamilisha miradi hiyo.
Kutokana na jibu hilo, Misanga alisema jibu hilo ni kiini macho kwani kwa sasa halmashauri zote zina ukata kutokana na serikali kushindwa kupeleka fedha za ruzuku za kila mwezi katika halmashauri hizo na kukwamisha miradi mingi ya maendeleo.
Akijibu swali hilo, Waziri Mkuchika alikiri kwamba hali ya kifedha katika halmashauri zote nchini ni mbaya.
“Ni kweli Mheshimiwa Spika, serikali haijapeleka fedha za ruzuku na miradi mingine katika halmashauri zote za wilaya nchini kwa takriban miaka miwili kutokana na upungufu wa fedha,” alisema Mkuchika.
Waziri huyo alisema halmashauri zote za wilaya zina matatizo ya kifedha na hata vikao vya kisheria havifanyiki tena na badala yake maamuzi yanafanywa na watendaji wenyewe.
Kutokana na hali hiyo, Mkuchika alisema halmashauri zote zimeagizwa kukusanya fedha zake za ndani kwa ajili ya kuendesha shughuli zake hasa zile zilizokuwa zikiendeshwa kwa fedha za ruzuku.
“Halmashauri zimeagizwa kukusanya pesa za ndani, lakini hazitoshi kwani kodi nyingi hasa zile za manyanyaso zilifutwa. Kwa hiyo hawana vyanzo vya kutosha vya kukusanya fedha,” alisisitiza.
Hata kabla ya agizo hilo la Mkuchika, tayari halmashauri kadhaa nchini zimeanza kuwalazimisha wananchi kuchangia elimu katika maeneo yao, huku zikitumia nguvu wakuu wa wilaya kutisha wananchi hao.
Tayari wananchi katika wilaya kadhaa wameanza kulalamikia hatua hiyo ya serikali, huku baadhi ya watendaji wakisema mabavu hayo ya serikali yataongeza chuki na hasira kwa wananchi dhidi ya serikali na CCM.
Katika wilaya ya Muleba, mkoani Kagera, wananchi wamekuwa wakisema mkuu wa wilaya anawalazimisha kuchangia elimu; watachanga kwa hasira na baadaye watafanya uamuzi wa hasira wakati utakapofika.
Ili kukabiliana na hali hiyo, Waziri Mkuchika alisema wizara yake imeandaa mkutano na Waziri Mkuu pamoja na Wizara ya Fedha na Uchumi ili kuangalia namna ya kukabiliana na hali hiyo ya ukata.

No comments:

Post a Comment