NJOMBE

NJOMBE

Monday, January 30, 2012

Zitto: Futeni posho tuboreshe maslahi ya watumi

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), amesema serikali inapaswa kufuta kabisa mfumo wa posho za vikao katika stahili za viongozi na badala yake iboreshe maslahi ya watumishi wote kuepusha migomo kama inayoendelea sasa kwa madaktari.
Mbali na kutaka posho hizo ziondolewe, pia alisema kuna wabunge wanawapotosha wananchi kwa kuwaambia suala la posho ni suala lake binafsi kwa kile wanachoeleza kuwa ana vyanzo vingine vya mapato.
Zitto alitoa kauli hiyo jana katika Kanisa la Maisha ya Ushindi lililopo Ubungo External jijini Dar es Salaam, wakati akizindua albamu ya nyimbo za Injili ya msanii Miriam Ikombe.
“Tukizungumzia ugumu wa maisha wengine wanasema sisi wa upinzani tuna vyanzo vingine vya mapato, wanatutaka tusiseme ukweli juu ya maisha magumu yanayosababishwa na ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali ya nchi. Kwa hakika nchi imefika pabaya kwa kila anayesema ukweli kufikiriwa ana maslahi binafsi,” alisema Zitto.
Kuhusu mgomo wa madaktari, alitaka umalizwe kwa hekima na kueleza kuwa malipo duni kwa wafanyakazi wa umma ni matokeo ya uchumi kutozalisha mapato ya kutosha, hivyo kutaka uzalishaji uongezwe kwa kile alichosema bila uzalishaji hakuna kodi na mishahara itaendelea kuwa midogo.
“Hapa nataka viongozi wenzangu tuhamasishe watu kufanya kazi, tuonekane mashambani na viwandani na tuwe wakweli kwa wananchi, wabunge watumie muda wao kuzungumzia namna ya kukuza uchumi na kuleta ajira pia, kuwe na mkakati wa kweli wa kutokomeza ufisadi kwani nchi ni tajiri ila wananchi wake wanafanywa kuwa maskini kwa makusudi ya wachache,” alisema Zitto.
Alisema kwa jinsi gharama za maisha zinavyopanda kila kukicha huku wachache ndiyo wakifikiriwa kukabiliana na ongezeko hilo, ni wazi itakuwepo migomo isiyoisha katika jamii kwani hata kama madktari watatatuliwa matatizo yao leo, kuna uwezekano mkubwa sekta zingine zikaingia katika migomo.
“Tusishangae hata siku moja maaskari nao wakagoma kwa maana duka atakaloenda kupata mahitaji yake, mbunge anayelipwa laki mbili kwa siku ndilo hilohilo analotumia mfanyakazi anayelipwa chini ya laki moja na nusu kwa mwezi,“ alisema Zitto.

No comments:

Post a Comment