NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, January 17, 2012

Lema azidi kuikomalia mahakama


WAKATI shauri la kufanya kusanyiko lisilo halali linalomkabili Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema na wenzake 18 likiahirishwa hadi Februari 7, amelalamikia kadhia ya washtakiwa kutakiwa kufika mahakamani asubuhi na kusubiri hadi mchana kesi inapotajwa.

Lema na wenzake wanadaiwa Oktoba 28, mwaka jana walifanya kusanyiko lisilo halali, kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani Oktoba 31, mwaka jana Lema kwa hiari yake aliamua kwenda mahabusu.

Katika waraka wake, aliotoa muda mfupi kabla ya kupelekwa mahabusu, mbunge huyo alidai kufikia uamuzi huo kupinga uonevu na unyanyasaji wa polisi kwa kuwatuhumu kubambikia kesi viongozi, wanachama na wafuasi wa Chadema.
Wakili wa Serikali, Rose Sulle, alimweleza Hakimu Mkazi, Judith Kamara, kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo lipangiwe tarehe ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali ya makosa yanayowakabili.

Baada ya upande wa mashtaka kuomba shauri hilo kuahirishwa, Lema kwa niaba ya wenzake alitoa hoja ya kutaka mahakama kuzingatia muda na kwamba, washtakiwa wanahimizwa kufika saa 3:00 asubuhi, lakini kesi inasomwa mchana.
Alitoa mfano wa jana walipofika mahakamani saa 3:00, lakini shauri lao likaanza saa 5:30, huku wakilazimika kurandaranda katika viwanja vya mahakama kwa zaidi saa mbili na nusu kusubiri muda, ambao wangetumia kutekeleza majukumu mengine ya jamii.

Lema aliomba mahakama kupanga muda wa kesi baada ya kuangalia na kujiridhisha na shughuli za siku husika kulingana na kalenda yake, ili kuwatendea haki washtakiwa kwa kuwapunguzia muda wa kusubiri.

Kwa mara ya kwanza, Lema alitoa hoja kama hiyo Desemba 14, mwaka jana baada ya kulazimika kusubiri kwa zaidi ya saa tatu ndipo kesi yao iliposikilizwa licha ya wao kufika tangu saa 3:00 asubuhi.

Hakimu Kamara aliahidi kuwa mahakama itazingatia ombi hilo, lakini akieleza kuwa ni vigumu kutabiri muda utakaochukuliwa na kesi za madai ambazo zingine ziko hatua mbalimbali zinazopaswa kusikilizwa kabla ya zile za jinai.

“Kwanza hata sisi upande wa mahakama tunatamani sana kuwaondoa mapema, kwa sababu kila kesi yenu inapokuwapo hapa mahakamani, watu hufurika kwa wingi na kutatiza usikivu na baadhi ya taratibu za kawaida za mahakama,” alisema Hakimu Kamara.

No comments:

Post a Comment