NJOMBE

NJOMBE

Monday, January 16, 2012

Kikwete kaungana na wananchi kuhani kwa akina Mtema

RAIS Jakaya Kikwete jana alikwenda nyumbani kwa familia ya marehemu Regia Mtema (32), Mbunge wa Viti Maalumu Chadema Tabata Chang’ombe jijini Dar es Salaam kuomboleza msiba wa Mbunge huyo.

Regia alifariki Jumamosi asubuhi katika eneo la Ruvu mkoani Pwani kwa ajali ya gari alilokuwa akiendesha akiwa na watu wengine saba akiwemo mama yake Bernadeta Mtema (45). Familia hiyo ilikuwa ikienda shambani Vigwaza.

Pamoja na Rais Kikwete pia, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifika nyumbani hapo kutoa pole kwa familia kwa msiba huo uliotokea kwa ajali ya gari katika eneo la Ruvu, mkoani Pwani.

Rais aliwasili nyumbani hapo kabla ya saa saba na baada ya kutoa pole kwa familia akiwemo
baba wa marehemu Estelatus Mtema, aliwapa pole baadhi ya viongozi wa Chadema waliokuwepo msibani hapo akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe.

Mara baada ya Rais Kikwete kuondoka, alifika Pinda nyumbani hapo ambapo aliwafariji
familia hiyo kwa msiba na baada ya kukaa kwa muda, naye aliondoka.

Akizungumzia msiba huo Spika wa Bunge, Anna Makinda alisema, “Nimepokea kwa huzuni msiba huu si kwa kuwa ni Mbunge bali kijana jasiri na mkakamavu, nimemfahamu Regia kabla hajawa Mbunge, wakati huo nikiwa Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wabunge, nilikuwa katika mikutano nahamasisha ile hamsini kwa hamsini bungeni.”

“Regia ni miongoni mwa vijana wa kike waliokuwa wabunge wakakamavu, nilimtia moyo na kumwambia natumaini kumuona bungeni na kweli alifanikiwa kuwa Mbunge, alikuwa makini katika kila alichoongea na alijituma, alijichanganya hata na Wabunge wa CCM, huu ni msiba wa Taifa,” alisema Makinda kwa huzuni.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (Chadema) alisema mbali na kuonesha kukubalika na kupata kura kwa asilimia 45 katika Jimbo alikowania, ndiye aliyeibua wazo la viongozi wa Chadema kukutana na Rais Kikwete kuzungumza naye kuhusu Muswada wa Mabadiliko ya Katiba.

“Nitaweka kwenye mtandao hili, najua watu wengi hawajui lakini ndiye aliyeibua wazo kwenye mkutano wa chama kuwa viongozi wakutane na Rais kuhusu Muswada wa Katiba, nasikitika kwa kuwa kuelekea kwenye mchakato wenyewe, tunamkosa mtu muhimu kama huyu,” alisema Zitto.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alisema msiba huo si wa familia na chama pekee bali ni wa Taifa hasa wapiga kura wa Jimbo la Kilombero alikowania Ubunge na kupata kura 38,550 sawa na zaidi ya asilimia 45 ya kura zote.

“Regia alikuwa mcheshi na jasiri, haogopi kusema ukweli hata kama utakuumiza, tulimuhitaji sana hasa wakati huu wa mabadiliko ya Katiba ya kitaifa, hatuwezi kumuhoji Mungu lakini ni masikitiko makubwa,” alisema.

No comments:

Post a Comment