NJOMBE

NJOMBE

Sunday, March 18, 2012

NAMNA YA KUTOKA KWENYE UTUMWA WA NDOA…….

Sio lengo langu kuwafundisha wanawake namna yakuachana na wapenzi au waume zao. Lakini hebu fikiria kwamba kila wakati wanandoa au wapenzi wako kwenye vita. Hakuna amani, hakuna masikilizano. Kutwa nzima mtu anawaza kuhusu uhusiano wake mbaya hadi anashindwa hata kufanya kazi. Je, hali kama hii ina maana kwa mtu kuendelea kuwa kwenye ndoa?




Hapa nazungumzia wale ambao wanashindwa kutoka kwenye uhusiano, ambao wanajua kabisa kwamba, unawatesa na kuwaumiza. Kuna sababu nyingi kwa nini watu hawa wanashindwa, lakini nyingine zinatokana tu na kutojua namna ya kutoka, sio utegemezi wa aina yoyote.


Moja ya sababu, ambazo ninaziona sana hasa kwa wanawake ni kujali jamii itasemaje. Mtu anaona kabisa uhusiano haufai na anatamani kutoka . lakini anajiuliza, hivi watasemaje? Kuna wakati ndugu wanamwambia, yeye ndiye mkorofi. Kama hii ndio sababu anachotakiwa kufanya mwanandoa ni kuhakikisha kwamba anajifunza kuishi kama yeye. Nijuavyo mimi, hata wanandugu au jamii hata ikisema vipi, anayeumia au kuepuka kuumia au kuuawa ni yule aliye kwenye mateso ya ndoa

Jambo la kujiliza hapa ni kama, jamii ndiyo inayopigwa, kutukanwa, kutelekezwa au kudhalilishwa? Lakini jambo kubwa zaidi la kufahamu ni kwamba mtu alishaolewa maana yake ni mtu mzima mwenye haki ya kuamua juu ya maisha yake. Akisbiri ndugu wamwamulie, basi huyo bado ni mtoto..


Jambo lingine ni lile la, je nikimwacha nitapata mwingine? kwani wanaume siku hizi ni shida sana? Ni ujinga unaowafanya wengi kuuliza swali hilo. Unahitaji mwingine wa nini? Unahitaji mwingine ili maisha yako yawe ya maana zaidi au? Kama hakuna mwingine ni vyema kwa sababu maana yake ni kwamba hakuna mwingine wa kukutesa. Lakini wanasaikolojia wanaamini kwamba, ‘kila bidhaa ina mnunuzi.’ Kama unataka mwingine, hata ukiwa na miaka sitini utampata. Huwezi kumpata wakati ukiwa ndani ya tanuru la mateso. Ni lazima utoke kwanza.


Kuna wale wanaoshindwa kutoka kwa sababu wanaamini kwamba mwanamke haruhusiwi kutoa talaka. Hi siyo kweli. Kuna wanaoshindwa kutoka kwa sababu dini zao zinakataza kuachana, hii pia siyo kweli. Mwanamke au mwanaume, yeyote anaweza kuomba talaka na ikatolewa, kama kuna sababu zenye kukidhi haja hiyo. Chombo pekee kinachoweza kutoa talaka au kuidhinisha wanandoa kuachana ni Mahakama, siyo dini au taasisi nyingine. Kinachoitwa ‘talaka tatu’ kwa mfano, ni ushahidi tu, na sio talaka.


Kuna wale ambao hawako tayari kutoka kwenye uhusiano mgumu kwa sababu ya mali. Wanaogopa watagawana mali na wenzao, jambo ambalo hawako tayari kulifanya na mara nyingi hawa ni wanaume. Wapo pia wanawake ambao wao ndio waliokuwa watafutaji wakuu. Swali la kujiuliza ni hili. ‘Ni kipi bora, ni mali au ni amani na utulivu na uhai wako?’ kama ni mali, basi hakuna anayeweza kukuingilia kwenye uamuzi wako.


Lakini, kwa ufahamu tu, ni kwamba, pasipo na amani, mali haina maana na pasipo na amani uhai ni wa kubahatisha pia.

Wengine wanashindwa kutoka kwenye husiano kwa sababu wazazi wa mume na ndugu wanampenda sana. Anaogopa kuwaudhi kwa kuondoka kwenye ndoa ya mateso ya mtoto wao na ndugu yao. Anataka wafurahi, hivyo hawezi kuondoka. Huu nao ni upungufu.

Hivi unakuwa umeolewa na ndugu na wazazi au na mume? Lakini, kwani ukiondoka utashindwa kuwa karibu na watu hawa? Hutashindwa na pengine urafiki wenu utakuwa wa kudumu. Ukiendelea kukaa kwenye ndoa ya mateso kuna siku utakosana hata na hawa, maana unaweza ukalipukwa ukamuuwa mtoto au ndugu yao.


Kuna wale wanaoshindwa kutoka kwenye uhusiano mgumu kwa sababu wana watoto na wanaogopa kwamba, watoto wao watateseka. Hivi ni kuteseka kupi kubaya, kule kwa utotoni au ukubwani? Mtoto anayeishi kwenye ndoa yenye vurugu, anaharibikiwa kuanzia utotoni hadi ukubwani. Lakini, hata hivyo kuachana kwa wazazi, sio lazima kuwe na maana ya watoto kuteseka.


Kuna wakati hata watoto wanamwambia mama atoke kwenye ndoa, halafu mama huyo huyo anadai anakaa kwenye ndoa hiyo kwa sababu ya watoto! Kuna haja ya kujiuliza maswali kwa upana zaidi.


Ukitaka kutoka kwenye ndoa ngumu jiulize maswali haya. Je, ndoa hii ni kwa faida ya nani? Je, niliolewa au kuoa ili kupata shida au amani na upendo? Je, bila ndoa,nisingeweza kuishi mwenyewe? Tafuta mifano ya wasio na ndoa ambao wanafurahia maisha.


Jiulize ni kwa kiasi gani wengine wanasaidia kukusukuma zaidi kwenye ndoa hiyo? Jiulize ukamilifu wako. Je, wewe ni nusu mtu au mtu kamili? Kama ni mtu kamili , basi ishi kama mtu kamili.

No comments:

Post a Comment