NJOMBE

NJOMBE

Saturday, January 14, 2012

UWOYA NA NDOA YAKE ADAI AMEROGWA

Na Imelda Mtema
Beautiful mama wa Kiwanda cha Filamu Bongo, Irene Pancras Uwoya (pichani) amesema matatizo yaliyoikumba ndoa yake, yana mkono wa mtu.
Uwoya alimueleza ripota wetu mwanzoni mwa wiki hii kuwa anaamini kuna mtu amemroga ili amchukie mume wake, Hamad Ndikumana ‘Kataut’.
“Itakuwa nimerogwa, najishangaa sana. Kusema kweli nampenda sana mume wangu. Kinachotokea hata sijui ni kipi,” alisema Uwoya.
“Akiwa mbali namkumbuka, natamani awe karibu yangu. Akiwa karibu namchukia.”
Uwoya aliongeza: “Wewe unaonaje hali hiyo, siyo kurogwa? Kuna mtu ameniroga ili nikiwa karibu na mume wangu nimchukie, nisiwe na msisimko naye. Nimeambiwa anayenichezea ni msanii mwenzangu, tena naye ni maarufu Bongo, sijui kwa nini tunarogana?”
Kutokana na hali hiyo, Uwoya alisema kuwa ‘juju’ alilopigwa, litakwisha kwa maombi kwa vile amejipanga kumlilia Mungu.
“Naamini ndoa yangu itakuwa salama nikimshirikisha Mungu, nitaomba ili kama kuna mtu anaivuruga kwa nguvu za giza ashindwe,” alisema.
Mrembo huyo ambaye kwa sasa ni mama wa mtoto mmoja anayeitwa Krish, alisema Kataut ni mwanaume mzuri na anampenda sana ndiyo maana kila akikumbuka vitendo alivyomfanyia, anahisi kuumia.
“Ndoa yangu haitavunjika jumla, siwezi kuachana na mume wangu kwa sababu bado nampenda. Ninachotakiwa kufanya kwa sasa ni kumuomba Mungu ili kuyashinda majaribu ya Shetani yanayonikabili.
“Mungu atanisaidia kuondoa nguvu za giza zilizopo. Huyo aliyeniroga ili amani isiwepo kati yangu na mume wangu atashindwa na familia yangu itarudi kuwa imara,” alisema.
Wakati Uwoya anazungumzia maombi, ‘shosti’ wake, jina tunalo, alimueleza ripota wetu: “Irene (Uwoya) ameitwa Moshi. Anatakiwa akatakaswe na wazee kwa sababu mambo yanayotokea kwenye ndoa yake si ya kawaida.
“Tatizo lake la kumpenda mume wake akiwa mbali lakini wakiwa pamoja anamchukia, limeishangaza hata familia, kwa hiyo kuna mambo ya kimila anayotakiwa kufanyiwa.”
Uwoya ambaye ni Miss Tanzania namba tano mwaka 2006 na Kataut aliye mwanasoka wa kulipwa, raia wa Rwanda, walifunga ndoa ya kifahari jijini Dar es Salaam, Julai, 2009.
Pamoja na kuwepo kwa minong’ono kwamba Uwoya hakuwa mwaminifu kwenye ndoa yake, hususan pale mumewe alipokuwa kwenye majukumu yake ya kucheza soka nchini Cyprus, bado wanandoa hao walisisitiza kuwa wapo imara na wanapendana sana.
Mei, mwaka jana, Uwoya alijifungua na kwa kadiri mtoto anavyokua ndivyo na migogoro kwa wanandoa hao inavyoongezeka.
Hivi karibuni, yaliibuka madai kuwa hata mtoto huyo si wa Kataut, ingawa wanandoa hao wanasisitiza Krish alizaliwa kihalali ndani ya ndoa yao.
Tayari wawili hao, walishatangaza kuachana, ingawa Uwoya sasa ni kama amezinduka usingizini na kudai anampenda Kataut kuliko chochote na anaamini Mungu atainusuru ndoa yao kwa kumshinda Shetani anayewaroga.

No comments:

Post a Comment