NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, January 31, 2012

Madaktari ‘waidharau’ Serikali

JUMUIYA ya madaktari jana iliendelea ‘kuiendesha’ Serikali, tabia ambayo Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameiita dalili ya kuidharau Serikali, baada ya kukaidi kufika katika kikao chake cha majadiliano huku wakisubiriwa na mawaziri wengine sita pamoja na watendaji wengine wa juu serikalini.

Katika Ukumbi wa Karimjee, watendaji kadhaa wa Serikali na waandishi wa habari walikuwepo katika ukumbi huo kuwasubiri lakini hadi saa sita mchana hakukuwa na daktari hata mmoja aliyetokea.

Mawaziri hao ni pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia.

Wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi, Waziri wa Mamabo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha na Naibu Waziri wa Afya, Dk, Lucy Nkya. Watendaji wakuu serikalini ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, Mganga Mkuu wa Serikali, Deo Mtasiwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, wakuu wa Polisi na wakuu wa wilaya.

Ilipotimu saa sita na nusu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliwasili na kuzungumza na waandishi wa habari kuelezea uamuzi ya Serikali baada ya kuwaita madaktari hao mara kwa mara kuzungumza nao bila mafanikio.

Walivyoanza dharau

Alisema Januari 20 mwaka huu jioni, ujumbe wa watu sita ulifika ofisini kwake na kutaka kuonana naye lakini kutokana na kuwa na ratiba ya kwenda Arusha katika maziko ya Mbunge wa Arumeru, Jeremiah Sumari, alimtaka Lyimo na Dk. Nkya kuzungumza nao na kumjulisha akiwa Arusha.

Alisema katika mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Namala Mkopi, walifikia maelewano kurudi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuendelea na majadiliano ya madai yao ambapo walienda kesho yake na kufikia muafaka wa utaratibu wa kuyafanyia kazi.

“Hata hivyo, waliporejea kwa wenzao kutoa ripoti ya matokeo ya majadiliano na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, yalifanyika mapinduzi ya uongozi ikaundwa Kamati ya Mpito kushughulikia madai ya madaktari ikiongozwa na Dk. Stephen Ulimboka,” alisema Pinda.
Alisema alipotoka kwenye maziko alipokea maombi yao ya kuonana naye na kupangiwa siku iliyofuata yaani Novemba 24, mwaka huu, saa 11 jioni.

Pinda alisema madaktari hao hawakutokea huku namba za simu walizoacha kwa Katibu Mkuu zikiwa za waliopinduliwa na hawakuwa tayari kufika tena ofisini. Pinda alisema alipozungumza na wahariri wa vyombo vya habari Januari 25 mwaka huu, alitumia fursa hiyo kuwaomba waonane ili awasikilize na kutafuta ufumbuzi wa madai yao akiamini wangefanyia kazi ombi hilo baada ya kusikia katika vyombo vya habari.

“Pamoja na jitihada zote hizo, hakuna aliyekuwa tayari kufuata ushauri nilioutoa, kwa hiyo si kweli kwamba Serikali imetoa taarifa ya muda mfupi ya kutaka kukutana nao kama walivyodai na kunukuliwa na vyombo vya habari,” alisema Pinda.

Ushauri Tughe nao watupwa nje

Pinda alisema wakati wakiendelea na vikao vyao, alikutana na mawaziri kadhaa pamoja na viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Ramadhani Kiwenge na kukubaliana kutuma ujumbe wa Serikali ili ikawasikilize.

Alisema alituma ujumbe wa Serikali ukiongozwa na Dk. Mponda, Dk. Nkya na Ghasia kwenda kuonana nao kwenye ukumbi wa Hoteli ya Starlight Ijumaa iliyopita. Alisema katika mkutano huo yaliyotokea ni tabu kweli, kulikuwa na dalili za dharau huku wakipokewa kama siyo viongozi wao wakati waliwasilisha malalamiko yao kuomba kuonana naye.

Alisema kila mawaziri hao walipotaka kutoa maelezo ya malalamiko yao, waliandamwa na ghasia na waliporipoti kwake aliwataka kutokukata tamaa. “Lyimo aliwapigia simu juzi (Ijumaa iliyopita) asubuhi lakini hazikupokelewa ikabidi aende hadi katika Hoteli ya Starlight alipotafuta sana ili awaone lakini alibahatika kuzungumza na mwenyekiti wao tu.

“Walikataa ujumbe wangu niliompa Katibu Mkuu kwa madai hawataki kwa mdomo wanataka kwa barua, na aliponieleza nilimshauri asichoke akaandika barua na kuwapigia simu wakamtaka awapelekee karibu na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,” alisisitiza.

Alisema baada ya kupokea barua hiyo wakamwambia kuwa watamjibu na ilipofika juzi (Ijumaa iliyopita) saa tatu usiku walimpelekea barua ya kukiri kupata barua ya Waziri Mkuu na kutoa masharti matatu.

Pinda apewa masharti

Kwanza hawako tayari kukutana naye jana hadi leo ili kuwasubiri wenzao wa mikoani wahudhurie, pili Ofisi ya Waziri Mkuu iwajibu kwanza kwa maandishi madai yao kabla ya kukutana nao ili wapate nafasi ya kujadili hoja moja baada ya nyingine. Na tatu, walitaka Serikali itoe tamko wakati wa kuzungumza nao; kwamba haitatoa adhabu yoyote kwa daktari au mtumishi wa kada yeyote wa afya kutokana na mgomo huo.

Uwezekano wa kufikia muafaka

Pinda alisema kutokana na ukubwa wa mahitaji yao hawawezi kutekeleza mara moja, lakini kutokana na mzungumzo ikiwa wangekutana, wangefikia muafaka kwani uchumi wa nchi pia unaamua mambo mengi. Alisema kwa kutizama madai yao, ufumbuzi ungepatikana kwa mazungumzo na siyo kutoa amri ya kutaka ifanyike mara moja kama posho ya kulala kazini ambayo wanalipwa Sh 10,000 kweli ni ndogo wangeweza kuiongeza.

Alisema kwa dai la posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi, lingeweza kuangalia kwa makundi kwa wale wanaofanya kazi katika wodi za vichaa, katika mionzi na wengineo kwa kuwa inawezekana. Kuhusu uhaba wa nyumba, alisema uahaba huo upo kwa sekta nyingi hata polisi na wanajeshi, lakini kuna juhudi Serikali inafanya kwa kutambua hilo kwa kujenga nyumba 10 kwa kila wilaya katika wilaya 18 hivyo wangeweza kujadili kutoa posho bila kujali cheo.

Alisema kuhusu posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu Serikali inaelewa na ipo tayari kutoa posho katika ameneo yasiyo na mvuto kwa watumishi wa kada mbalimbali.
“Kama kuhusu usafiri, utaratibu wa kukopeshana magari upo serikalini, kama tungekutana tungeona namna ya kuwapa kipaumbele kwa wanaoishi maeneo yanayolazimu usafiri kwa kuwa mfuko huo hautoshi,” alisema.

Kuhusu bima ya afya, Pinda alisema ni jambo la kuangalia na kama fedha ipo, siyo mbaya kutibiwa maeneo mazuri na kuongeza kuwa alidhani wangetaka kutibiwa bure na familia zao katika hospitali wanazofanyia kazi. Alisema katika suala la mshahara siyo rahisi kutekelezwa kwa kiwango hicho kwa mtumishi wa umma kwani ni lazima ufahamike kuwa utumishi wa umma pia unatoa huduma, hivyo ni vyema kutambua kuwa wako wa kada mbalimbali ingawa wao ni muhimu lakini kuna haja ya kuwa na uwiano.

Pia alisema kutaka uongozi wote wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ujiuzulu, siyo jambo la msingi kwani hawakutoa sababu ya msingi na kama kucheleweshwa kwa posho ni suala la serikali siyo wizara. Alisema kama upo upungufu mwingine wasioujua serikalini hilo lingejadilika lakini kuweka uongozi huo wote wa Wizara katika kundi moja kwa tuhuma zisizojulikana siyo sawa.

Pinda alisema huduma duni kwa wananchi ni moja ya changamoto kubwa serikalini ikiwa ni sehemu ya changamoto nyingi zilizopo katika sekta mbalimbali ambazo Serikali wanafanyia kazi hatua kwa hatua.

Uongozi wa mgomo mamluki

Alisema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari hao inayoongoza mgomo, Dk. Stephen Ulimboka siyo mtumishi wa Serikali na hajasajiliwa kama daktari kwa kuwa usajili wake ulisitishwa na Baraza la Madaktari mwaka 2005 baada ya kuongoza mgomo wa madaktari nchi nzima.

Kwa mujibu wa Pinda, Ulimboka alihitimu Shahada ya Udaktari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2004 na kupata usajili wa muda wa baraza kisha kupangiwa mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Alisema Novemba mwaka 2005, alishitakiwa katika Baraza kwa Ukiukwaji wa Maadili ya Taaluma ya Udaktari kwa kuitisha mgomo ambao ni makosa kimaadili na kukataa kufika mbele ya baraza kujibu tuhuma hivyo shauri lake halikumalizika.

Pinda alisema mwaka 2006, Rais alimsamehe na kurejeshewa usajili wa Baraza na kuruhusiwa kuendelea na mafunzo ya vitendo lakini hakuna taarifa kama alimaliza mafunzo hayo kwa kuwa hajawasilisha cheti cha kumaliza mazoezi na haifahamiki anafanya kazi wapi ingawaje inasemekana anafanya katika taasisi isiyo ya kiserikali (NGOs) inayojihusisha na masuala ya Ukimwi.

“Katika kumpa taarifa za msamaha wa Rais, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Baraza la Madaktari kwa nyakati tofauti walimtaka kutojihusisha na mgomo au suala lolote ambalo ni kinyume cha maadili ya taaluma ya udaktari,” alisema Pinda. Alisema Ulimboka katika barua yake ya Februari 2, 2007 ambayo ipo serikalini alikiri kwamba hatajihusisha wala kutoa ushawishi wowote kwa wengine kufanya vitendo kinyume na maadili ya udaktari.

Akizungumza na gazeti hili, Ulimboka alikiri kuitwa na Baraza la Madaktari mwaka 2005 na kweli alikuwa kiongozi wa mgomo huo wa madaktari. Alisema mwaka 2007 alimaliza mafunzo yake ya vitendo katika Hospitalia ya Mwananyamala na kupewa cheti chake katika Hospitali ya Muhimbili alipofukuzwa kabla ya mgomo kama utaratibu ulivyo.

Alikana kuandika barua Serikalini na kumtaka Waziri Mkuu kama anayo, aiweke hadharani huku akikiri kutokuwa mtumishi wa serikali na kudai siyo sababu ya kumzuia kutopigania maslahi ya madaktari.

No comments:

Post a Comment