NJOMBE

NJOMBE

Thursday, January 12, 2012

Dk. Mwakyembe mambo mazito



RIPOTI ya ugonjwa unaomsumbua Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk. Harrison Mwakyembe, imeendelea kuivuruga serikali, safari hii Wizara ya Mambo ya Ndani ikisisitiza kuwa Wizara ya Afya ndiyo inayopaswa kuzungumzia suala hilo.
Kauli hii mpya toka Wizara ya Mambo ya Ndani imekuja ikiwa ni takriban wiki moja tangu gazeti hilt lilipomuuliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni, kuhusiana na ripoti hiyo na kusema kuwa suala hilo haliwahusu.
Uamuzi wa Tanzania Daima Jumatano kutaka kupata kauli toka Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo kimantiki inashughulikia madai ya jinai ulikuja baada ya kile kinachodaiwa kuwa ripoti ya ugonjwa wa waziri huyo kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali maarufu ya Apollo nchini India ambayo hadi sasa imebaki kuwa siri, inadaiwa kueleza chanzo cha ugonjwa wa Dk. Mwakyembe kuwa umetokana na sumu kali aliyowekewa hapa nchini.
Gazeti hili jana lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, kutaka kupata kauli yake juu ya ripoti hiyo na tuhuma zinazotajwa ambapo alisema mwenye uwezo wa kuzungumzia juu ya ripoti hiyo ni Mkemia Mkuu wa Serikali toka Wizara ya Afya.
Alipoulizwa na gazeti hili anazungumziaje juu ya kile kinachodaiwa Dk. Mwakyembe kuwekewa sumu hapa nchini, Waziri Nahodha alijibu kwa sauti kali kidogo: “Aa..ah, sikiliza; wenye uwezo huo nimekwambia ni Wizara ya Afya, mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani kuzungumzia suala hilo ni mpaka niletewe taarifa kama mtu anatuhumiwa kwa sababu wizara yangu inashughulika na kesi za jinai.
“Sasa sijaletewa taarifa, mimi ripoti siijui, ripoti za afya za watu ziko Wizara ya Afya… hao si ndiyo wanawapeleka watu India?…Sijaletewa ripoti sijaiona na sidhani kama nitalewa,” alisema.
Alipoulizwa kwa nini anasema hadhani kama ataletewa ripoti hiyo je hakuna taarifa zinazodai kuwa ugonjwa unaomsumbua Dk. Mwakyembe unatokana na sumu? Bado aliendelea kusisitiza kuwa hajapokea taarifa zozote za mtu kutuhumiwa kumuwekea sumu Dk. Mwakyembe na kusisitiza kuwa kama gazeti hili linamfahamu mtuhumiwa huyo basi limtajie.
Hata hivyo ingawa taarifa rasmi ya serikali haijatolewa, ripoti ya ugonjwa wa waziri huyo kutoka kwa madaktari bingwa wa hospitali maarufu ya Apollo nchini India ambayo hadi sasa imebaki kuwa siri inadaiwa kupelekwa serikalini kupitia Wizara ya Afya.
Taarifa za Dk. Mwakyembe kuwekewa sumu, mara ya kwanza ziliibuliwa rasmi nchini na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, ambaye ni rafiki mkubwa na mshirika wa karibu wa Dk. Mwakyembe katika mapambano dhidi ya ufisadi nchini katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ITV katika kipindi chake cha dakika 45 kilichorushwa mwaka jana.
Sitta alisikika akisema kuwa wasiwasi huo wa Dk. Mwakyembe kuwekewa sumu unatokana na mabadiliko ya ngozi na nywele alivyoondoka navyo nchini kwenda India.
Kwa Mujibu wa Sitta ambaye ni Mbunge wa Urambo Mashariki (CCM), alisema alipokwenda kumwona Dk. Mwakyembe nyumbani kwake, alipata mshtuko mkubwa kwani ilikuwa ni mara yake ya kwanza katika umri alionao kushuhudia ngozi ya mtu ikitoa unga.
Sitta alikaririwa akisema, “Kuna kitu kama mba kwenye nywele na kwenye ngozi ya Dk. Mwakyembe. Akishika hivi, baadhi ya nywele zinadondoka. Mkono umevimba, sehemu mbalimbali. Mke wake alichukua video. Alikuwa anatuonyesha kwenye laptop (kompyuta ndogo). Kwa kweli inatisha.”
Hata hivyo, Sitta alihojiwa na polisi kuhusiana na taarifa hiyo kwa madai kuwa ingeweza kuhatarisha amani, lakini alipotakiwa kutoa ushahidi anadaiwa kutoa ushahidi wa habari za kwenye mitandao ya kijamii.
Kabla ya Dk. Mwakyembe kwenda India kutibiwa, kulikuwa na uvumi kwamba kuna uwezekano mkubwa kwa kiongozi huyo kulishwa sumu, ingawa yeye binafsi hajakanusha wala kuthibitisha habari hizo.
Katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu aliporejea nchini, Dk. Mwakyembe alisema ripoti ya ugonjwa wake iko serikalini.
Hata hivyo, serikali hadi sasa imekataa kuitoa hadharani ripoti hiyo ya madaktari bingwa wa Hospitali ya Apollo, India, waliomtibu Dk. Mwakyembe.
Habari zaidi zinasema kuwa mwanasiasa huyo amepania kuianika ripoti hiyo hadharani kama serikali itaendelea kuifanya kuwa siri.
Mwakyembe alipelekwa India Oktoba 9 mwaka jana na kurejea nchini Desemba 11 mwaka jana hata hivyo licha ya kupata matibabu nchini India na kuendelea na tiba hiyo hapa nchini, hali yake bado siyo ya kuridhisha kwani amenyonyoka nywele, kope, nyuzi na hata vinyweleo vyote mwilini.

No comments:

Post a Comment