NJOMBE

NJOMBE

Tuesday, January 31, 2012

Madaktari rudini kazini - Pinda aagiza


SERIKALI imewaagiza madaktari wote walio katika mgomo kurejea kazini leo asubuhi na asiyeripoti atakuwa amepoteza ajira serikalini.

Uamuzi huo wa Serikali umetolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, katika mkutano na waandishi wa habari katika viwanja vya Karimjee baada ya madaktari hao kususa kukutana naye kuzungumzia malalamiko yao.

Pinda pia amewaagiza wakuu wa mikoa, wilaya na waganga wakuu katika hospitali zote nchini kukagua watumishi wao leo na asiyekuwepo kazini jina lake lipelekwe ashughulikiwe.

Alisema Serikali tayari imechukua tahadhari ya kukabiliana na hali hiyo kwa kuagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kupeleka madaktari kutoka katika Majeshi ya Ulinzi na Usalama katika hospitali za mkoa wa Dar es Salaam, ili kusaidia wagonjwa walioko hospitalini.
Waziri Mkuu pia ameagiza vyombo vya dola kuzuia mikutano yoyote ya madaktari hao inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Wamegoma suluhu

Pinda alisema katika hatua iliyofikiwa, Serikali imetambua kwamba madaktari wanaongozwa na Kamati ya Mpito, hawataki suluhu kwa kuwa imefanya juhudi za kuwaita kwa kuwabembeleza ili kujadili na kushughulikia madai yao bila mafanikio. Alisema baada ya kuwabembeleza kwa muda mrefu ili kupata suluhu ya tatizo hilo bila mafanikio, wameona wasiendelee na mgogoro na kuonekana Serikali haina maana kwani watu wanaumia na madaktari hawataki mazungumzo.

Pinda amekiri kuwa atakabiliwa na changamoto, lakini akasema bora kushughulikia changamoto hiyo mpya kuliko kuendelea na iliyopo sasa. Alisema mbali na kuomba madaktari kutoka jeshini, Serikali pia imewaoamba madaktari wenye utu na ubinadamu kuendelea kutoa huduma wakati jitihada za kuwatafuta madaktari wengine katika taasisi binafsi zikiendelea.


Madai yao kushughulikiwa

Alisisitiza kuwa licha ya uamuzi huo, amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia kuendelea kushughulikia malalamiko ya madaktari hao na kwa yale yanayowezekana yaingizwe kwenye bajeti ijayo ili kuwasaidia watakaokuwepo kazini.

“Madaktari hawa wamefanya kinyume kwa mujibu wa kiapo na sheria za nchi zinazowaagiza wazi kutojihusisha na migomo, hususani katika sekta yao ambayo inahusu uhai wa binadamu kwa kuwa husababisha kupoteza maisha bila sababu,” alisema.

Mikoa 14, wilayani shwari

Waziri Mkuu alisema tangu mgomo uanze, Serikali imekuwa ikifuatilia kutoka katika mikoa yote na hadi kufikia juzi, katika mikoa 14 hospitali za mikoa na za wilaya hazikuwa na mgomo.
Mikoa hiyo ni Ruvuma, Lindi, Mtwara, Shinyanga, Arusha, Tabora, Kagera, Iringa, Mara, Pwani, Kigoma, Singida, Manyara na Rukwa.

Alisema katika mikoa saba, baadhi ya hospitali za mikoa zilikuwa katika mgomo huku hospitali za wilaya zote za mikoa hiyo, zikiendelea kutoa huduma kama kawaida. Mkoani Kilimanjaro Pinda alisema mgomo ulikuwepo katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC ambao ulihusu madaktari waliopo katika mafunzo kwa vitendo.

Mbeya Pinda alisema mgomo ulikuwa kwa madaktari 65 walioko katika mafunzo kwa vitendo, madaktari kumi waliosajiliwa na madaktari bingwa kumi. Hospitali nyingine zilizogoma ni za Mkoa wa Mwanza ambako hata hivyo hakukuwa na mgomo wa wazi licha ya madaktari 46 wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kutoa tangazo la wazi la kushiriki mgomo, lakini dalili za mgomo zikionekana kwa waliopo katika mafunzo ya vitendo.

Alisema Morogoro waligoma madaktari katika Hospitali ya Mkoa wakati Tanga watumishi wote wa kada zote katika Hospitali ya Mkoa ya Bombo walikuwa na mgomo wa chini chini na Dodoma katika Hospitali ya Mkoa na Dar es Salaam mgomo huo ulipoanzia.

Mshahara na mlolongo wa posho wanazodai

Pinda alisema katika barua ya madaktari hao ya Januari 27 mwaka huu kwake, walitoa madai nane wakitaka mshahara wa daktari anayeanza kazi kuwa Sh milioni 3.5 kwa mwezi.
Kwa sasa katika madai hayo walidai wanalipwa Sh 700,000 lakini Pinda alisema wanalipwa Sh 957,700 na ndio wanaoongoza kwa malipo mazuri katika sekta ya umma. Wanaofuata kwa mujibu wa Pinda ni wahandisi Sh 600,000 na wahasibu kati ya Sh 300,000 hadi Sh 400,000.

“Uamuzi wa kuwawekea mshahara mkubwa madaktari ni wa makusudi kwa kutambua umuhimu wao katika kubeba maisha ya watu, inawezekana haitoshi lakini nyongeza ya posho kwa asilimia mia na ishirini hakuna Serikali inayoweza kuongeza,” alisema.

Mbali na mshahara huo, madaktari hao kwa mujibu wa Pinda, wamependekeza kulipwa posho ya kulala kazini ya asilimia 10 ya mshahara wa mwezi. Kwa sasa wanalipwa Sh 10,000 kwa siku. Pia wametaka posho ya kufanya kazi katika mazingira hatarishi asilimia 30 ya mshahara wa mwezi na posho ya nyumba asilimia 30 ya mshahara au wapewe nyumba.

Madaktari hao pia wamependekeza walipwe posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu iwe asilimia 40 ya mshahara na posho ya usafiri asilimia 10 ya mshahara au ikishindikana wakopeshwe magari. Baada ya mlolongo huo wa posho, madaktari hao ndio wakaweka pendekezo la kutaka madaktari waliokuwa katika mafunzo ya vitendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, warejeshwe mafunzoni hospitalini hapo.

Kipato cha Sh milioni 17

Pinda alisema kwa mujibu wa mapendekezo ya madaktari hao, akilipa mshahara wa Sh milioni 3.5 kwa mwezi na posho hizo, daktari anayeanza kazi atalipwa Sh milioni 7.7 kwa mwezi na Daktari Mshauri Mwandamizi atalipwa milioni 17.2 kwa mwezi.

Alisisitiza kuwa ili kutekeleza pendekezo hilo, Serikali italazimika kurekebisha viwango vya mishahara kwa watumishi wote wa kada ya afya na nyingine, ili kuweka uwiano kufuatana na muundo katika utumishi wa umma. “Kwa kuzingatia ukubwa wa gharama hizi, utekelezaji wa mapendekezo ya madaktari utakuwa hauwezekani kwa kuzingatia hali halisi ya bajeti ya Serikali,” alisema Pinda.

Alisisitiza kuwa madai yao ni sawa na nyongeza ya Sh bilioni 301.7 katika bajeti ya mshahara ya mwaka 2011/ 2012 ukijumlisha na nyongeza ya posho kwa watumishi wengine wa kada ya afya kwa miezi mitano iliyobaki, watapaswa kulipwa posho ya Sh bilioni 84.3.

Pinda alisema katika makundi hayo mawili tu; mishahara na posho Serikali itajikuta ikitoa Sh trilioni 2, ambayo ni zaidi ya theluthi mbili ya mishahara ya wafanyakazi wote serikalini ambayo kwa sasa ni Sh trilioni 3.45. Kwa maana hiyo, Pinda alisema madaktari wanataka wapewe theluthi mbili za mishahara ya wafanyakazi wote na waliobakia, wagawane theluthi moja iliyobakia jambo ambalo haliwezekani.

No comments:

Post a Comment