NJOMBE

NJOMBE

clock

Friday, March 9, 2012

Mgomo madaktari wafuta ziara ya Pinda Mwanza

MGOMO wa Madaktari umeshika kasi kiasi cha kusababisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kufuta ziara yake ya siku kumi iliyokuwa ikitarajiwa kuanza mkoani Mwanza leo, huku huduma za afya katika baadhi ya hosipitali nchini zikiathirika kwa kiasi kikubwa.

Ziara hiyo ambayo ilipaswa kuanza leo Machi 9, mehairishwa hadi hapo itakapopangwa baadaye huku taarifa za ndani zikieleza kuwa kuhairishwa huko kunatokana na Waziri Mkuu huyo kuwa katika majukumu ya kushughulikia kutatua mgomo wa madaktari ambao ulianza juzi.  Mgomo wa madaktari umeshika kasi na kuathiri huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (MOI) ambayo jana ilitangaza kusitishwa kwa huduma za klinini kwa wagonjwa wa nje (OPD).

Msemaji wa Taaisi hiyo, Juma Almasi alisema jana kwamba hatua hiyo imelenga kuwawezesha madaktari wachache waliopo kuhudumia wagonjwa 237 waliolazwa wodini.

“Taasisi ina wagonjwa 237 waliolazwa wodini na madaktari wanaoendela kufanya kazi ni wakuu wa idara na wenye nafasi za uongozi ambao idadi yao haizidi 15”alisema Almas.

Alifafanua kuwa katika siku za kawaida huduma za Kliniki kwa wagonjwa wa nje hutolewa na zaidi ya Madaktari 20 huku idadi ya wagonjwa ikitofautiana kutokanana na aina ya kliniki zilizopangwa kwa siku husika.

“MOI inamadaktari zaidi ya 70 na kila siku huduma za Kliniki za nje hutolewa na Madaktari zadi ya 20,kutokana na mgomo huu tumeamua kusitisha huduma za wagonjwa nje wanaokuja kwa ajili ya Kiliniki na kwamba tutaendelea kuwahudumia walioko wodini”.

Pia msemaji huyo alisema huduma nyingine zitakazopatikana katika Taasisi hiyo ni katika kitengo cha dharura.

Wagonjwa walalama
Wagonjwa wote waliofika MOI jana kupata huduma za vipimo mbalimbali katika Kliniki waliamriwa kurejea  nyumbani kwao hadi watakapopata taarifa za kumalizika kwa mgomo huo kupitia vyombo vya habari.

Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wagonjwa na wauguzi waliitupia lawama serikali kwa kushindwa kutatua tatizo hilo ambalo walidai dalili zake zilionekana tangu mwanzo.

Mmoja wa wagonjwa hao, Kulwa Amiri (30) Mkazi wa Dar es Salaa alimtaka  Rais Jakaya Kikwete,Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mawaziri wanaokataliwa na madaktari kutafakari na kuchukua hatua zaidi ili kunusuru maisha ya wagonjwa.

“Katika mgomo wanaoathirika ni wengi siyo tu mgonjwa,wapo waangalizi wa wagonjwa nao wanapoteza muda kwa kumsindikiza mgonjwa,nauli na pia hata kazi wanazozifanya zinasimama”alisema Amiri na kuhoji:

“Hivi ni kweli serikali haioni mateso tunayopata?,inashindwa nini kuwawajibishwa hao mawaziri  hao, hata kutaka kututoa sisi kafara?mbona Mh Edward Lowasa alipokuwa waziri Mkuu alijiuzulu, tunaomba watafakari kwa makini kwani tunaoteseka ni sisi”alisema Amiri ambaye alivunjika  uti wa mgongo.

Wakati mgonjwa huyo akilalamikia kitendo hicho,baadhi ya ndugu wa wagonjwa wengine waliokuwa wamelazwa Wodini walifika hosptalini hapo na kuanza kuahamisha wagionjwa wao.

Marwa Chacha na ndugu zake walimhamisha, Edina Kimeta aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Mwaisela huku akieleza kufikia uamuzi huo kuwa imetokana na hali ya kutisha na isiyotabirika iliyopo katika eneo hilo.

“Tumeamua kumchukua bibi yetu Edina na kumhamishia katika hosptali ya binafsi ya Regency sababu tumeona hali katika eneo hili inatisha,kwanza mambo yanaingiliana wapo wanaofahamu na wengine hawafahamu”alisema Marwa.

Bugando nako moto
Madaktari katika hospitali ya rufaa ya Bugando jana waliingia siku ya pili katika mgomo wao na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa waliofika kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu.  “Leo tuliitwa kwenye kikao na Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, lakini tulikubaliana tusifike kwenye kikao hicho hivyo hatutakwenda,” alieleza mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka kuandikwa gazetini kwa kile alichoeleza kuwa sasa sio wakati wa kuandikana majina kwenye vyombo vya habari.  Huduma katika hiospitali hiyo jana zilianza kuzorota kwani licha ya baadhi ya madaktari kutogoma hali ilikuwa ikionyesha kuzidiwa kwa madaktari waliokuwa wakiendelea na kazi.

 “Unajua hapa kuna madaktari wa aina mbili wapo wale wa kanisa na wale wa wizara. Sasa hawa wa kanisa wanaendelea na kazi, lakini kwa vile wale wa wizara ni wengi, imekuwa vigumu kuendana na mahitaji,” alifafanua mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo.  Hata hivyo uongozi wa hospitali hiyo haukupatikana jana kuzungumzia suala hilo baada wengi wao, akiwamo mkurugenzi, Dk Charles Majinge kuwa kikaoni.
Tamko la Tughe
Ikiwa ni siku ya pili tangu mgomo kuanza Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (Tughe) kimetoa tamko la kuzitaka pande mbili zinazolumbana kutumia busara kumaliza mgomo huo.

Katibu Mkuu wa Tughe , Ali Kiwenge alisema jana Dar es Salaam kwamba mgomo huo ni matokeo ya pande hizo mbili kutegemeana na kutoaminiana katika kufikia mwafaka juu ya suala hilo.

“Sisi tunasema Serikali na Madaktari, hayo yanayoendelea wananchi wanawashangaa, tunasema hivyo sababu wanajua madai ya Madaktari Serikali iliyapokea na kuahidi kuyafanyia kazi, na ndiyo sababu Waziri Mkuu Pinda aliunda tume, lakini nao madaktari wakakubali kutoa nafasi ili madai hayo yafanyiwe kazi”alisema Kiwenge.

Alisema kufuatua hatua hiyo Tughe wanasisitiza kuwa suluhu lazima ifikiwe kupitia kwenye vikao na kuonya kila upande kutumia busara kunusuru maisha ya Watanzania.

Kiwenge  aliitaka serikali kufanya kazi kama chombo cha umma ikiwa ni pamoja na kushughulikia masuala mbalimbali kwa kufuata sheria,taratibu na kananuni zilizopo.

Alisema ni jambo la kawaida kwa serikali nyingi hususani za kiafirika na Tanzania ikiwamo kufanya kazi kinyume na taratibu jambo ambalo husababisha manungĂșniko, mgogoro, migomo baridi na baadaye migomo kamili na maandamano.

Pinda afuta ziara
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameahirisha ziara ya siku kumi mkoani Mwanza kutokana na mgomo wa madaktari, imethibitishwa.  Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evalist Ndiliko ingawa hakueleza wazi iwapo ziara hiyo imehairishwa kutokana na mgomo wa Madaktari, alidai kuwa ziara hiyo imesogezwa mbele kutokana na waziri mkuu kuwa na majukumu mengine ya kitaifa ambayo anapaswa kuyashughulikia.  “Ni kweli ziara hii imesogezwa mbele kutokana na Mheshimiwa waziri mkuu kuwa na majukumu mengine, kwa sasa tunangoja taarifa itaanza lini,” alisema Ndikilo jana.

 Hata hivyo, Mwandishi Msaidizi wa waziri Mkuu, Irene Bwire alithibitisha kuahirishwa kwa ziara hiyo kutokana na mgomo huo wa madaktari na kueleza kuwa ziara hiyo itafanywa hapo baadae.  “Ni kweli tumeelezwa kuwa ziara imeahirishwa kwa ajili hiyo na tumetangaziwa kuwa ziara hiyo itafanywa wakati mwingine” alisema Bwire.

 Katika ziara hiyo Waziri Mkuu alitarajiwa kutembelea wilaya zote nane za mkoa wa Mwanza ambazo ni Ilemela, Nyamagana, Magu, Kwimba, Misungwi, Ukerewe, Geita na Sengerema ambako angekagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuzungumza na viongozi wa Halmashauri hizo.  Ziara hii ilikuwa ni ya pili kwa Waziri Mkuu tokea alipoteuliwa kushika wadhifa huo, ambapo ziara ya kwanza alifika Jijini mwanza wakati wa maadhimisho ya miaka 40 ya Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Madaktari juzi walitoa tamko linaloeleza msimao wao wa kuendelea na mgomo usiokoma nchi nzima.
Habari na Mwananchi

No comments:

Post a Comment