NJOMBE

NJOMBE

Monday, January 16, 2012

Wajawazito Ileje wakwepa kujifungulia hospitali

WILAYA ya Ileje mkoani Mbeya imetajwa kuwa miongoni mwa wilaya nchini zinazotisha kwa wanawake wajawazito kutojifungulia hospitali na vituo vingine vya afya licha ya kuhudhuria kliniki katika kipindi chote cha ujauzito.

Hali hiyo imebainishwa na Meneja Uwezeshaji wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Dk. Mathias Sweya katika mkutano wa kupanua uelewa kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje juu ya mradi wa kuwasaidia wanawake wajawazito wasio na uwezo kupata huduma za matibabu chini ya utaratibu wa NHIF na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).

Dk. Sweya alitolea mfano kwa Kituo cha Afya cha Sange kilichopo wilayani hapa ambapo katika mwaka 2011 wanawake 137 walihudhuria kliniki kituoni hapo, lakini kati yao ni 34 pekee waliojifungua hapo.

Alisema uchunguzi unaonesha kuwa gharama za vifaa vinavyopaswa kununuliwa kwa mama mjamzito zinachangia kwa kiasi kikubwa wanawake kutojifungulia kituoni hapo.

Hata hivyo, mmoja wa maofisa maendeleo wilayani Ileje, Lucy Mwani akichangia hoja alisema yapo mambo mengi yanayopaswa kuchunguzwa ili kupata sababu ya wajawazito kutohudhuria kliniki ukiachilia mbali gharama akitaja baadhi kuwa ni pamoja na mila potofu.

Mwani alishauri kurejeshwa kwa Mpango wa Uhai, Ulinzi na Maendeleo ya Mama na Mtoto (CSPD) akisema uliwezesha kupatikana kwa taarifa za haraka juu ya mama mjamzito na mwenendo wa maisha yake tangu dalili za mimba hadi kujifungua pamoja na changamoto anazokumbana nazo.

No comments:

Post a Comment