NJOMBE

NJOMBE

clock

Saturday, January 21, 2012

Madaktari wakomaa wapiga hodi kwa Pinda

 BAADA ya vuta nikuvute baina ya madaktari wanaoendelea na vikao vya kutaka nyongeza ya posho na mishahara na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, hatimaye madaktari hao wametangaza kuisusa Wizara hiyo na kubisha hodi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, wakimwomba asikilize madai yao.


Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya juzi kutokea kutokuelewana baina ya Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya na madaktari hao baada ya kutofautiana juu ya mahali wanapotakiwa kuonana ili kujadiliana.


Wakati Dk. Nkya alikwenda katika ukumbi wa mikutano wa Arnatouglo Mnazi Mmoja ili kuonana na madaktari hao, wao walikusanyika ukumbi wa Don Bosco nao wakimsubiri.


Kutokana na hatua hiyo, madaktari hao chini ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), jana waliendelea na vikao vyao vya kudai nyongeza hiyo ya mishahara na posho wakiwa Don Bosco na baadaye Makamu wa Rais wa MAT, Dk. Primus Saidia alitangaza azma ya kukutana na Pinda ili kutafuta jibu la madai yao.


“Napenda kuwafahamisha kwamba baada ya jana (juzi) Naibu Waziri wa Afya kushindwa kukutana nasi, sasa tumeona Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii haina dhamira ya dhati ya kusikiliza hoja zetu.


“Naibu Waziri aliamua kwenda Arnatouglo kukutana nasi wakati hakukuwa na mawasiliano yoyote rasmi ya sisi kuonana naye kule, sisi tulikusanyika hapa (Don Bosco) kumsubiri, kwa vile tulikuwa na mawasiliano rasmi ya kuonana naye hapa.


“Baada ya kutafakari, sasa tumeona suala hili tulifikishe kwa Waziri Mkuu, kwani ndiye kiongozi pekee ambaye sasa tumeona anaweza kutusikiliza na kujibu hoja zetu. Hapa tunaandika barua rasmi kwenda kwa Waziri Mkuu. Rais wetu (Dk. Namala Mkopi) atakwenda kwa Waziri Mkuu na ataambatana na baadhi ya madaktari kati yetu,” alisema Dk. Saidia.


Alisema chama hicho kina imani kubwa na Waziri Mkuu Pinda, kuwa ana uwezo na utashi wa dhati wa kutatua matatizo yao kutokana na kuwa na uhusiano mzuri na chama hicho.


“Nikukumbusheni tu kwamba mara zote Waziri Mkuu amekuwa mtu makini na msikivu sana kwetu. Kama mtakumbuka Novemba mwaka jana Waziri Mkuu alifanya mazungumzo na viongozi wa MAT Mwanza alipokuwa kwenye hafla Chuo Kikuu cha Bugando. Baadhi ya mambo tunayoyatoa leo tulimpa wakati ule, hivyo anafahamu kwa dhati madai yetu,” alisema.


Gazeti hili jana jioni liliwasiliana na mmoja wa viongozi wa madaktari hao ambaye alisema Ofisi ya Waziri Mkuu, ilikuwa tayari imeanza kujibu hoja zilizowasilishwa na madaktari hao kupitia barua maalumu waliyomwandikia Pinda.


“Waziri Mkuu hataweza kuja, lakini ofisi yake imeanza kujibu hoja zetu na viongozi wetu wapo huko wanasubiri majibu tutakayojibiwa ingawa tuna imani kubwa ya kupewa majibu mazuri.


“Tumeambiwa kwamba huenda Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Peniel Lyimo) atakuja kuzungumza na sisi ili kutafuta muafaka. Uwezekano wa kuonana naye kesho (leo) ni mkubwa sana,” alisema kiongozi huyo wa MAT.


Kutoka Mwanza, Grace Chilongola, anaripoti kwamba MAT Kanda ya Ziwa imeiomba Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuacha malumbano na madaktari na badala yake isimamie matatizo yaliyopo ili kuboresha sekta ya afya.


Walitoa ombi hilo jana baada ya kikao cha pamoja kilichojumuisha madaktari wa Kanda ya Ziwa kilichokuwa kikiunga mkono madai ya madaktari wenzao wa Muhimbili.


Akizungumza Katibu wa MAT, Dk. Rodrick Kabangila alisema Serikali iangalie mambo ya msingi katika sekta ya afya kama ya milipuko ya surua inayoendelea kutokea wakati chanjo zinatolewa, ukosefu wa dawa na vifaa badala ya kuendeleza malumbano na madaktari.


Kabangila ambaye pia ni Mwenyekiti wa MAT, Kanda ya Ziwa alisema Serikali inapoendeleza malumbano na madaktari, inaamsha machungu ya madaktari ya siku za nyuma na kutaka kuyafanyia kazi madai yao ya mishahara, posho na kusomeshwa, ili waweze kufanya kazi pamoja.


Aidha, aliiomba Serikali kuangalia ugumu wa shule ya madaktari, gharama kubwa wanayosomea pamoja na changamoto wanazokumbana nazo kazini, kwa kuwalipa kile kinachostahili na si kusingizia kuwa Serikali haina fedha.


Dk. Godfrey Mbawala alisema madaktari hawataki wafikie kwenye mgomo, kwani itakuwa ni vita na watakaoathirika ni wananchi wenye wagonjwa hospitalini.


“Hofu ni kwa wagonjwa watakaokufa na kuziacha familia zao zikihangaika na ugumu wa maisha na ukiuliza sababu ni madaktari kulumbana na Serikali, inatia uchungu sana, hatutaki kufika huko,” alisema na kuiomba Serikali ichukulie suala la madai ya madaktari kwa uzito unaostahili.


Alisema jamii inapaswa kuwaunga mkono ili nao wasiathirike na mgomo unaoweza kutokea .


“Hatutaki kufikia mgomo kutokana na athari zake kuwa kubwa kiuchumi, kidini na kijamii, lakini kwenye mgomo tutafikishwa na Serikali iwapo itashindwa kutusikiliza,” alisema Dk. George Adriano.


No comments:

Post a Comment