NJOMBE

NJOMBE

clock

Monday, January 30, 2012

Serikali yageuka mbogo

•  Madaktari wasema hawataenda kazini, kesho kukutana

SERIKALI imetangaza kuwafuta kazi madaktari wote watakaoendelea na mgomo huku ikiviamrisha vyombo vya dola kuwakamata watakaodiriki kufanya mikutano kwenye maeneo mbalimbali.
Msimamo huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Karimjee na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jana mara baada ya madaktari kushindwa kufika kwenye mkutano ulioandaliwa kuzungumzia madai na mgomo wa wataalamu hao.
Pinda aliwaamaru madaktari wanaoendelea na mgomo katika mikoa saba nchini kurejea kazini mara moja leo asubuhi huku akiweka wazi watakaokiuka agizo hilo watapoteza ajira zao.
Alisema serikali inatambua madaktari hao wanaongozwa na kamati ya mpito isiyotaka suluhu licha ya juhudi zilizofanywa za kuwaita kushughulikia madai husika.
“Serikali tayari imechukua tahadhari ya kukabiliana na hali hii kwa kuagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupeleka madaktari wake katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini. Kwa hiyo huduma zitaendelea kama kawaida,” alisema Pinda.
Katika mkutano huo Pinda aliongozana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya; Waziri wa Nchi Ofsi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia; Waziri wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Shamsi Vuai Nahodha; na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika.
Akionekana kukerwa na kitendo hicho cha madaktari hao kushindwa kukutana naye, Pinda alisema kuanzia leo ameviagiza vyombo vya dola kuzuia mikutano yote ya madaktari hao, akisema ni kinyume cha sheria ingawa serikali ilikuwa ikiwavumilia tu.
“Mgomo wao si sahihi kwa sababu haukufuata taratibu za kuuitisha. Wao walipaswa kutangaza mgogoro na kisha kutoa notisi ya siku 60, jambo ambalo hawakufanya,” alisema Pinda na kukipongeza Chama cha Wafanyakazi wa Afya na Serikali Kuu (Tughe) kwa kutambua hoja za madaktari hao lakini wakasema njia iliyotumika si sahihi.
Pinda ambaye aliwasili ukumbuni hapo saa 6:12 mchana badala ya saa 4:00 kama ratiba ilivyokuwa, alianza kwa kufafanua chimbuko la mgomo huo na hatua kadhaa zilizochukuliwa na serikali kuutatua.
Alisema tangu mwishoni mwa Desemba mwaka jana, kulikuwa na madai ya wataalamu mbalimbali waliokuwa kwenye mazoezi kwa vitendo (interns) kwamba wangeitisha mgomo kwa sababu ya kucheleweshewa posho zao; alisema juhudi zilifanyika na wakalipwa madai hayo yaliyokuwa yakifikia sh milioni 876.
Waziri Mkuu aliongeza kuwa baada ya malipo kufanyika, mgogoro ulihama kutoka kwa interns na kuwahusisha wataalamu wa kada nyingine za afya wakiwemo madaktari na kwamba kwa kuwa interns hao nafasi zao zilikuwa zimezibwa wakati wakiwa wamegoma, serikali iliona ni vyema kuwasambaza kwenye hospitali nyinge jijini hapa.
“Uhamisho huo ulifanywa kwa nia njema ila wenzetu waliutafsiri kama adhabu ya kuwakomoa interns hao na kupitia Chama chao cha Madaktari (MAT), walileta madai kuwa tuwarejeshe Muhimbili wakitoa sababu nyingi ambazo kimsingi tuliona zina mantiki,” alisema Pinda.
Aliongeza kuwa wakati wakiwa kwenye majadiliano ya hoja hiyo na yeye kuonyesha nia ya kukutana nao, MAT walienguliwa na jukumu hilo kupewa Jumuiya ya Kamati ya Mpito iliyoongozwa na Dk. Stephen Ulimboka, ambayo ilitoa madai nane.
Katika madai yao walitaka posho ya kulala kazini ya sh 10,000 kwa siku, ilipwe kwa kiwango cha asilimia 10 ya mshahara wa mwezi, posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi iwe asilimia 30 ya mshahara wa mwezi; na posho ya nyumba walipwe asilimia 30 ya mshahara wa mwezi.
Madai mengine ni kupandishwa kwa posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu zifikie asilimia 40 ya mshahara, kupatiwa posho za usafiri kwa asilimia 10 ya mashajara iwapo itashindikana wapatiwe usafiri wa kwenda na kurudi kazini.
“Wanadai mshahara wa sh 700,000 ni mdogo sana kwa daktari anayeanza kazi, hivyo wanapendekeza alipwe sh 3,000,000 kwa mwezi. Wanataka kupatiwa bima ya afya pamoja na familia zao kwa kupewa kadi za kijani na wanataka interns warejeshwe Muhimbili bila masharti yoyote,” alisema Pinda.
Hata hivyo, akichambua madai hayo alisema serikali haiwezi kuyapatia ufumbuzi mara moja madai hayo ila taratibu za kuyapatia ufumbuzi zinaendelea huku akikanusha kuwa daktari anayeanza kazi analipwa sh 700,000 bali ni sh 957,7000.
Alisema madaktari hao wamependekeza wanaoajiriwa hivi sasa walipwe mshahara wa sh milioni 3.5 wakati watumishi wa kada nyingine kama wahandisi wanaanza na sh 600,000 na wahasibu wanaanza na mshahara wa sh 300,000; kwamba posho zote wanazodai zikijumuishwa zinafikia asilimia 120 ya mshahara wa daktari mmoja.
“Kwa mujibu wa mapendezo yao ina maana kiwango cha kuanzia mshahara wa mhudumu wa afya kitakuwa sh 670,316 na mshahara wa juu utakuwa sh mil. 8.1 kwa mwezi. Utekelezaji wa pendekezo hili utagharimu sh bil 83.5 kwa mwezi ambayo ni sawa na sh bil. 417.5 kwa kipindi kilichobaki cha miezi mitano,” alisema.
Pinda alifafanua kuwa kwa mujibu wa mapendekezo hayo mshahara na posho, daktari anayeanza kazi atapata sh mil. 7.7 na daktari mshauri mwandamizi atapata sh mil. 17.2 kwa mwezi.
“Endapo madai hayo yatatekelezwa kwa mwaka mmoja jumla ya mishahara yao itakuwa sh bil. 799.7 badala ya sh bil. 222. 2 hadi kufika Juni 2012.
Kiongozi wao si daktari
Katika hatua nyingine, Pinda alisema kuwa katika uchunguzi wao walibaini kuwa kiongozi wa mgomo, Dk. Ulimboka alihitimu shahada ya udaktari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 2004 na kupata usajili wa muda No. 2022 wa Baraza la Madaktari mwaka huu na kupangiwa internship Muhimbili.
Alisema kuwa Novemba 2005, aliongoza mgomo wa madaktari nchini na usajili wake ulisitishwa na kushtakiwa mbele ya baraza hilo kwa ukiukaji wa maadili ya taaluma ya madaktari kwa kutishia na kufanya mgomo.
Mwaka 2006 Rais alimsamehe na hivyo kurejeshewa usajili na baraza na kuruhusiwa kuendelea na internship.
“Katika kumpa taarifa za msamaha wa Rais, Wizara ya Afya na Baraza la Madaktari walimtaka Dk. Ulimboka kutojihusisha na migomo au suala lolote kinyume na maadili ya udaktari ambapo Februari 2, 2007 alikiri sharti hilo kwa maandishi.
Hadi sasa hakuna taarifa kama alimaliza internship kwa kuwa hajawasilisha cheti cha kumaliza mazoezi hayo na hatuna taarifa anafanya kazi wapi ila si mtumishi wa serikali na hajasajiliwa kama daktari, alisema Pinda.
Dk. Ulimboka anena
Mwenyekiti wa Kamati ya Muda ya Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka, alisema hakuna sheria ya kumfukuza mfanyakazi asiyeenda kazini kwa siku moja na hivyo kuwataka madaktari waendelee kukaa nyumbani.
Alisema leo wanafanya taratibu za kisheria ili kesho wakutane kuzungumzia mgomo huo ambao sasa serikali inaonekana kutaka kutumia nguuvu kuwasambaratisha.
Alibainisha kuwa sababu ya wao kushindwa kwenda kukutana na Waziri Mkuu jana ni kuchelewa kupata barua ya wito wa kuitwa kwenye mkutano.
“Sisi tulipata barua saa 11 jioni na tukaandika barua kumjibu Pinda kuwa hawawezi kukutana leo kwa kuwa wenzao wengine wameshatawanyika, pia tulifanya hivyo kwa kuwa jana tulitarajia wenzetu kutoka mikoani wangewasili Dar es Saalam.”
Kuhusu kutohitimu mafunzo ya udaktari, alisema huo ni uongo kwa kuwa alimaliza mafunzo kwa vitendo katika Hospitali ya Muhimbili na kutunukiwa cheti chake cha udaktari mwaka 2007.

No comments:

Post a Comment