NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, January 31, 2012

Mgomo wa madaktari wamkera RC Dodoma

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi amekerwa na mgomo wa madaktari na kuwataka viongozi wa madhehebu ya dini kusaidia kabla maafa makubwa kutokea.

Dk. Nchimbi alisema hayo juzi wakati wa mahafali ya 16 ya wanafunzi wa kidato cha sita katika
Shule ya Sekondari ya Jamhuri mjini Dodoma. Katika mahafali hayo, wanafunzi 354 walitunukiwa vyeti, wakiwemo wavulana 266 na wasichana 88.

Aliwataka viongozi wa madhehebu ya dini kwenda kwenye Hospitali ya Mkoa wa Dodoma
kuzungumza na madaktari kwani wanaofanya mgomo nao wana dini pia ni waumini wao.

“Muende Hospitali ya Mkoa wale madaktari ni waumini wenu, waulizeni hatua waliyoichukua inaendana na mahubiri wanayopata?” alihoji. Alisema hatua hiyo hailingani na maadili ya
kimungu kwa kuwa wagonjwa wanaotakiwa kutibiwa hasa wajawazito pia wanahitaji sana msaada wao.

“Hili si suala la kisiasa na linahitaji mikakati kulimaliza, wakumbusheni haya wanayofanya duniani watakutana nayo siku ya hukumu,” alisema. Mkuu huyo wa Mkoa ametuma salamu kwa Mbunge wa Dodoma Mjini na kumtaka atembelee shule hiyo kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge ili aone anaweza kujenga darasa lipi kutokana na shule hiyo kuwa na upungufu wa madarasa.

“Nakutuma Katibu wa Mbunge, tungependa Mbunge aje atembelee shule hii kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge ili aone ni darasa lipi anaweza kujenga,” alisema. Alisema kumekuwa na taarifa zisizo sahihi kuwa taasisi za dini hazitoi fursa sawa kwa wanawake lakini ukweli ni kuwa taasisi hizo zinatambua na kutoa fursa kwa wanawake.

Dk. Nchimbi alisema kuwa taasisi za dini zimekuwa zikitoa mchango mkubwa kwa Serikali na
Taifa na kuonyesha upendo mkubwa ambao thamani yake haiwezi kupimika.

No comments:

Post a Comment