NJOMBE

NJOMBE

Friday, January 20, 2012

Simanzi nyingine ndani ya Bunge

 SIKU mbili baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Regia Mtema (Chadema) kuzikwa, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Jeremiah Sumari (CCM) amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Baadhi ya viongozi akiwemo Rais Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge, Anne Makinda na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa jana walikwenda nyumbani kwa marehemu Mbezi Beach kutoa salamu za pole kwa ndugu na jamaa wa mbunge huyo.

Akitoa taarifa za msiba huo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema mbunge huyo aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, alifariki juzi saa nane usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alilazwa.

Alisema kutokana na msiba huo, ratiba ya vikao vya kamati za Bunge kwa siku ya jana ilivurugika ingawa kamati nyingine ziliendelea na shughuli kama kawaida.

“Hata hivyo, tutaendelea na kamati kesho (leo) kama kawaida hadi siku rasmi ya ibada na kumuaga marehemu,” alisema Dk. Kashililah.

Kwa mujibu wa mtoto wa kwanza wa Sumari, Sioi Sumari, ratiba ya msiba huo inaonyesha kuwa mbunge huyo, atazikwa rasmi nyumbani kwao Arumeru Mashariki siku ya Jumatatu na ataagwa jijini Dar es Salaam kesho na kusafirishwa kwenda Arumeru kesho kutwa.

Ingawa mtoto huyo alikataa kutaja ugonjwa uliokuwa ukimsumbua baba yake na kuwataka waandishi wa habari kwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupata taarifa hiyo, taarifa za Bunge baadae zilithibitisha kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa saratani ya ubongo.

Taarifa hizo zilieleza kuwa mwili Sumari utaagwa kesho katika viwanja vya Karimjee kuanzia saa 5 asubuhi na baada ya hapo atasafirishwa Jumapili asubihi kwenda kijijini kwao Akeri, Meru, mkoani Arusha kwa maziko yatakayofanyika Jumatatu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sumari alikuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na ugonjwa huo mwaka juzi alipelekwa nchini India kwa upasuaji na alirejea nchini na hali yake ilikuwa ikiendelea vizuri.

Hata hivyo mwishoni mwaka jana hali yake ilibadilika ghafla na kuanza kuwa mbaya na kurejeshwa nchini Januari, 9 mwaka huu na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo alifariki dunia usiku wa kuamkia jana.

Kutokana na msiba huo, shughuli za kamati za Jumamosi na Jumatatu zimesitishwa na zitaendelea tena Jumanne baada ya maziko.

Naibu Spika Job Ndugai kwa upande wake alisema ofisi ya Bunge imepokea kwa mshtuko taarifa za msiba huo ambao umetokea siku chache baada ya mbunge Regia kufariki kwa ajali ya gari hali ambayo alisema ni pigo kubwa kwa Watanzania.

“Kwa kuwa ni siku chache tu tangu utokee msiba wa Mheshimiwa Regia kila kitu kitakuwa kama ilivyofanyika katika msiba ule, hivyo kuna uwezekano mkubwa Sumari akaagiwa Karimjee,” alisema.

Alisema Kamati ya Bunge ya Uongozi inatarajiwa kukutana leo kupanga ratiba rasmi ya kuaga, ibada na mazishi ya Mbunge Sumari.

Wakizungumzia marehemu, Lowassa alisema amesikitishwa na kifo cha kiongozi huyo kwani pamoja na kwamba alikuwa mkwe wake lakini alikuwa ni rafiki yake mkubwa aliyetoa mchango wake kwa watu wa Arumeru.

“Wananchi wa Arumeru watamkumbuka kwa uchapakazi wake na uadilifu wake, kwa kweli Mkoa wa Arusha umepoteza kiongozi imara,” alisema.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa alisema marehemu alikuwa mtu anayependa ukweli na kufanyakazi kwa juhudi kubwa hata kama akiwa mgonjwa.

Alisema pamoja na hayo alikuwa akimpenda Mungu na ndiyo maana alikuwa mzee wa Kanisa.

“Pamoja na usomi wake alijishusha, alipenda kusali na alimpenda Mungu, tunamshukuru Mungu kwa kuwa Sumari amekufa katika mazingira ya kumtegemea na kumuamini Mungu,” alisema.

Marehemu aliyezaliwa mwaka 1943, ameacha mjane mmoja, watoto wanne; wakike mmoja na wa kiume watatu na wajukuu saba.

Kutokana na msiba huo, Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Makinda kutokana na kifo cha Sumari.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Mheshimiwa Sumari, alikuwa kiongozi aliyewatumikia vema wananchi wa Arumeru Mashariki na Taifa kwa ujumla katika wadhifa wake wa Waziri kwa umahiri na uhodari mkubwa,” alisema Rais Kikwete katika salamu zake.

Kutokana na msiba huo, wananchi wa Arumeru Mashariki wamepoteza kiongozi wa kutegemewa huku Taifa likiachwa na pengo kubwa ambalo si rahisi kuzibika ikizingatiwa kwamba alikuwa kiongozi katika Wizara ambayo ni mhimili muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu.

“Kwa dhati ya moyo wangu, natuma salamu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya Marehemu Sumari kwa kumpoteza kiongozi na mhimili madhubuti wa familia.

“Ninawahakikishia kwamba nipo pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa, na namuomba Mungu, mwingi wa Rehema aipumzishe roho ya Marehemu Sumari mahali pema peponi, amina,” alisema Rais Kikwete.

Ameiomba familia ya Marehemu Sumari kuwa na moyo wa uvumilivu na subira katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo ya mpendwa wao kwa kutambua kuwa yote ni mapenzi yake Mola.

No comments:

Post a Comment